Taifa limefikaje hapa? (1)

Kutokana na ile makala yangu “Pilipili usizozila zakuwashiani?” nimepokea mrejesho wa kushangaza kutoka wasomaji wa JAMHURI. Moja ya SMS hizo ilisomeka hivi nainukuu: “Brigedia Jenerali Mstaafu Francis Mbenna, shikamoo mzee wangu na hongera kwa makala zako nzuri na zenye kuelimisha na kutufundisha kwa vijana kama mimi.

Baba Mungu akubariki sana. Mimi naitwa (jina limehifadhiwa). Kwa sasa napatikana Tanga ambako niko kikazi kama mhasibu. Nakuomba mzee wangu uweze kunitumia materials yanayohusu nchi yetu kupitia barua pepe ambayo ni (imehifadhiwa). Lengo langu ni kutaka kujua na kujifunza na kuelewa nchi yangu kwa mapana yake, maana nimesoma makala zako nyingi katika gazeti la JAMHURI nimegundua kuwa wewe una hazina ya Historia ya Tanzania kabla ya Uhuru.  Ninatanguliza shukrani zangu za dhati ombi langu endapo litakubaliwa na kufanyiwa kazi. Alhamisi 9:37 alasiri (tarehe 27 Aprili)”.

Ombi namna hii ni vigumu kulipuuza. Huyu kijana na labda wengine wengi katika nchi hii wako kama yeye – hawajui kabisa huko nyuma nchi yetu ilikuwaje, hivyo wana kiu ya haki kujua tulikotoka mpaka hapa tulipo.

Kwanza niseme asante sana kwa SMS yako na asante kwa wale wote wanaosoma makala zangu na wananipa mrejesho kwa SMS zao. Kiu yao kubwa hapa ni kufahamu taifa letu lilianzaje na kujua taifa limefikaje hapa tulipo leo hii.

Ninafikiri ni vizuri kuwapa wahusika angalau kwa ufupi namna nchi ilivyokwenda hadi leo tuko katika Awamu ya Tano. Nianze kwa kusema hivi; hapo kale wazee wetu walikuwa wanatupatia habari za zamani kwa njia ya mazungumzo – ilikuwa ni historia ya mapokeo katika makabila mbalimbali. Lakini makabila yale yaliunganishwa kwa nguvu na Wazungu tunaowaita wakoloni baada tu ya ule mkutano wa Berlin, Ujerumani mwaka 1885 ulioitishwa na mtawala wa Ujerumani aliyeitwa Kaizari Wilhem na Waziri wake akiitwa Bismarck.

Baada ya mkutano ule ndipo nchi yetu ilichukuliwa na Wajerumani na wakaita Koloni la Wajerumani la Afrika Mashariki. Wenyewe Wajerumani wakiita “Deutsch Ostafrika”. Basi historia ya taifa letu ndiyo ilianzia hapo na kwa namna hiyo. Hapa ni vema ukajua hiyo ‘nchi mpya’ ambayo ni Tanganyika ya leo, pia ilizijumuisha pamoja nchi za Burundi na Rwanda. Kabla yake sisi hatukuwa taifa na hatukujuana. Tanganyika ilianza kujulikana kuanzia pale Wajerumani walipotutawala. Utawala wao ulijaribu kutuunganisha makabila yote ya katika koloni lao hili na wakatuita sote kwa umoja wetu WATANGANYIKA.

Wazungu hawakutuita sisi taifa. Wao walisema ni makabila tu yanayopigana pigana ndipo wakaleta utawala wao mmoja (colonial rule) kutufanya sisi tuunganike pamoja katika nchi yao walipotawala. Utawala wao ulidumu kwa takribani miaka 25 hivi yaani kuanzia mwaka gavana wa kwanza wa Kijerumani aje Tanganyika mwaka 1891 mpaka siku gavana wa mwisho wa Kijerumani alipovurumishwa na Waingereza baada ya ile Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (First World War) mwaka 1918.

 

Kwa mantiki hiyo naweza kusema AWAMU YA I ya utawala katika nchi yetu ni ile ya enzi za utawala wa Wajerumani 1891 – 1918; Ni muda wa miaka 25 tukaanza kujengwa kuwa wamoja kitaifa. Awamu ile ilikuwa na magavana wa Kijerumani saba kuanzia yule wa kwanza mwaka 1891 aliyeitwa Gavana Julius Von Soden na kumalizia na Gavana Heinrich Schnee aliyetoka mwaka 1918.

