Sunny Safaris waishi kwa bahshishi

Wafanyakazi 23 wa Kampuni ya Utalii ya Sunny Safaris ya jijini Arusha, wamelalamikia uongozi wa kampuni hiyo kwa kufanya kazi bila mikataba na kunyimwa mishahara kwa miaka miwili. Wanadai kuwa uongozi wa kampuni hiyo umekuwa ukiwafanyisha kazi kwa saa nyingi bila malipo ya ziada, huku wakiendelea kukosa mishahara kwa madai kuwa kampuni haina fedha. Wafanyakazi hao ni madereva wanaoongoza watalii wanaotembelea vivutio vya utalii Kanda ya Kaskazini. Wanasema wameelezwa na mwajiri kuwa hawawezi kulipwa kwa kuwa wanapata ‘asante’ [bahshishi] kutoka kwa watalii. Madereva hao waongoza watalii (Tour Guides) ndiyo ‘roho’ ya sekta ya utalii kwa kuwa huwaongoza na kuwapeleka katika vivutio mbalimbali, hivyo kuwa mabalozi muhimu wa kuitangaza nchi na vivutio vyake kwa wageni. Mamlaka zinazopaswa kuwasaidia wafanyakazi hao mkoani kuanzia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Idara ya Kazi na Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF) zinaonekana kuungana katika kuwakingia kifua waajiri hao kwa kupuuza kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya mwajiri. Wafanyakazi hao wanasema kwa miaka miwili sasa wanafanya kazi bila mikataba inayoeleweka, hawalipwi mishahara wala posho stahili na kila wanapodai haki zao wamekuwa wakitishiwa kufukuzwa kazi. Wakizungumza na JAMHURI kuhusu sakata lao, wawakilishi wa wafanyakazi hao ambao wanahofu kujulikana kupitia vyombo vya habari, wanadai kuwa wamezunguka katika ofisi hizo za Serikali kwa miezi zaidi ya miwili sasa, na kila wanapofika wanashauriwa warudi waelewane na mwajiri wao. Wakiwa na barua ya malalamiko waliyoiandikia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Aprili 15, mwaka huu, wanasema wamefanya kazi katika kampuni hiyo kwa vipindi tofauti. Wanasema kuwa matatizo ya kutolipwa mishahara yalianza mwaka 2016 na wamekuwa na malimbikizo makubwa, huku mwajiri wao akiendelea kuwapiga danadana na kutoa ahadi zisizotekelezeka. “Kila tukimfuata bosi kuhusu mishahara yetu anatupiga danadana, na kwamba eti hali ya kampuni kipesa ni mbaya hivyo tuendelee kusubiri na tui
shi kwa tip (bahshishi) ambayo hutolewa na mgeni kwa hiari yake na haina kiwango maalumu. “Unawezaje kumnyima mshahara kwa miaka miwili mfanyakazi aliyetimiza wajibu wake eti kwa sababu anapewa ‘tip’ na mgeni? Wageni wengine hawatoi ‘tip’ na bosi analijua hilo, kwa nini anatufanya tuishi katika mazingira magumu na ya udhalilishaji kama haya wakati tuna vyombo vya Serikali ambavyo havitaki kutusaidia?” Amehoji kiongozi wa wawakilishi wa wafanyakazi hao. Madai yao makuu, kwa mujibu wa barua hiyo (nakala tunayo), ni mikataba ya ajira isiyoeleweka, kunyimwa mishahara kwa miaka miwili, kubaguliwa katika kulipwa mishahara, michango yao kutowasilishwa NSSF, kufanya kazi bila kuzingatia muda wa kazi uliowekwa kisheria na kulipwa posho ndogo isiyolingana na ugumu wa kazi, gharama za maisha na muda mrefu wanaotumikishwa. Wanasema wafanyakazi wa kampuni hiyo wamegawanywa katika idara kuu tatu ambazo ni Utawala, Karakana na Madereva, lakini katika ulipaji wa mishahara ni madereva tu wanaonyimwa.Wanasema hata wakati walipokuwa wakilipwa mishahara, hawakupewa hati inayoonesha kiasi cha mshahara na makato zikiwamo kodi za Serikali na makato ya NSSF (salary slip). Wanasema wamekuwa wakisaini katika karatasi za malipo ya kawaida (petty cash); jambo ambalo wanasema wamelilalamikia kwa muda mrefu bila mafanikio. “Kuna wafanyakazi kama 15 katika Idara ya Utawala na wengine 50 wako gereji, ukichanganya na sisi 23; kuna wafanyakazi kama 90 hivi, lakini hakuna hata mmoja anapewa ‘salary slip’ na wote tunasainishwa katika petty cash kila tulipokuwa tunalipwa mishahara,” wanadai wawakilishi hao. Wanasema Machi 30, mwaka huu mwajiri wao huyo aliwapa hundi za malipo ya malimbikizo ya mishahara yao kwa maelekezo kwamba waende kuchukua fedha hizo Aprili 15, mwaka huu lakini zote zilikataliwa benki kwa kuwa hakukuwa na fedha katika akaunti. Hatua ya mwajiri kuwapa hundi, ambayo wanasema si ya kawaida, wanadai ilitokana na kuwapo kwa ziara ya Rais John Magufuli mkoani Arusha mwanzoni mwa Aprili, mwaka huu. Hatua hiyo, wanasema iliibua hofu kwamba pengine wafanyakazi hao wangeandamama, au wangefikisha suala lao kwa Rais. “Alifanya hivyo ili akibanwa aweze kujitetea kuwa tumelipwa wakati akijua kuwa hakuna hela benki,” wamesema.
