nyerere_karume_union_day copyTunaingia mwaka wa 16 bila ya kuwa na Mwalimu Nyerere. Oktoba, 14; Jumatano, 2015 siyo muda mfupi, lakini nchi hii bado inamkumbuka sana Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu, roho ya mzee wetu ipumzike kwa amani – Amina. 

Mwaka jana katika siku namna hii, Gazeti la Jamhuri, toleo maalum lilikuwa na kichwa cha habari “Watoto wa Nyerere wanena” tukasoma maelezo ya dada Anna Watiku uk. 3 na maelezo ya kaka Andrew Burito uk. 4 katika kila ukurasa kuliwekwa picha ndogo ya Baba wa Taifa katika mavazi rasmi ya Mkuu wa JKT kama yalivyovaliwa na wakurugenzi akina Nkulila, Kaswende na Gama. Picha ile katika kila ukurasa ilitusisimua sisi tuliokuwa viongozi wa JKT kuona alivyolipenda Jeshi hili na ubunifu wa Chama chake cha TANU.

Nami nilihabatika kutoa Makala yenye kichwa “Mwalimu Nyerere alinifundisha biolojia na historia” kwenye kurasa 12 – 13. Nilipokea meseji kadha zenye maoni tofauti. Wengine walifurahia wengine walinikosoa kuwa mimi ni shabiki sana wa CCM  na hasa natumia semi za Baba wa Taifa kuijengea uhalali Chama Tawala kwa vile kilianzishwa na Mwalimu wangu. Katika tafakari ya meseji zile nilikumbuka kuwa hapo zamani za Bwana Yesu, watu walimsema sana hata ikafika wakati Yesu aliwachukua wanafunzi wake mahali pa faragha panapoitwa Kaiseria Filipi (Caesarea Phillipi) na hapo tunasoma katika maandiko aliwauliza wanafunzi wake”, je makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani? Wakamjibu wakasema, “Yohanne Mbatizaji, lakini wengine Eliya, na wengine kwamba mojawapo wa Manabii wa kale amefufuka” (Luka sura 9 mistari ile ya 18 – 19). 

Nimefarijika na maneno haya, maana ile tabia ya watu kusemasema  haikuanzia leo bali toka enzi za watu wa kale watu walikuwa na mawazo tofauti juu ya watu wengine. Basi mawazo ya watu ndivyo yalivyo. Kila mtu ana haki ya kusema anachokifikiri kichwani mwake. Tunaona hata Mitume wametoa mawazo tofauti kwa swali lile la Yesu. Basi si ajabu leo kusemana. 

Leo tena tunapoelekea siku ya Nyerere nikaona hebu nijitokeze tena kutoa maoni yangu kuhusu Mwalimu Nyerere. Nia yangu ni kuchangia kuharakisha ule mchakato wa Jimbo Katoliki la Musoma kufikia maamuzi ya kumtangaza kuwa “MBARIKIWA” hatua ya pili kuelekea kuingia utakatifu. Sote tunautazamia kutunukiwa na Kanisa. Utakatifu nadhani unatokana na watu wa kawaida kutenda matendo ya kawaida kabisa kwa wenzao. 

Mimi namwona Mwalimu kuwa mtu aliyejaliwa tabia ya UTU (humanitarian aspect). Nilibahatika kukutana na Mwalimu katika fursa mbalimbali zilizojitokeza nikiwa katika JKT.  Mara ya kwanza nilishuhudia tabia yake ya UTU pale Ruvu ilikuwa Jumatano tarehe 23 Septemba 1970. Mwalimu alimpeleka Mgeni wake, Waziri Mkuu wa Guayana – bwana Forbes Burnham Ruvu kuona shughuli za vijana. JKT Makao Makuu waliamua chakula ha mgeni yule kiandaliwe kule Kilimanjaro Hoteli kisha kipelekwe Ruvu. Lakini Chef wa Kilimanjaro kwa busara zake asilia alinitaka niwapeleke baadhi ya wapishi huko Ruvu ili sehemu ya chakula kiandaliwe pale pale Ruvu huku kingine kiandaliwe Hotelini Kilimanjaro. 