Awamu ya pili mimi ningeita ni ile ya utawala wa mkoloni Mwingereza. Hii ilianza kwa mtutu wa bunduki pale Wajerumani walipoondolewa toka nchini mwetu baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914 – 1918) ambako Waingereza walikabidhiwa nchi yetu na Umoja wa Mataifa uliokijulikana kama League of Nations. Hivyo tukawa chini ya uangalizi wa Waingereza tukaitwa “TRUST TERRITORY”. Ndipo tukawa chini ya udhamini wa Uingereza, lakini tukiwa chini ya Umoja wa Mataifa yaani  League of Nations.

Sisi tuliosoma zamani tulifundishwa historia inayoitwa “British Empire History” hivyo tulijua ukoloni vizuri sana. Maana Tanganyika ilikuwa kama  nchi mojawapo ya makoloni ya Waingereza (British colonies) mfano Kenya, Zambia, na Malawi; nchi ambazo zilikuwa ni makoloni ya Mwingereza.

Pili, kulikuwepo nchi zilizolindwa na Waingereza (British Protectorate countries) mfano Uganda na Zanzibar. Kumbe sisi hatukuwa koloni la Waingereza wala hatukulindwa na Waingereza, bali tulikuwa chini ya Umoja wa Mataifa, lakini kwa mazingira ya kiutawala tulizungukwa na himaya ya nchi za Waingereza ndipo waliombwa wasimamie kutuongoza mpaka wakati tutakapofikia hali ya kujitawala wenyewe.

Kumbe kijiografia tulizungukwa na nchi zinazotawaliwa na Mwingereza (geographically we were sandwitched between British colonies). Ndipo Waingereza wakatutawala kama vile Tanganyika ilikuwa moja ya makoloni yake yale au nchi walizolinda. Hilo likawa tatizo kubwa kwetu.

Mwingereza alitawala Tanganyika kuanzia mwaka 1918 – 1961 takribani miaka 45 hivi yaani tangu mwisho wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mpaka tunapata Uhuru. Kwa muda wote huo wakaleta magavana wao kama ilivyokuwa kwa Kenya au Malawi au Uganda.

 

Awamu hii ya pili ya utawala katika nchi yetu wamekuwepo magavana wakoloni Waingereza 10 tukianzia na yule Mwingereza mtawala wa mara baada ya Vita Kuu ya Kwanza kumalizika aliyekuwa British Administrator” tangu mwaka 1918 – 1924. Huyu hakuwa gavana, la hasha, alikuwa tu msimamizi baada ya vita, aliitwa Sir Horace Byatt. Alisimamia mwaka 1918 – 1924.

Huyu alifuatiwa na Kaimu Gavana akiitwa John Scott kwa kipindi kifupi sana mwaka 1924. Nchi yetu baada ya kutulia baada ya vita ile aliletwa gavana mwenyewe, aliitwa Sir Donald Cameroon – huyu ndiye alianzisha hata utawala wa serikali za mitaa zikaitwa “Native Authority”.

Wamepita magavana watano baada ya yule Gavana Cameron ndipo mwaka 1949 akaletwa gavana anayejulikana sana hapa nchini (kwa ukorofi wake) aliyeitwa Sir. Edward Twinning. Wakati wake ndipo vuguvugu la siasa nchini Tanganyika lilipamba moto. Ona haya matukio muhimu:-

  1. TANU ilianzishwa Julai 7, 1954.
  2. Gavana Twinning na serikali yake ya ukoloni walishawishi walowezi katika nchi hii kuanzisha chama cha MSETO 1956 kilichoitwa U.T.P kukipinga chama cha TANU.
  3. Mwaka 1958 baada tu ya ule mkutano wa kihistoria wa TANU mjini Tabora kukubali uchaguzi wa mseto, Zuberi Mtemvu alikiasi chama cha TANU akaanzisha chama chake cha siasa kilichoitwa African National Congress – ANC.
  4. Mwanzoni mwa mwaka huo wa 1958 Rais wa TANU Mwalimu Julius K. Nyerere alishtakiwa na serikali ya wakoloni kwa makosa ya uchochezi kupitia gazeti la Sauti ya TANU. Mwalimu alipatikana na hatia, alihukumiwa faini ya Sh 3,000 au kwenda jela miezi 6. Akitoa hukumu katika kesi hii Hakimu aliyeitwa Davis alisema haya, namnukuu, “Nyerere ni mtu mwenye busara nyingi. Ni mtu mwajibikaji katika jamii”. “Halikuwa jambo la kawaida kutoa adhabu ya kifungo kwa makosa kama haya. Na mimi sitaki kujitenga na desturi hiyo. Namtoza mshitakiwa faini ya Sh 3,000 au kwenda jela miezi sita” (Tazama: Kesi ya Julius Kambarage Nyerere 1958 uk. 55).
1042 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons