Kutokana na umuhimu wa bandari katika nyanja za kiuchumi na kibiashara kwa Tanzania na nchi zinazotumia bandari za hapa nchini katika kuagiza na kusafirisha mizigo yao, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekuwa ikiboresha huduma zake kila wakati kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wateja wake zina ubora wa kiwango cha kimataifa.

 Ili kuharakisha utendaji kazi kisasa katika bandari na kuhudumia meli na mizigo ya wateja kwa ufanisi mkubwa, TPA iliamua kuwekeza katika mifumo ya kazi (Terminal Operations Systems – TOS) ambayo ni; Harbour View, Cargo System, Bill System, Message Interchange System na Integrated Electronic Payment System. Kila mfumo una kazi inayochangia kuleta tija kwa bandari.

Harbour View ni mfumo unaosaidia kupata taarifa za meli zinazoingia na kutoka bandarini. Mfumo huu hutumiwa na mawakala wa meli kutangaza ujio wa meli zao, hivyo meli inapowasili bandarini TPA inakuwa tayari imeshajiandaa kuipokea meli husika. Pia mfumo huu hufuatilia nyendo za meli, kutunza kumbukumbu za meli itakapokuja tena taarifa zinakuwa tayari zipo. Mfumo huu umeunganishwa na mfumo wa malipo ambao hutoa ankara kumwezesha wakala wa meli kulipia tozo za bandari kwa ajili ya huduma zilizotolewa kwa meli husika.

Aidha, kurahisisha na kuharakisha uhudumiaji wa shehena za mizigo bandarini, TPA iliamua kuweka mfumo wa Cargo System kwa ajili ya kuhudumia mizigo. Cargo System ni mfumo ambao unafuatilia taarifa za mizigo wakati ikiwa ndani ya bandari kuanzia mizigo inaposhushwa kutoka melini, taratibu za utunzaji wa mizigo hiyo katika maghala na yadi hadi utokaji wa mizigo hiyo bandarini. Mfumo huu umeunganishwa na mfumo wa taarifa za meli.

Pia mfumo huu umeunganishwa na mfumo wa utoaji ankara kwa ajili ya mzigo kumwezesha mteja kulipia tozo za bandari kwa ajili ya huduma zilizotolewa na TPA kwa mzigo wake.  Mawakala wa forodha hutumia mfumo huu kutoa taarifa za malori na madereva wakati wa kuja kuchukua mizigo bandarini.

Cargo System ni mfumo unaotumika katika utoaji wa vibali vya kuruhusu malori kuingia bandarini kuchukua mizigo na kutoa vibali (gate pass) kuwezesha lori kutoka ndani ya bandari baada ya kupakia mizigo. Mzigo unapotoka ndani ya bandari, askari wa getini atapokea nyaraka kwa dereva, anatumia mfumo huu kuhakiki kujiridhisha kuwa lori limepakia mzigo sahihi na limeshatoka nje ya bandari (gate out).

Mfumo mwingine ni wa Billing System. Mfumo huu umeunganishwa na mifumo ya Harbour View na Cargo System. Kazi ya mfumo huu ni kutoa ankara za tozo za bandari. Ankara hizo hutolewa baada ya kupata taarifa za huduma zilizotolewa kwa meli (kupitia mfumo wa Harbour View) na mizigo (kupitia mfumo wa Cargo System).

Mfumo wa Billing System unatumika kutoa taarifa kwenye mfumo wa Harbour View kuonyesha meli husika imeshakamilisha malipo, hivyo hatua nyingine zinaweza kuendelea kama vile kuruhusu meli kuondoka bandarini. Endapo meli husika itakuwa haijakamilisha malipo haitaweza kuruhusiwa kuondoka bandarini.

Pia Billing System hutoa taarifa kwenye mfumo unaohudumia mizigo (Cargo System) kwamba mzigo husika umeshakamilisha malipo hivyo kuruhusu hatua nyingine ziendelee kama vile kutoa vibali vya kuruhusiwa kutoka ndani ya bandari.

Mfumo mwingine ambao unatumika kurahisisha kazi bandarini ni Message Interchange System (MIS). Mfumo huu unatumika katika kupokea taarifa/ orodha ya mizigo (manifest) baada ya kuidhinishwa na TRA kupitia mfumo wa TANCIS. Orodha hiyo ya mizigo inapopokelewa kutoka TRA mizigo yote inakuwa katika nyaraka moja, hivyo huchambuliwa kutengeneza taarifa ya mzigo mmoja mmoja (bill of lading) kwa lengo la kumwezesha karani wa bandari pindi mizigo inapowasili kwa meli kufanya tallying kuhakikisha orodha ya mizigo iliyopo kwenye manifest kama ipo sawa na ile inayoteremshwa kutoka melini. Baada ya hatua hiyo, taarifa hizo hutumwa kwenda kwenye mfumo unaohudumia mizigo (Cargo System) kwa hatua nyingine za kutoa mizigo bandarini.

Aidha, mfumo mwingine ni Integrated Electronic Payment System (IePS/ e-payment) ambao umeunganishwa na Billing System kwa ajili ya kupokea ankara kumwezesha mteja kulipia tozo za bandari kwa njia za benki na simu. Baada ya tozo za bandari kulipwa, mfumo huu hupeleka taarifa kwenye mifumo ya Billing System na Cargo System kuwezesha vibali vya kutoa mzigo husika kutoka bandarini.

Matumizi ya mifumo hii katika kazi za bandari za kuhudumia meli na mizigo yameonyesha ufanisi mkubwa, kwani imepunguza muda wa kutembea na makaratasi kutoka sehemu moja kwenda nyingine, badala yake taarifa za meli au mizigo hutembea kidijitali.

Mifumo hii imeleta usalama na usahihi wa taarifa, kwani imeepusha watu wasio waaminifu kughushi taarifa kama zingekuwa kwenye makaratasi. Pia taarifa hutumwa na kupatikana kwa wakati na kwa usahihi, ukokotoaji wa taarifa na utoaji wa ankara hufanyika kwa haraka, imewezesha taarifa kuwafikia watumiaji wa bandari wa ndani na nje kwa haraka na imesaidia kuharakisha utolewaji wa huduma za meli na mizigo bandarini.

Matumizi ya mifumo hii imeboresha utoaji wa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam. Pamoja na hatua na maendeleo hayo, TPA imejipanga kuendelea kuboresha mifumo ya bandari kuwa ya kisasa zaidi kwani TPA ipo katika hatua muhimu za kupata mfumo wa kisasa unaoitwa Port Operations System na hatimaye kufanya automation ya shughuli na mitambo ya bandari.

Iwapo una tatizo au swali kuhusu huduma za bandari, usisite kuwasiliana nasi kwa kupiga simu au kutuma meseji za bure kupitia namba 0800110032 au 0800110047.

168 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!