Mungu bariki, ilikuja kutokea wakati wa chakula wakuu wako majilisi wanaanza kula, nikaletewa taarifa lile gari la chakula kutoka Kilimanjaro Hoteli lilipata ajali sehemu ya Misugwisugwi chakula chote kimemwagika! Unaweza kujua msomaji wangu hali yetu viongozi wa JKT pale Ruvu ilikuwaje hapo. Mkurugenzi wangu bwana Laurenti Gama akaamua chakula chote kilichopikwa pale Ruvu kiliwe na wageni waliomo majilisini tu – ndiyo kusema madereva, na maaskari wa msafara wa Rais wasile! Unasikia hilo? Tukaamua hao wapewe chakula cha askari wa JKT pale kambini. 

Wageni walipomaliza mlo wao niliwaongoza kwenye magari yao. Hapo, Dereva mmoja wa Ikulu akaja moja kwa moja kwa Mwalimu na kuomba wapatiwe dakika chache nao wale chochote! Nikaulizwa, kwani hawa jamaa hawajala muda wote huu? Ndipo aibu yetu tuliyotaka kumficha Mkuu wa nchi ikafichuka akasikia kuwa gari la JKT kutoka Kilimanjaro Hoteli lilipinduka! Mwalimu alikubali kurudi majilisini kusubiri wenzake wale. 

Hiyo niliona ni tabia ya UTU aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere. Kweli dereva amwendea Rais moja kwa moja? Ni tabia aliyowazoesha kuwasikiliza, ni tabia ya kuwajali watu (very approachable man). Vinginevyo ungekuwep ukiritimba mkubwa na wangetoka bila ya kula nani angethubutu kumweleza mkuu wa nchi hilo? Hakuna!  

Hiyo ni tabia waliyonayo watu wachache kabisa wenye hadhi ya juu kujishusha hadi kuwasikiliza watu wahitaji wa chini katika ofisi za Serikali. 

Mara ya pili kuona tabia ya UTU wa Mwalimu ilikuwa kule kijijini Butiama nyumbani kwao. JKT walipewa kazi pale kijijini kujenga Jumba la Meandeleo na Kituo cha Afya cha Kijiji. Tuliita operation Butiama. Kazi ilianza Agosti, 1971 na ilikamilika mwezi Mei 1972. Wakati wa Krismas Mwalimu aliagiza JKT wapande minyara kuweka mpaka kati ya eneo lake na la mwenyeji mwingine mzee wa pale mijijini. 

Ilipofika tarehe 20/05/1972 Mwalimu akaja kufungua rasmi kile Kituo cha Afya hapo kijijini Butiama. Ni utamaduni uliozoeleka Mwalimu akitoka mjini kuingia kijijini kwanza anafika nyumbani kwa Chief Wanzagi kumwamkia, toka hapo anapita kwa bibi Mgaya, mama yake mzazi kumwamkia halafu anakwenda kwenye mji wake kupumzika. Basi ile tunatoka tu uwanjani kwa Bibi Mgaya, Mzee mmoja mwanakijiji akamsogelea Rais huku akifoka. Kwa kizanaki na kuonyesha ile minyara ya mpaka. Mwalimu alimsikiliza, akamgeukia Chief Wanzagi kutaka ushauri – mara akaniita akanishika mkono, “Kamanda huyu jamaa tumemwingilia katika eneo lake, sasa bwana fuatana naye akuonyeshe mpaka halali na mhamishe hii minyara jamani”. Yule mzee akaonyesha mpaka, na kukubalika na Chief Wanzagi – sisi tukamwambia tutahamisha minyara ile siku ile ile. 

Cha ajabu, mzee yule aliingia nyumbani kwa Mwalimu, wakakumbatiana na kucheka kwa furaha. Mimi sikuelewa hata tabia ile ya Mwalimu. Kumbe pale kijijini watu wengine wote walimjua kuwa Mwalimu ana tabia ya kuwasikiliza wenzake wala haoni ugumu kutenda haki pale penye alama ya uonevu au dhuluma. Nchi gani, mzee wa kijiji anaweza kumwendea Mkuu wa nchi moja kwa moja bila kuzuiwa na walinzi wa Raisi? Ni Nyerere tu. Tena ni karama kubwa ya kujali utu wa wengine. Kwa taratibu za kawaida za kiofisi humuoni mkubwa kabla hujanaswa na walinzi au makatibu wa ofisi husika! 