OFISI YA MKUU WA MKOA Wafanyakazi hao wamepeleka malalamiko na vielelezo katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha, na nakala kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, lakini wakati wakisubiri kujibiwa barua yao walipigiwa simu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakitakiwa wafike mkoani kuonana na bosi wao, ambaye hata hivyo hakutokea siku waliyopangiwa. Wanasema mwajiri wao huyo alienda mwenyewe siku iliyofuata na kukutana na maofisa wawili wa Kitengo cha Malalamiko mkoani hapo waliojulikana kwa majina ya Mhando na Hellen. Baada ya kikao cha mwajiri na maofisa hao, wafanyakazi walipigiwa simu wakitakiwa wafike ofisini kwa mwajiri wao Mei 5, mwaka huu ambako kutakuwa kikao kati yao, mwajiri wao na maofisa hao wa mkoani. Wanadai kuwa katika kikao hicho cha pande tatu, mwajiri alikiri kutowalipa mishahara na akatoa tamko kwamba atawalipa baada ya wiki mbili, lakini hakuna utekelezaji wa ahadi hiyo hadi sasa [wiki iliyopita]. “Baada ya wiki mbili alizoahidi bosi wetu kutulipa kupita bila ya kulipwa chochote tulianza kufuatilia mkoani, lakini bahati mbaya sana kila tukiwapigia simu wanadai wako kwenye vikao na hata tulipofika ofisini kwa Hellen alitujibu kuwa hana nafasi ya kuonana na sisi na atatupigia akipata nafasi,” wanasema. JAMHURI lilipofika Ofisi ya Malalamiko, ilizungumza na Hellen ambaye ndiye anayesikiliza malalamiko ya wananchi, na akakiri kuyatambua malalamiko ya wafanyakazi hao na kukutana nao, lakini akaanza kumtetea mwajiri kwamba ana mdororo wa kiuchumi, hivyo apewe muda atawalipa wafanyakazi madai yao. “Ni kweli tulikutana nao na kuzungumzia mishahara yao, lakini wote tunajua kwamba hali ya uchumi si nzuri kwa sasa na wafanyakazi wanaelewa hilo, hivyo wavute subira watalipwa malimbikizo yao baada ya ‘high season’ (msimu wa utalii) kuanza,” amesema Hellen. Ameulizwa kama kinachofanywa na mwajiri huyo ni sahihi, ilhali waongoza utalii wake wakisema mwaka mzima wamekuwa wakipokea watalii hasa kutoka Ujerumani bila kujali msimu, Hellen amesema hayo ni mambo ya kawaida katika biashara. “Biashara ya utalii ni sawa na biashara nyingine. Kuna wakati msimu unakuwa mzuri na wakati mwingine unakuwa mbaya, hivyo tunawashauri waendelee kuvumilia, watalipwa tu malimbikizo yao,” amesema. Ameulizwa iwapo mwajiri atashindwa kulipa hata baada ya msimu
kuanza kwa kuwa kuna misimu miwili imepita na hakuweza kuwalipa, Hellen amejibu kuwa ikitokea hivyo atawashauri wafanyakazi waende mahakamani kudai haki zao. Kuhusu Serikali kukosa kodi zinazokatwa katika mishahara ya wafanyakazi hao, Hellen amekiri, “Ni kweli Serikali inakosa kodi zinazostahili kukatwa katika mishahara ya wafanyakazi hao, lakini wa kufuatilia hilo ni Labour (Idara ya Kazi).”
KAULI YA NSSF Meneja wa NSSF mkoani Arusha, Dk. Frank Maduga, amekiri kampuni hiyo kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati, lakini amesema kuwa wamewasiliana na uongozi na kukubaliana namna ya kulipa malimbikizo hayo. Kuhusu kampuni hiyo kutoa hundi isiyo na fedha benki ya Sh milioni 30, Dk. Maduga anasema; “Hayo ni mambo ya kawaida, inawezekana kulikuwa na makosa ya kibenki, lakini tumewapa muda warekebishe kasoro na wakishindwa tutawafikisha mahakamani.” Akizungumzia tuhuma kwamba baadhi ya wafanyakazi wa NSSF wanapewa ofa ya kutembelea hifadhi za wanyama na uongozi wa kampuni hiyo, Dk. Maduga amesema kuwa kiofisi hakuna kitu kama hicho, lakini kama inatokea mtu binafsi anapewa fursa, hilo linabaki kuwa makubaliano ya watu binafsi na ofisi haihusiki.
MKURUGENZI MTENDAJI WA SUNNY SAFARIS Akizungumzia madai ya wafanyakazi wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sunny Safaris, Firooz Seleman, amekiri kudaiwa malimbikizo ya mishahara, lakini akasema kuwa tayari ameshaanza kuwalipa kwa awamu na waliobaki atamaliza kuwalipa wakati wowote baada ya msimu wa utalii kuanza. Msimu wa utalii huanza Julai mosi kila mwaka.