Kumbe muda wote nilikuwa sikielewi kile kinachoongelewa kuhusu haki za kina mama, nimekuwa nikijiuliza ni kitu gani kinachoitwa haki za wanawake? Muda wote nimejiuliza ni haki gani zinazodaiwa na wanawake?  Sikupata jibu!

Sababu niliamini kwamba wanawake wanapata haki zao kulingana na maumbile yao yalivyo. Muda wote nilikuwa nikijisemea kwamba siku ambayo nitasikia wanawake wamezuiwa kuingia kwenye siku zao, watazuiwa kupata mimba au kunyonyesha, papo hapo na mimi nitaungana nao kuendeleza madai yao, maana hizo ni haki zao zisizokuwa na mbadala.

Lakini kina mama wamekuwa wakiendeleza madai ya haki ambazo sikuelewa ni haki gani? Jambo la kushangaza wamekuwapo hata wanaume wanaojidai kuungana na wanawake kudai haki za kina mama ambazo hazitajwi ni haki gani! Tena wanaume hao wamekuwa wakali zaidi kuliko hata kina mama wenyewe!

Kumbe tatizo nililoligundua ni la kukificha kile kinachomaanishwa, kutopenda kukiweka wazi, huku wanaume wanaolivalia njuga tatizo hilo wakiwa ndio wanaoongoza kulitenda tatizo lenyewe!

Tuseme hao wanalia machozi ya mamba, hiyo ikiwa ni sawa na kujificha nyuma ya kile kinachodaiwa wasiweze kujulikana kuwa wao ndio wahusika wakuu wa tatizo linaloongelewa.

Maana mara nyingi ni vigumu kumfikiria mtu anayesema kuwa kufanya kitu fulani ni kosa, tena kosa la jinai, kuwa mtu huyo ndiye anayeweza kuwa anahusika na kosa hilo!

Mtenda kosa atabaki anatafutwa kusikojulikana, kumbe mhusika ni yuleyule mwenye kulinadi kosa husika! Kumbe mhalifu, kwa mbinu za kigaidi, anajificha kwenye kivuli cha kulinadi kosa hilo.

Ni baada ya kukigundua kitu hicho ndipo nimeamini kuwa kina mama wanacho cha kudai, isipokuwa kitu hicho kinadaiwa kinafiki.

Yaani kudai kitu wakati hutaki kumtaja mhusika wala kuonyesha namna anavyojihusisha na kosa linalodaiwa kutendwa, badala yake kubaki wanamshangilia anayelinadi kosa kuwa ni shujaa!

Kama inavyosemwa bungeni, kwamba kuna baadhi ya wana ndugu wasiotaka kuyaweka wazi matatizo yanayofanywa na baadhi ya wanaume dhidi ya wanawake na mabinti, ikiwa ni njia mojawapo ya kuwafichia siri wanaume hao wabovu wa tabia wasiumbuke. Na kwa kufanya hivyo matatizo dhidi ya kina mama ndipo yanazidi kukua na kukomaa!

Kuna usemi wa wahenga kuwa mficha maradhi, kifo humuumbua. Kwa jinsi hiyo sioni malalamiko yanatoka wapi na kwa nini yaendelee kuwepo! Ni kiasi cha kuwataja wanamaume hao bila aibu kusudi tukalikomeshe tatizo.

Tatizo mojawapo kubwa ni pamoja na ubakaji wa wanawake. Kuna watu, wabakaji, wanaojifanya kusema lugha laini kwa kina mama, kumbe wakiwa ni wanaume waliokubuhu kwa wanawake!

Dawa iliyopo inayoweza kulimaliza tatizo ni kufumba macho na kukiweka wazi kila kinachojiri ndani ya jamii kuhusu kina mama bila kujali aibu itamuangukia yupi. Anayelikataa hilo moja kwa moja anapaswa naye ahesabike ni adui wa wanawake, hata akiwa ni mwanamke mwanyewe.

Fikiria mwanamume aliyempenda binti ambaye hajaanza darasa la kwanza akajitolea kumsomesha darasa la kwanza mpaka la saba, baadaye sekondari ya kulipia kidato cha kwanza hadi cha nne, baadaye kumrudisha kidato cha kwanza tena, baada ya kuwa amefanya vibaya kwenye mitihani ya kidato cha nne, na kuendelea, hatimaye akawa mke wake!

Mtu huyo utamfikiriaje ukisikia anasema haki za wanawake? Kuna haki yoyote hapo? Maana ndugu wa mwanamke walipotaka binti aolewe na kijana wanayeendana kiumri, jamaa, mwanamume, akataka kunywa sumu ili akajiue! Si bora angejiua kuliko kuendeleza ubakaji! Sababu huo ni ubakaji wa kudumu!

Watu wengi wanalielewa hilo ila hawasemi chochote hapo, wakimuona mwanamume huyo kama mwanaharakati wa haki za kina mama! Nasema huo ni unafiki na ushenzi,  ambalo ni tatizo kubwa linapokuja suala hili la haki za wanawake.

Ni kwamba tatizo lipo ila linafunikwa na kitu ambacho katika kabila la Wahaya kinaitwa “kakitandugao”, kwa maana ya acha lisianzie kwangu!

Kwa mtindo huo wa kakitandugao sidhani kama tunaweza kufanikisha jambo lolote, na harakati zote za haki za kina mama lazima ziwe kazi bure.

Ni kama yale yaliyosemwa bungeni ambapo panatokea mtu anamhujumu mtoto wa kike kijinsia, pengine baba mkubwa au mdogo, lakini wanandugu wanaamua kuyamaliza kimyakimya ndani ya familia, badala ya kuyaanika hadharani ili sheria ichukue mkondo wake kusudi yasijirudie.

Kinachofuatia baada ya hapo ni tabia hiyo ovu kukua na kugeuka sehemu mila, ambapo mtoto wa kike kuzaa na baba mkubwa au mdogo, au wakati mwingine mjomba,  linakuwa jambo la kawaida!

Hiyo yote inatokana na kulifuga tatizo kwa kulionea aibu ya ‘kakitandugao’, acha lisianzie kwangu! Tungejitahidi kuifutilia mbali aibu ya aina hiyo tungeokoa mambo mengi upande wa kina mama. Lakini tunapoiendekeza aibu hiyo ya kijinga, tusiyashangae yanayojiri kwa sasa,  maana mficha uchi hazai.

Kwa hiyo mambo ya binti kukutwa na mtoto akisema ni wa baba mkubwa au baba mdogo litakuwa ni jambo la kawaida, si tunaona kutunziana siri za kijinga ndilo jambo la maana!

Walio tayari kupambana na tabia hiyo ovu wanaweza kujitokeza ili tuweze kushirikiana, nina imani tunaweza kushinda. Tusiyaachie mashetani yaendeleze libeneke huku yakijifanya kukipinga kile yanayokifanya! Tusikubali kuyaachia mafisi kazi ya kulinda nyama halafu huku tukisema kwamba  nyama inapotea!

Mimi nadhani tungeachana na unafiki linapokuja suala la kulinda haki za kina mama, tuseme wazi hata kile ambacho hakipaswi kusemwa ili kukomesha tabia hiyo chafu ndani ya jamii, vinginevyo tukae kimya tukiogelea ndani ya bahari ya uovu.

prudencekarugendo@haoo.com

0654031701 – 0784989512

115 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!