Mwalimu ni MTU wa WATU, mwenyewe anayo hiyo tabia ya UTU kama imani ya TANU inavyosema “Binadamu wote ni SAWA” aliamini hivyo na alitenda alivyoamini. 

Ningali nachungulia kurasa mbalimbali za DIARI zangu. Ninakuta tukio jingine la kunishangaza juu ya tabia hii ya UTU aliyonayo Mwalimu. Ilikuwa tarehe 30 Desemba 1971 Mwalimu akiwa katika mapumziko yake ya Krismasi kijijini Biatika wakati ule. Aliamua ghafla siku ile ya Alhamisi ya tarehe 30 kutembelea kijiji cha Butiamam karibu sana na kambi za JKT Buhemba. Mahali  hapo ndipo ofisi ya kwanza ya TANU kule Uzanaki ilianzishwa katika Wilaya ya Musoma. NikajulishWa tu kama Mwalimu na mgeni wake Bibi Wilson (mama mzungu) kutoka Edinburgh, mji aliosoma Mwalimu 1948 – 52 wakati ule alipanga chumba nyumbani mwa mama huyu kule Uingereza wanasema alikuwa mama mwenye nyumba wake (Land Lady wake) watapitia kambini kumwonesha mgeni wake baadhi ya shughuli za vijana wa JKT. 

Basi baada ya kuzuru ile ofisi ya TANU wakaja kikosini Buhemba. Bila kuficha tulijisikia tunapwaya maana hatukujiandaa kumpokea Rais na Amiri Jeshi Mkuu pale kambini. Mwalimu alijifanya mwenyeji sana akatusimulia soga za ule mgodi wa dhahabu pale, tukacheza naye table tennis mle mesi tukajiona tumetulia. 

Ndugu yangu Joseph Butiku alitutuliza kwa kutuambia tumpe zawadi zilizotengenezwa na vijana wa kutoka vijiji vya vyama pale kikosini. Pale tulifundisha vijana uashi, ushonaji nguo, ushonaji viatu, kazi za kutengeneza vibatari na mapipa ya takataka na masanduku ya bati na useremala.

Basi tulimzawadia pea 1 ya vitau na tukampa PIPA moja kubwa la takataka (dust bin). Loo! Kwa mshangao wetu Mwalimu alilipokea lile pipa kwa kicheko kikubwa na kusema, “Loo vijana asanteni sana sana. Kama lipo pipa jingine nipeni nikampe mama yangu pale nyumbani. Ilikuwa nimtume Joseph (Butiku) kwenda mjini Mwanza Government Store kunitafutia dustbin hizi”. Sasa loo mmenifaa kweli”. Kisha tukampa yule mgeni wake trey ya mbao iliyonakishiwa vizuri tu.  Sisi viongozi wa JKT Buhemba tulishikwa na mshangao. Kweli pipa la takataka ni zawadi ya kumpa Mkuu wa nchi? Lakini kwake Mwalimu alifurahia kupokea kazi ya watoto kutoka vijijini na hilo pipa eti lilikuwa hitaji muhimu kwake. Tulitiwa moyo wa kuendeleza mafunzo kwa vijana wa kutoka vijijini. Lakini mimi nililiona tendo lile la Mwalimu kuthamini vitu vinavyotengenezwa na sisi wenyewe nifundisho tosha kwa viongozi wa nchi zinazoendelea. Tabia hii ya Mwalimu ni kama ya hayati Mahatma Ghandhi Baba wa Taifa la India aliita CIVILIZED SIMPLICITY “kuthamini ulichonacho” na ndiyo alihubiri, wahindi waishi maisha namna hiyo. Huyo ndiye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere nilivyomuona mimi. 

