Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeanza uchunguzi wake dhidi ya Meneja wa Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Dk. Milali Machumu ambaye analalamikiwa kwa kuwanyanyasa na kuwafukuza wafanyakazi bila kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, miezi miwili iliyopita aliwapeleka Takukuru baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo wanaomlalamikia kwa kuwanyanyasa kwa kuwashusha vyeo na kuwahamisha vituo vya kazi kwa kile kinachoitwa kutumikia adhabu.
Hata hivyo baada ya kuwafikisha wafanyakazi wake Takukuru na mahojiano ya awali kufanyika iligundulika kuwa yeye ndio chanzo cha matatizo yote na hivyo ameanza kuchunguzwa kwa kuchezea muundo wa utumishi wa taasisi ya anayoingoza.
Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Mussa Misalaba amethibitisha kuendeshwa kwa uchunguzi dhidi ya Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo na kwamba bado uchunguzi unaendelea.

“Siwezi kueleza kuwa uchunguzi dhidi ya Mtendaji huyo na malalamiko yaliyofikishwa katika Taasisi yamefikia wapi kwa sasa, lakini bado taratibu za uchunguzi zinaendelea na ukikamilika utakuwekwa wazi,” amesema Misalaba.
Meneja wa taasisi ya MPRU, Dk Machumu hakupatikana kuelezea sababu za kuwafikisha wafanyakazi wake Takukuru. Hata hivyo vyanzo vyetu vinaeleza kuwa wiki iliyopita amehojiwa pia na tume kutoka Hazina.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya taasisi hiyo, Profesa John Mochiwa ameliambia JAMHURI, malalamiko mengi ya wafanyakazi kama hayafikishwi katika ngazi mbalimbali serikalini hayawezi kupatiwa ufumbuzi na matokeo yake ni kuchelewesha upatikanaji wa haki zao.

Profesa Mochiwa amesema Bodi haipati taarifa zozote kama malalamiko ya mtumishi yako hayajafikishwa katika ngazi nyingine au yako kwenye Menejimenti.
“Bodi haiwezi kusikiliza malalamiko yoyote yanayoletwa na mtu binafsi kwani vikao vyake vyote vinaitishwa na Menejimenti na vikao hivyo vina gharama,” amesema.
Pamoja na hayo Mwenyekiti huyo hakuweza kukanusha bodi hiyo kuhojiwa na TAKUKURU kutokana na malalamiko ya watumishi hao dhidi ya meneja wa taasisi hiyo.

Malalamiko ya wafanyakazi hao dhidi Meneja huyu ni kuwatisha mara kwa mara kuwa atawafukuza kazi na amekuwa akitekeleza kauli yake hiyo kwa kuwafukuza bila makosa na kufuata taratibu za kazi.
Tuhuma nyingine za Dk Machumu ni kuchezea muundo wa utumishi wa taasisi hiyo na kuwashusha vyeo baadhi ya watumishi na kuwapunguzia viwango vyao vya mishahara kwa lengo la kupambana nao bila kuwa na sababu za msingi.
Wamedai kutokana na manyanyaso wanayoyapata kutoka kwa Meneja huyo ari na moyo wa kufanya kazi imepungua na kinachoendelea ni ugomvi na vitisho kwa kila mtumishi.

Wakitoa mfano wa manyanyaso hayo wamesema hata mlinzi akichelewa kidogo kufungua geti anafokewa na kutishiwa kutimuliwa kazi na kwamba manyanyaso haya ya wafanyakazi yamechangiwa kwa kiasi kikubwa uongozi wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Malalamiko yao mengine ni uhamisho ambao ukifanyika kwa watumishi kutoka Makao Makuu ya Taasisi hiyo na kwenda katika vituo vingine kuwa ni adhabu kwa wale ambao wamekuwa wakihoji kuhusu taratibu za utendaji wa kazi ambazo zimekuwa hazifuatwi na meneja huyu na kuigeuza taasisi ya Serikali kama kampuni binafsi ya Mhindi.

‘‘ Tunaishi kwa hofu sana kama sio Watanzania; tumechoka kunyanyaswa na kiongozi huyu ambaye hana utu zaidi ya kuendekeza ubabe usiokuwa na tija kwa taasisi hii, kwani hataki hata kushaurika,’’ kinaeleza chanzo chetu.
Vituo vya kazi ambavyo wanahamishiwa kama mahabusu za kutumikia adhabu vimekuwa na mazingira magumu ikiwemo ofisi zao kukosa huduma mbalimbali muhimu.
Pamoja na malalamiko yao wameiomba Serikali kuiweka taasisi hiyo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ili kupanua sekta ya utalii nchini, badala ya kuwaacha wawekezaji kutoka nje ya nchi wakiendesha biashara zao katika fukwe za bahari bila kulipa mapato yoyote na Serikali kukosa mapato.

Pamoja na Sheria ya ulipaji wa tozo ya dola za Marekani 1,500 iliyopitishwa na Serikali mwaka 2009 na kutakiwa kuanza kutumika rasmi Julai Mosi mwaka huo kwa wamiliki wa Hoteli ambazo ziko katika maeneo ya hifadhi za bahari katika kituo cha Mafia.
Kutokana na muundo mpya wa utumishi ulioidhinishwa na Msajili wa Hazina mwaka 2006, Bodi ya Wadhamini ya taasisi hiyo iliwapandisha vyeo baadhi ya maofisa wake akiwemo Dk Machumu, lakini amewashusha vyeo na mishahara bila sababu za msingi.
Miongoni mwa madai yaliyotolewa na Dk Machumu ni kuwa watumishi hao walijipandisha vyeo wenyewe, huku akifahamu hakuna mtumishi anayejipandisha cheo mwenyewe. Bodi ya Wadhamini ndio iliyohusika katika mchakato huo baada ya kuona utendaji wao hivyo vyeo vyao ni halali.

Kutokana na maboresho ya miundo ya utumishi, Msajili wa Hazina aliidhinisha miundo ya utumishi ya Bodi ya Wadhamini ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kwa barua ya Mei 16, 2006 yenye kumbukumbu namba TYC/T/200/598/02/7 iliyobadili miundo ya utumishi ya taasisi ya mwaka 1999.
Maboresho hayo yalipanua wigo wa mishahara kwa kada zote za taasisi akiwemo Mtendaji Mkuu aliyepanda kutoka PGSS 19 hadi PGSS 21.
Mfumo huo (scheme of service) hauwezi kuhalalisha vyeo vya baadhi ya watumishi wa taasisi hiyo akiwemo meneja na kubatilisha vyeo vya wajumbe wote wa menejimenti kwa madai kwamba walijipandisha vyeo wenyewe.
Pamoja na kuwahamisha baadhi ya watumishi katika vituo vingine vya kazi hajawalipa fedha zao za uhamisho hadi sasa na kati ya Sh milioni 10 walizostahili kulipwa wameambulia malipo ya Sh milioni 1 tu.

NA CLEMENT MAGEMBE

1343 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!