Wakati Rais John Magufuli `akimkaanga’ Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeokoa jahazi kwa kuchangia usafirishaji wa mbolea kutoka jijini Dar es Salaam kwenda mkoani Rukwa.

Januari 8, mwaka huu, Rais Magufuli aliagiza kusafirishwa mbolea kwenda Rukwa na Katavi na kwamba kama hatua hiyo isingefikiwa hadi kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita, wenye jukumu hilo watapaswa ‘kuachia ngazi’.

Kabla ya kutoa agizo hilo, Rais Magufuli alieleza kutoridhishwa na utendaji kazi wa Dk Tizeba na Waziri wa Madini, Angella Kairuki, akihoji kama wanakijua anachokitaka na kinachotakiwa na Watanzania katika kuchagiza kasi ya maendeleo.

Agizo la Rais Magufuli ‘lilimuamsha’ Dk Tizeba aliyeshiriki mchakato wa kuhakikisha mbolea inasafirishwa na kufika kwenye maeneo husika ndani ya muda ulioagizwa na Rais Magufuli.

Lakini Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Lazaro Kitandu, anasema pamoja na mamlaka hiyo kuchangia jitihada zilizofanikisha mbolea kusafirishwa kwa wakati, zipo changamoto na vyanzo vilivyosababisha ucheleweshwaji wa mbolea hiyo kuelekwa kwenye mikoa hiyo.

Amezitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni pamoja na mgomo baridi wa wasambazaji pembejeo waliokuwa wakiidai Serikali.

Hata hivyo, Kitandu amesema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi, iliyahakiki madeni hayo yaliyotoka Wizara ya Kilimo na kubaini miongoni mwao yalikuwa ni ‘hewa’, hivyo kuchelewesha ulipaji wake.

Kitandu amesema tatizo lingine linawahusu wasambazaji wakubwa ambao ndio waagizaji wa mbolea kutoka nje ya nchi, wanaolalamikia kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la dunia.

Amesema wasambazaji hao wanadai kuwa gharama za kuwalipa wasafirishaji wa mbolea kwenda katika maeneo mbalimbali nchini zimeongezeka, hivyo wanaibua hoja ya kushindwa kumudu gharama hizo.

“Wametumia sababu za kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la dunia, wengine wakaficha mbolea kwenye maghala ili waiuze kwa bei kubwa badala ya ile iliyoelekezwa,” amesema Kitandu.

Amesema waliwaeleza wasambazaji wa mbolea hiyo kufuata bei elekezi ambayo walikubaliana pamoja na Serikali, lakini wameshindwa kufanya hivyo.

Amesema Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba ameshiriki kikamilifu katika mipango ya usafirishaji wa mbolea, hadi ikawafikia walengwa kwa wakati ulioagizwa na Rais Magufuli.

Pia ameelezea TFRA kutambua malalamiko ya wananchi hususani wakulima kuhusu mawakala wa pembejeo kuongeza bei ya mbolea kati ya Sh 500 hadi 1,500 kulingana na umbali.

Mwaka jana, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilitangaza utaratibu wa kuagiza mbolea kwa pamoja na kuweka bei elekezi katika mbolea za kupandia na kukuzia, huku ile ya DAP ikitakiwa kuuzwa kwa bei isiyozidi Sh 56,000 na UREA Sh 48,000.

16887 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!