Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, trafiki wamekuwa wakifanya kazi ambayo matokeo yake yamechanganyika pongezi na lawama.

Mpita Njia (MN) anatambua namna watumishi hawa wanavyojitahidi kusimamia sheria za usalama barabarani na hata kufanikiwa kwa kiwango fulani kupunguza ajali- japo kazi wanafanya mchana tu -usiku unatolewa kama ofa kwa wavunja sheria!

Juzi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, akawapa jeuri. Akawaagiza ikibidi sasa wawakamate madereva ‘wakorofi’ wawaweke korokoroni! MN anaamini wengi wataumia.

Pamoja na kazi nzuri ya kurejesha heshima barabarani, Mpita Njia anaona trafiki wamekuwa wababe mno. Wanajenga mazingira ya kuchukua fedha kwa madereva hata kama nafsi zao zinawasuta!

Mpita Njia anatoa mfano wa pale makutano ya Barabara ya Sam Nujoma, Dar es Salaam kwenye mzunguko wa kwenda Chuo Kikuu cha Ardhi. Hapo kwenye ‘service road’ inayoenda Calabash, trafiki wamepafanya ndipo kijiwe chao cha kukusanya fedha. Wameamua kuweka kibanda kabisa kukusanya pesa!

Haki ya dereva ni pamoja na kuwekewa alama za barabarani. Dereva yeyote- mgeni au mwenyeji- anaongozwa na alama. Pale kwenye mzunguko kuna alama za ujanja ujanja zimechorwa chini. Hazionekani kwa urahisi kutokana na kuchakaa, kufunikwa na mchanga na wakati mwingine maji hutuwama. Hali hiyo humfanya dereva asizione.

Mpita Njia ameshuhudia polisi wakijibanza hapo na kuwakamata madereva wengi tu. Mara kadhaa kumeibuka zogo.

MN anauliza, kwanini TANROADS wasiweke alama kubwa za kuonekana katika eneo hili ili madereva wawe kwenye nafasi nzuri ya kutii sheria? Je, TANROADS wana makubaliano gani na trafiki katika eneo hili?

Mpita Njia ameamua kulisema hili ili wahusika waone namna ya kuwasaidia madereva wanaoonewa kwa kuwekewa alama zilizofichika. Hili hata RTO wa Kinondoni anaweza kuanza nalo. MN anashauri kuwa lengo la trafiki liwe kuzuia makosa, na wala si kuvizia ili kukusanya faini ambazo baadhi kwa kweli ni za uonevu. Sh 30,000 kwa usawa huu ni fedha ndefu jamani.

By Jamhuri