Tangazo la NEC lahitimisha udiwani wa Manji

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata 21 ikiwamo ya Mbagala Kuu katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, jambo linalohitimisha udiwani wa mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Athuman Kihamia, juzi alitangaza uchaguzi huo mdogo kupitia taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari.

Katika taarifa yake, Dk Kihamia alieleza kuwa uchaguzi huo utafanyika Septemba 16, akisema kata hizo ziko wazi kwa sababu mbalimbali ikiwamo waliokuwa madiwani kujiuzulu, kufariki dunia, kutohudhuria vikao vya mabaraza ya udiwani na kufutwa uanachama na vyama vyao vya siasa.

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi mgombea urais, ubunge, udiwani, uenyekiti wa mtaa, kitongoji au kijiji anadhaminiwa na chama chake cha siasa kuwania nafasi husika.

Septemba 7, 2017, Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo alitangaza Manji kuvuliwa udiwani wa Kata ya Mbagala Kuu kwa kushindwa kuhudhuria vikao sita vya baraza la madiwani vya 2016 bila kutoa taarifa.

Chaurembo aliwaambiwa waandishi kuwa waliamua kumuondoa Manji kwenye nafasi hiyo kwa kukosa sifa ikiwa ni pamoja na kutohudhuria vikao hivyo na kamati za madiwani alizokuwa mjumbe.

Alisema mbali na kukosa sifa za kuendelea na udiwani kwa kosa hilo, baadhi ya wananchi wa Kata ya Mbagala Kuu waliwasilisha malalamiko ya kukosa uwakilishi katika baraza la madiwani, huku chama chake – CCM nacho kikiridhia avuliwe udiwani.

Katika mahojiano na gazeti hili Septemba 14, 2017, Chaurembo alisema, “Manji hakuhudhuria vikao na hakutoa taarifa mpaka sisi tulipomtafuta ndipo akajibu. Tukawasiliana na chama chake wakasema tuendelee na taratibu.”

Meya huyo alisema Manji hakuhudhuria vikao vya baraza la madiwani Februari 3, Machi 24, Juni Mosi, Agosti 25, Novemba 24 vyote vya mwaka 2016 na Februari 14 hadi 15 vya 2017.

Alisema vikao vingine alivyokosa ni vya kamati ya maendeleo ya halmashauri hiyo ambavyo alikuwa mjumbe vilivyofanyika Machi 18, Agosti 17, Novemba 8 vya mwaka 2016 na Februari 2, 2017.

Chaurembo alisema kuwa Februari 20, 2017 Manji aliandika barua kwa mkurugenzi akitoa taarifa ya kutohudhuria vikao vya halmashauri hiyo kutokana na sababu za kiafya bila ya kuwasilisha uthibitisho wa daktari.

Chaurembo alisema Machi 2, mkurugenzi wa manispaa alimwandikia barua Manji akimtaka awasilishe taarifa za daktari kuthibitisha matatizo ya kiafya kama alivyoeleza kwenye barua yake, lakini badala yake waliendelea kumuona kwenye vyombo vya habari akifanya shughuli zake.

Alisema Mei 25, diwani huyo alimwandika barua meya na kumpatia nakala mkurugenzi akieleza kuwa ameshindwa kuhudhuria vikao kwa sababu za kiafya bila kuweka uthibitisho wowote.

Chaurembo alisema pia Manji aliweka wazi nia yake ya kutaka kujiuzulu kama hali yake ya kiafya haitaimarika.

Hata hivyo, baadaye Manji ambaye alikabiliwa na kesi kadhaa ikiwamo ya uhujumu uchumi alieleza kutokubaliana na hatua ya kumvua udiwani na mara baada ya kuachiwa aliulizia kuhusu malalamiko yake.

Katika taarifa ya Dk Kihamia juzi, alieleza kuwa taarifa za kata hizo kuwa wazi wamezipata kutoka Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na kuamua kuitisha uchaguzi utakaofanyika katika mikoa 10 ya Tanzania Bara.

Alizitaja kata zingine mbali na Mbagala Kuu kuwa ni pamoja na Vingunguti na Zingiziwa (Dar es Salaam); Machame Uroki, Kia na Nasai (Kilimanjaro); Kiutu, Olturoto na Mswakini (Arusha).

Zingine ni Maanga, Sisimba, Iwambi, Nsalaga na Nkuyu (Mbeya); Mwanzange na Masuguru (Tanga); Loorela (Manyara); Kashenye (Kagera); Kizota (Dodoma); Bugalama (Geita) na Mwanhuzi (Simiyu).

Dk Kihamia pia alitumia fursa hiyo kuviasa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali ya Mitaa ya mwaka 2015, maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2015 pamoja na maelekezo yote yatakatolewa na NEC.

765 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons