Na Mwandishi Wetu

Napenda nianze hotuba yangu kwa kuishukuru Mahakama kwa kuweka misingi ya kudumu katika kuadhimisha wiki ya sheria kila mwaka, kwa kufanya ufunguzi rasmi wa shughuli za Mahakama.

Sisi mawakili na wanasheria ni wadau muhimu katika mchakato wa utoaji wa haki, tunaiona wiki hii kuwa ni fursa muhimu ya kuwafahamisha wananchi juu ya misingi ya utoaji haki kupitia Teknolijia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Tehama inaharakisha mchakato wa kutoa haki bila kuathiri maadili ya taaluma na haki yenyewe.

Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kinapaza sauti katika misingi ya kaulimbiu ya mwaka huu, “Matumizi ya Tehama katika utoaji wa haki kwa wakati na kwa kuzingatioa maadili”.

Kaulimbiu hiyo ni kichocheo muhimu na bora katika mchakato wa utoaji haki kwa ubora na wakati stahiki.

Hivyo, matumizi bora ya Tehama ni kichocheo kinachoharakisha maendeleo kwa sababu kinawawezesha wananchi kufanya mawasiliano, makubaliano, kutekeleza sheria, kutatua migogoro kwa haraka na kuwapa fursa ya kuendelea na shughuli za maendeleo bila kupoteza muda.

Ni dhahiri kwamba maendeleo yoyote yanakuja na hitaji la kutumia dhana na miundombinu, ili kuendana na kasi yake.

Kwa hali hiyo, mamlaka za utoaji haki zinasukumwa na maendeleo ya Tehama iliyopo katika msukumo wa maendeleo.

Ufahamu wa kompyuta kama chombo na vyombo vingine vinavyoweza kupitisha matumizi ya Tehama, lazima viwezeshwe  au kulishwa mifumo ya kimuundo na kisheria, ili kupitisha na kutumia Tehama kuharakisha utoaji haki.

Uamuzi na hatua hii ni mojawapo ya mafanikio ya rai yetu ya kipindi kirefu kwenye vyombo vya utoaji haki.

Tehama imetuwezesha kutuweka pamoja kwa muda mfupi sana, mchakato wa kupashana habari na kufahamishana nini kimetokea, kimemtokea nini mmoja wetu na nini tunaelekezwa kufanya pale wito au agizo linapotolewa na chombo chochote kinachotusimamia, kinachotuongoza, kinachoshiriki kutunga sheria au kinachotoa haki.

Kwa kipindi kirefu sasa jumuiya yetu imeweka mifumo ya Tehama kama ifuatavyo:

 • Mfumo wa regesta ya taarifa za mawakili ambazo mtu yeyote anaweza kuingia katika tovuti kumthibitisha wakili na yuko katika mfumo sahihi.
 • Mfumo huo pia umetuwezesha kutoa vitambulisho au taarifa kadhaa kwenye vyombo vya dola kwa muda mfupi;
 • Mfumo mmoja wa mawasiliano na upashanaji habari;
 • Mfumo wa pamoja wa taarifa za maendeleo ya elimu ya sheria unaotoa alama pindi tunapohudhuria mafunzo kwa mujibu wa sheria na kanuni tuliojiwekea, ili tuweze kupata leseni ya uwakili  kwa mwaka unaofuata;
 • Mifumo ya kukusanya mapato  inayopatikana kupitia njia mbalimbali ambayo huwawezesha wanachama wetu pamoja na wadau kulipia ada za uanachama, mafunzo, michango na misaada kutoka kwa wadau.
 • Kutunza kumbukumbu za matumizi ili kutoa taarifa sahihi katika dhana ya uwajibikaji;
 • Mfumo wa kupokea maoni na maswali kutoka kwa wanachama ikiwa ni pamoja na wadau wetu waliounganishwa kwenye mfumo;
 • Kwa kushirikiana na Lexis Nexis Publishers,tumeweza kuweka mfumo wa orodha ya uamuzi elekezi, unaoweka orodha ya mashauri elekezi (High Court and Court of Appeal judgement landmark cases).

Mfumo huu pamoja na kuwezesha kuona mashauri ya Tanzania kupitia taarifa ya uamuzi wa Tanganyika Law Society (TLS TR) inatuwezesha kuona uamuzi wa Mahakama nyingi za Jumuiya ya Madola duniani.