Bahati ya kuonja tabia ya UTU ya Mwalimu sikuiona mimi peke yangu hata niitolee ushuhuda namna hii. Wapo baadhi ya watu wamemuona Mwalimu katika matendo makubwa zaidi ya haya. Nirejee maelezo ya mpishi wake aliyoyatoa katika Gazeti la Jamhuri Toleo Maalumu No. 158 ukurasa 23. Huyo mpishi anaitwa Bwana Evaristus Ernest Nchia. Yeye alisimulia kwa kirefu namna Mwalimu alivyomsaidia kulipwa fedha zake za likizo. Ni hadithi ya kusononesha kidogo kuona watumishi wa madaraja ya chini wanavyonyanyasika kupata haki yao ya stahili kwa mujibu wa sheria za utumishi. Makala yake ile Jamhuri waliipa kichwa “SITASAHAU SIKU MWALIMU NYERERE ALIPONISAIDIA KUPATA PESA ZANGU ZA LIKIZO”. Katika maelezo yake mengi alifikia kusema tulipofika Airport Mwalimu alimuuliza (bosi aliyekuwa na hizo fedha) swali moja tu, “kwanini unamtaabisha huyu kijana? Hata kabla huyo boss hajajibu alipewa amri moja (na mwalimu) haya mpe pesa yake huyu kijana. Sipandi ndege hadi umempa huyu kijana pesa yake (maneno ya Mwalimu akiwa amekasirika).

Kweli Mwalimu alikuwa tayari kususia kupanda ndege ya kumpeleka Butiama kama yule afisa asingelilipa fedha za mpishi yule. Kwa Rais wa nchi, hii ni hali ya unyenyekevu mkubwa. Si angesema tu, “we kazi kwangu basi, sifanyi kazi na watu wakorofi” na akamrudisha siku ile ile ofisi mama alikoajiriwa yule boss?

Mwalimu hakuwa mtu wa namna ile alikuwa na mizania ya kupimia maisha ya wote na alifanikiwa kuwafanya wengine waonje UTU wake mioyoni mwao. Na wanyonge walimuona kama ni mkombozi wao katika nchi isiyo na haki wala huruma kwa binadamu wengine (Hadithi ya mpishi Evaristus inapatikana katika lile Toleo Maalumu la Mwaka jana tarehe 14 uk. 23 gazeti la Jamhuri). Hii ni kielelezo cha Tabia ya Mwalimu kutokupenda kuona wanyonge na wadhaifu wanapnewa au wanadhulumiwa au wananyanyaswa kinyume cha sheria za nchi. Aliamini kila binadamu anastahili heshima maana yu sawa na huyo binadamu mwingine. 

Mfano mwingine ni ile tabia ya Mwalimu kusaidia wahitaji mbalimbali ipo simulizi tena mwenye hilo hilo gazeti la Jamhuri inayoelezea kisa cha mlemavu kutoka Mtwara. Huyu alifunga safari bila miadi na Mwalimu hapo Ikulu. Alifika Dar akaenda Ikulu kumwona Mwalimu naye akamsikiliza hitaji lake. Aliomba ajengewe nyumba – Mwalimu baada ya kumsikiliza alikubali ombi lake Mlemavu yule hatimaye kweli alijengewa nyumba na sasa anaishi humo. Hili mimi nalitafsiri kama ni tendo la huruma na linaambatana na ile amri kuu ya mapendo. 

Tunasoma katika Matayo sura ile ya 22 mstari wa 35 – 39 maneno haya, “mmoja wao, mwanasheria, akamuuliza akimjaribu Mwalimu, katiaka torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia  Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili yako yote. Bwana wetu Yesu Kristo alimjibu yule muilizaji…. Na ya pili yafanana nayo; nayo ni hii, mpende jirani yako kama nafsi yako” (Mat. 22:35 na 39). Hapa ndipo mimi naona Mwalimu hakupendekezwa na tabia za baadhi ya wasaidizi wake. Yeye mwenyewe alikuwa na moyo wa wazi na wa huruma (open hearted with humanitarian aspect) alijua wahitaji, aliwapokea, aliwasikiliza na awaliwatendea vilivyo!

Kwa tabia hii amewasaidia wengi sana. Kwa ule utayari wake ametatua matatizo ya wengi. Aliwaona watu wote kama majirani zake, na shida au mahitaji yao ni kama vile yeye mwenyewe aliyahitaji ndiyo maana akawa mwepesi kuwatatulia wenzake matatizo yao. Alijisikia kama vile yeye anateseka. Haya ni mawazo yangu jamani, ninavyomuona Mwalimu. 

Basi napenda nimalizie mawazo yangu haya juu ya hiyo tabia ya UTU aliyokuwa nayo Mwalimu hivi. Akiwa hospitalini kule London, bado aliwakumbuka watu wa nchi hii. Alifikiria namna ya kutumia fedha zilizosalia katika mfuko ule wa Tanganyika Education Trust Fund kwa kuwanufaisha wahitaji wa kweli wa Elimu. Nimebahatika kupata nakala ya agizo lake kwa Mweka Hazina wa Mfuko ule. Mwalimu akitumia anwani ya ofisi yake iliyoko hapa hapa Dar es Salaam ya SOUTH CENTRE S.L.B 71000 aliandika barua ile kwa Mzee Manilal Devani na kuagiza haya ninanukuu baadhi tu ya maelekezo yaliyomo katika barua ndefu ile nayo ni kama haya “It thus seems to me that the Open University of Tanzania would be an appropriate institution to receive the money which is still in the hands of the Tanganyika Education Trust Fund. It is non – sectarian, non – Party political, focused on the education of adults, and makes special provision for distance learning by visually impaired potential students as well as those suffering from hearing difficulties. 

When I next come to Dar es Salaam I hope we shall be able to meet and discuss these matters together with any ideas you may have as well as any problems which might have arisen or can be anticipated. 

I should also make it clear that in carrying out the tasks you will receive any necessary support from me and my office, and (albeit from her home in Britain) from Joan Wicken. 

With my good wishes,

Your sincerely,

Chairman Of Tanganyika  Education Trust Fund

 

Kwa mtazamo wake, Mwalimu aliamini sana kuwa fedha zilizosalia katika mfuko ule zote zihamishiwe OUT kwa sababu moja tu ya msingi kuwa Chuo kikuu hicho siyo cha KIDINI, siyo cha CHAMA CHA SIASA bali kinajikita katika kuhudumia watu wazima mkazo zaidi kuelekea wenye ulemavu wa kuona na kusikia. Kiongozi gani anawafikiria zaidi wenzake wenye uhitaji huku yeye mwenyewe yu hoi kitandani hajiwezi? Mbona siyo jambo la kawaida kwa wagonjwa kufikiri namna hiyo! Ni tendo la huruma kwa wengine hilo. 

Kuna wakati nilisoma katika gazeti moja la Uganda, liitwalo “UGANDA NEW VISION” la June 2009 mle iliandikwa kuwa Rais Yoweri Museveni wakati anaongea na Mahujaji pale Namugongo siku ya kilele cha sherehe ya mashahidi wa Uganda, alimsifu baba wa Taifa kwa maneno haya. “Museveni Yesterday praised Mwalimu Nyerere for the different religions groups in Tanzania and advancing Swahili as a common language to unite the ethnically diverse country”. Today Tanzania is the most peaceful country in Africa with no civil wars”. Akaendelea kusema “Nyerere was like the Ugandan Martyrs who stood for truth against sin, even at the expense of their lives. I join those who are praying for the canonisation of Mwalimu to be a saint” (Uganda New Vision pg. 1).

Kwa maombi namna hiyo, nami naandika haya mambo madogo madogo ya kawaida kabisa aliyotenda Mwalimu kwa imani yataongeza uzito wa mizania yake mbele ya wale wanaoandaa mchakato huko Musoma wa kumfikisha Mwalimu kwenye hatua ya pili kuelekea utakatifu. Hiyo hatua inaitwa “MBARIKIWA” amekuwa Mtumishi wa Mungu, sasa tunamwombea aingizwe kwenye kuitwa MBARIKIWA).

Pindi maombi yetu kwa Mungu yakijibiwa basi baadhi yetu huenda tukajaaliwa kupata yale tunayoomba kwa Mungu kupitia sala na maombezi ya huyu MTUMISHI WA MUNGU, MWALIMU, JULIUS KAMBARAGE NYERERE. 

 

INSHAALLAH MUNGU AKIPENDA. 

By Jamhuri