Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita Mamlaka ya Vifaa Tiba na Dawa (TMDA) imefanikiwa kukamata  dawa bandia zisizofaa kwa matumizi ya binadamu na mifugo zenye thamani ya Sh milioni 56.966.

Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo inaonyesha kuwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 TMDA ilifanya ukaguzi  maalumu wa dawa za binadamu na mifugo katika mikoa ya Arusha na Kigoma ambako walibaini dawa za mifugo ambazo hazijasajiliwa zenye thamani ya takriban Sh milioni 25 na dawa za  binadamu zenye thamani ya Sh milioni 19.449.

Ukaguzi huo ulihusisha maeneo 162, yakiwemo maduka ya dawa za binadamu 12, maduka ya dawa muhimu za binadamu 68 na maduka ya mifugo 80.

Aidha, vipodozi vilivyopigwa marufuku vyenye thamani ya Sh milioni 122.46 pamoja na bidhaa za vyakula zenye thamani ya Sh 4,397,000 vilikamatwa kutokana na kutokidhi matakwa ya sheria. 

Asilimia 28 ya maduka ya dawa yaliyokaguliwa yalikutwa yakihifadhi dawa katika joto baridi lisilostahili na baadhi ya maduka ya dawa yalikutwa yakiuza dawa za serikali.    

Katika operesheni iliyofanyika mwaka huu wa fedha, mamlaka hiyo imefanikiwa kukamata aina saba za dawa bandia zenye thamani ya Sh 12,495,500.

Kaimu Mkurugenzi wa TMDA, Akida Khea, amesema kuwa ukaguzi huo maalumu ulifanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Ruvuma, Arusha, Geita, Kilimanjaro, Mwanza, Shinyanga, Mara, Singida, Dodoma, Morogoro, Iringa, Mbeya, Kigoma, Rukwa na Kagera.

Khea amesema kuwa katika ukaguzi huo pia waligundua aina saba za dawa bandia zenye thamani ya Sh 12,495,000. 

Khea amesema baadhi ya dawa zilizokamatwa zinatumia majina ambayo yamesajiliwa na mamlaka hiyo lakini uchunguzi wa maabara umebaini kuwa dawa hizo ni bandia.

Aidha, dawa zisizosajiliwa zenye thamani ya Sh 31,934,360 nazo zilinaswa katika msako huo.

Amesema vifaa tiba duni vyenye thamani ya Sh 640,000 zikiwemo glavu za upasuaji na vifaa tiba vya serikali vyenye thamani ya Sh 224,300 vilikamatwa.

Amesema operesheni pia ilibahatika kukamata vifaa tiba ambavyo havijasajiliwa vyenye thamani ya Sh 16,384,750.

Amesema watu kadhaa walikamatwa na majalada 19 yalifunguliwa katika vituo mbalimbali vya polisi ili kuhakikisha kuwa sheria inachukua mkondo wake.

By Jamhuri