TCRA YASHUSHA RUNGU KWA VITUO 5 VYA RUNINGA HAPA NCHINI

Mamlaka ya mawasiliano Tanzania, TCRA, imevipiga faini ya shilingi milioni 60 vituo vitano vya Runinga kwa kurusha taarifa ambazo zinakinzana na kanuni za utangazaji kwa kurusha habari ambayo inasadikiwa kuwa na viashiria vya uchochezi.

Vituo vilivyokutana na rungu hilo ni ITV, EATV, CHANNEL TEN, AZAM TWO na STAR TV.

Mwenyekiti wa kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Joseph Mapunda amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kuvihoji vituo hivyo na kukiri kuwa vimetenda makosa hayo.

Akisoma maamuzi ya kamati hiyo Bw. Mapunda amesema kuwa habari zilizoripotiwa na vituo hivyo December 6 mwaka jana hazikuwa na upande wa pili na hivyo kukosa sifa kimaadili na zingeweza kuhatarisha usalama wa Taifa.

Hata hivyo vituo hivyo vinaruhusiwa kukata rufaa katika tume ya ushindani kibiashara kama havikuridhishwa na hukumu iliyotolewa na Mamlaka ya mawasiliano Tanzania –TCRA.