Kwa hivi sasa tuko katika mchakato wa kuingiza katika Tehama mambo yafuatayo:

 • Jinsi ya kutoa elimu ya kisheria, majibu ya papo kwa papo na ushauri wa kisheria kwa wananchi ambao kwa namna yoyote hawawezi kupata fursa ya kupata elimu ya sheria;
 • Mfumo utakaowawezesha wanachama wetu kupokea taarifa za shughuli, mikutano na mafunzo kupitia simu zao za kiganjani;
 • Mfumo utakaowawezesha wanachama wetu kushiriki moja kwa moja kwenye mikutano  na mafunzo yetu, hata pale wanapokuwa nje ya ukumbi popote pale nchini;
 • Mfumo unganishi wa wadau wetu wa taasisi za fedha kama vile benki na mitandao ya simu utakaowawezesha wanachama, wadau, na wabia wetu katika maendeleo ya taasisi, kulipia ada na michango yao bila kulazimika kutembea kwenda kwenye ofisi za mawakili zilizopo kwenye kanda zetu.
 • Kuweka mifumo mingine wezeshi ili kuharakisha huduma kwa wanachama, Serikali, Bunge na wananchi kwa ujumla.

Najua changamoto zilizopo katika Tehama, lakini ninaamini kwamba wakati umefika Mahakama, maofisa wa mahakama na wadau wake waanze kutumia Tehama.

Labda nitumie wasaa huu kutaja mambo kadhaa tunayoweza kuanza nayo:

 

 • Kulipa na kufaili mashauri na mawasiliano mengine mahakamani kwa njia ya mtandao;
 • Kuchukua na kutoa taarifa za kumbukumbu ya shauri kwa wakati wa usikilizwaji wa shauri. Hii huondoa udanganyifu, upotoshaji, upindishaji haki, hofu kwa wananchi kuhusu uamuzi, ulazima wa kupinda mgongo kwa waheshimiwa kuchukua kumbukumbu.
 • Tunasema hiki kinawezekana kwa sababu vyombo kama Bunge, kwa muda mrefu sasa, hutoa kumbukumbu zao kwa muda mfupi;
 • Kutoa taarifa za mashauri kama vile, kuhudhuria na kuahirisha  kwa wadaiwa na wadau wa kuweka katika kumbukumbu ya pamoja na wazi taarifa ya Mahakama, sheria na kanuni mbalimbali ili kuwawezesha majaji, mahakimu na maofisa wa Mahakama kutumia uamuzi (judgement), sheria na kanuni ambazo zinatumika kwa wakati huo hapa na duniani kote;
 • Ili kuhakikisha uwepo wa maadili na uelewa sawa katika upatikanaji wa haki na utekelezaji wa wajibu kwa wananchi kwa wakati.

Ninaliomba Bunge, Serikali na vyombo vyake kuangalia tena kwa makini sheria zinazosimamia Tehama ili zisitafsiriwe au kutumiwa vibaya na hivyo kudhoofisha matumizi ya Tehama katika utoaji haki kwa wakati kupitia upashanaji habari na ukusanyaji wa ushahidi.

Kazi hii inaweza kufanywa kwa makini kuangalia sheria za Tehama na sheria ya makosa ya mtandaoni.

Sisi mawakili na jumuiya ya mawakili kwa ujumla, tukiwa wadau na kiungo muhimu kulingana na malengo ya taaluma yetu kwa mujibu wa majukumu yetu, tumekuwa chombo muhimu cha mabadiliko.

Sisi mawakili pamoja na jumuiya yetu hatuogopi mabadiliko  na tuko tayari kwa mabadiliko. Hatuogopi kusema madhaifu yetu na tuko tayari kukosolewa ili kufungua mlango wa mabadiliko.

Ukiangalia kwa makini majukumu yetu yaliyopo kwenye sheria yetu, utaona wito wetu kila kukicha ni kuomba mabadiliko.

Naomba nifanye marejeo kidogo kwenye kifungu cha 4 cha Sheria ya The Tanganyika Law Society Act, cap 307 ili kukamilisha hoja yangu kuhusu azma yetu kwa pamoja kuhusu mabadiliko ya kimfumo, kisheria na kiutendaji.

Makala hii ni sehemu ya risala iliyohaririwa ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Godwin Ngwilimi, katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.

Itaendelea wiki ijayo

 

1174 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!