Nchini Marekani, mwezi Novemba, 2016 walifanya uchaguzi wa Rais. Aliyekuwa mgombewa wa Chama cha Republican, Donald Trump alishinda katika mazingira yaliyoshangaza wengi. Alimshinda aliyekuwa mgombea wa Democrat, Hillary Clinton. Ingawa Clinton alishindwa katika kura za majimbo, aliibuka mshindi katika kura za wananchi.

Sitanii, hiyo ndiyo Marekani. Si lazima anayechaguliwa na wananchi ndiye awe Rais. Baada ya hapo tulishuhudia kelele za hapa na pale. Tulisikia baadhi ya watu wakidai kuwa baadhi ya Wamarekani walikataa kumchagua Clinton si kwa sababu nyingine, ila u-mwanamke wake. Basi. Clinton, aliwahi kusema kuwa wanawake wamekigonga kioo cha mbingu, ila bado ni kigumu.

Yametokea maandamano kadhaa. Rais (mstaafu) Barack Obama aliwafukuza nchini Marekani wanadiplomasia wapatao 35 wa Urusi kwa maelezo kuwa Urusi ilidukua mchakato wa uchaguzi wa Marekani. Yote hayo sasa ni historia. Yamepita. Januari 20, wiki iliyopita Trump ameapishwa kuwa Rais wa Marekani.

Ahadi za Trump katika hotuba yake ya kwanza ndizo zinaitia dunia hofu. Anasema kuanzia sasa Marekani kwanza. Trump (70) anasema kama ni bidhaa ununue za Marekani kwanza, na kama ni ajira, umwajiri Mmarekani kwanza. Anasema si siri, bali masilahi ya Wamarekani kwanza. Anasema anataka watende na dunia ijifunze kutoka kwao.

Sitanii, nasubiri kuona falsafa za Trump. Amesema atahakikisha anafagia ugaidi katika uso wa dunia. Hii maana yake ni nini? Ametangaza vita. Dunia ijiandae kwa miaka  minne ya vita. Ametangaza anaondoa majeshi ya Marekani sehemu mbalimbali duniani. Hili ni jambo jema akilifanya, ila kwa vurugu zilizoasisiwa na mtangulizi wake George Bush, akiondoa majeshi bila utaratibu, dunia itaangamia.

Maandamano bado yanaendelea nchini Marekani.  Nasubiri kuona jiwe la kwanza la ukuta kati ya Mexico na Marekani. Nasubiri kuona wahamaji milioni 15 akiwafukuza kama alivyoahidi. Nasubiri kuona akiwafutia huduma ya bima ya afya Wamarekani. Nasubiri kuona Trump akizuia Waislam kuingia Marekani kama alivyoahidi. Ingawa ameanza kutoa hotuba za kujikosha, ila hatari inaikabili dunia.

Sitanii, kwa Marekani pamoja na yote yaliyotokea bado Trump ameapishwa kama Rais wa 45 wa Marekani. Hapa kwetu Africa, Desemba, 2016 umefanyika uchaguzi nchini Ghana na The Gambia. Kwa nchini The Gambia, Rais aliyekuwa madarakani kwa miaka 22, Yahya Jammeh, mwanzo alikubali kushindwa, baadaye akabadili mawazo. Nitamzungumzia zaidi huyu ngoja nimguse wa Ghana kwanza.

Nchini Ghana mgombea wa upinzani Nana Akuffo Dankwah, alimshinda Rais aliyekuwa madarakani, John Mahama. Rais Mahama amekubali kushindwa na akakabidhi madaraka kwa Nana. Alichokisema yeye katika hotuba ya kukubali kushindwa kwake ni kuwa wale wote waliokuwa wakimsifia, huku wakijua kuwa hawezi kushinda wakimpa taarifa za uongo laana ya kushindwa kwake i juu yao.

Rais wa Gambia Jammeh, ametangaza kuondoka madarakani mwishoni mwa wiki baada ya tishio la kushushiwa kipigo. Adama Barrow, aliyemshinda Jammeh ameweka rekodi ya kuwa Rais wa kwanza barani Afrika kuapishwa katika nchi ya ugenini. Hapa nieleweke. Si lazima chama tawala kishindwe ndipo uchaguzi uwe huru na wa haki.

Hata hivyo, inakera na kutia kinyaa chama tawala kinaposhindwa wazi, kikasubiri kutumia nguvu za jeshi kubaki madarakani. Kama si Mkuu wa Majeshi wa Gambia kusema asingeruhusu askari wake kupigana vita ya kijinga, huenda hivi unavyosoma makala hii, huko Gambia damu ingekuwa inamwagika. Binafsi napata shinda na uongozi wa nchi zetu.

Sitanii, dhana ya vyama kugombea uongozi na kushinda urais au wabunge wengi kueleza mipango mikakati jinsi gani vyama vitawaletea wananchi maendeleo ya uhakika na kwa haraka, ni ya msingi. Jinsi gani vitadumisha amani, elimu itakuwa bora, barabara, reli, viwanja vya ndege na treni zitakavyofanya kazi kwa ufanisi, ni msingi.

Tunaraji vyama vya siasa kushindana jinsi ya kuhakikisha wananchi wanapata maji, hakuna ujinga na magonjwa yamefutwa katika uso wa nchi. Kwa bahati mbaya, baadhi ya viongozi wanaingia madarakani kulinda heshima zao na si kitu kingine chochote. Kwetu sisi Afrika, nasema wakati umefika. Katika uchaguzi tuzungumze na tukishinda tutekeleze ahadi badala ya kushindania umaarufu. Kwa kulinganisha uchaguzi wa Marekani na huu wa Ghana na Gambia najiuliza, je, Afrika tutafika? Tafakari, chukua hatua.

1601 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!