Tuishi kirafiki na mazingira tuepuke majanga

Na Dk. Felician Kilahama

Kuna usemi usemao “hakuna lisilowezekana chini ya jua.” Nimejiuliza mara kadhaa chimbuko la usemi huo ni nini, na bado sijapata jibu la uhakika. Pengine kilichomaanishwa ni kuwa na ari ya kutaka kufanikisha jambo muhimu katika maisha.
Vilevile ni kama kusema “penye nia pana njia”, kwa msingi kwamba ukiwa na uthubutu wa kweli utafanya na kufanikiwa. Yote heri, isipokuwa tujitahidi tukimtanguliza Mwenyezi Mungu au kwa maneno mengine “Mungu Kwanza” kabla ya yote.
Hii ni muhimu sana, maana yeye ndiye aliyetuumba na binadamu bila kuwepo nguvu ya Mungu au uwezo wa kimbingu juu yetu ni sawa na kazi bure.
Baada ya uumbaji wa vitu vyote alituumba binadamu kwa sura na mfano wake na akatupa madaraka ya kumiliki na kutawala vitu vyote vilivyopo juu na chini ya ardhi, kwenye maji, pia vilivyopo angani. Kusema kuwa hakuna lisilowezekana chini ya jua ni mtazamo chanya wa kuelekea kwenye dhana ya kumiliki na kutawala.
Ninamshukuru sana Mungu kwa kuwatofautisha binadamu na viumbe wengine. Kwanza, kwa kutuumba kwa sura na mfano wake, kwani hii ni heshima kubwa kwetu.
Pili, kwa kutupa uwezo huo kumiliki na kutawala rasilimali zote duniani isipokuwa kukatazwa kula matunda ya mti uliokuwa katikati ya Bustani ya Edeni.
Hata hivyo, binadamu alishindwa kutii amri hiyo na kusababisha udhaifu kwenye kumiliki na kutawala, hivyo kusababisha laana kumwandama binadamu mpaka leo.
Hali halisi tunayoishuhudia nyakati hizi zenye maafa mengi dunia ni matokeo ya udhaifu uliojengeka miaka mingi sana kutokana na kutotii pamoja na kujengeka ubinafsi zaidi kuliko kuwapo mtazamo halisi wa kutumia rasilimali tulizopewa na Mwenyezi Mungu kwa misingi endelevu na kwa faida ya wanajamii wote au kwa masilahi mapana ya taifa letu.
Kwa hali hiyo, shughuli nyingi za kibinadamu mijini na vijijini zimekuwa na matokeo hasi kwa mazingira. Mathalani, ukataji hovyo wa miti na ufyekaji wa misitu ya asili bila kufuata kanuni za uhifadhi wa mazingira, kuchoma mapori moto au kutotekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi vijijini, kumesababisha misitu ya asili na uoto juu ya ardhi kutoweka.
Kabla na baada ya kupata Uhuru, hali ya mazingira nchini ilikuwa ni ya kijani sana ukiilinganisha na sasa. Ingawa idadi ya watu ilikuwa chini ya milioni 10 wakati tunapata Uhuru, na sasa inakadiriwa kuwa milioni zaidi ya 55 na mifugo zaidi ya milioni 35, hatuwezi kusema ongezeko hilo ndiyo sababu kubwa ya uharibufu wa mazingira kuwa mkubwa kiasi hicho.
Kwa mtazamo wangu, sababu kubwa ni kushindwa kumiliki na kutawala vyote kwa kutumia njia endelevu. Kukosekana utayari wa kutumia rasilimali asilia ikiwemo misitu, wanyamapori, ardhi, maji, samaki na kadhalika kwa misingi endelevu ndiyo chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa maafa na majanga asilia.
Sasa tunalia na athari za mabadiliko ya tabianchi, kumbe kisababishi ni kazi za mikono yetu na kusababisha ongezeko kubwa la joto duniani. Matokeo ni maafa kila mahali, likiwemo Bara la Afrika kukumbwa na njaa, ukame, mafuriko, kupoteza uhai na mali kama nyumba kubomoka au kuezuliwa mapaa.
Uoto wa asili kwenye nchi za Afrika ikiwemo Tanzania umetoweka kwa kasi kubwa sana. Tanzania kwa mfano, inakadiriwa kupoteza misitu ya asili kwa kiwango cha kati ya hekta 370,000 na 470,000 kwa mwaka kutegemea hali halisi ya mahalia.
Hivyo, maeneo mengi nchini hayana uoto wa asili kama ilivyokuwa miaka iliyopita. Kila kukicha uoto wa asili, yaani nyasi, mimea, miti na misitu vinapotea kwa kiwango kikubwa. Ndiyo maana kwa nyakati hizi, tofauti na zamani, mvua ikinyesha baada ya muda mfupi tu mafuriko yanatokea. Vilevile, msimu wa mvua ukiisha baada ya muda mfupi upatikanaji wa maji unakuwa wa shida (chemchemi zinakauka na mito mingi kuwa na maji machache).
Kwanini zimekuwepo athari hizo nyakati hizi kuliko zamani? 
Binadamu, pamoja na idadi ya watu kuongezeka, hatuishi kirafiki na mazingira au hatumiliki na kutawala kwa kuzingatia misingi sahihi. Badala yake, tumekuwa waharibifu wa mazingira na sasa yanatugeuka na kutuangamiza.
Miaka ya nyuma mvua zilikuwa zikinyesha za kutosha. Nakumbuka nikiwa kijana miaka ya 1950 na 1960 mvua za masika zilikuwa nyingi kiasi cha kushindwa kupata kuni za kupikia chakula. Kaya nyingi zililazimika kuweka kuni za kutosheleza mahitaji nyakati za masika kinyume cha hapo “mtapiga miayo” kutokana na njaa kwa kukosa nishati ya kupikia — kisa mvua nyingi wakati wa masika.
Pamoja na mvua hizo nyingi, mafuriko makubwa au kubomoka kwa madaraja yalikuwa ni matukio ya nadra sana tofauti na hali ilivyo sasa. Hali ilikuwa salama zaidi kuliko sasa, maana tulikuwa bado tunaishi kirafiki na mazingira, hivyo uoto wa asili ulikuwepo wa kutosha.
Kwa maneno mengine, kukiwepo na uoto wa asili wa kutosha maji ya mvua huingia ardhini taratibu na hatimaye kutiririka kwenye mito hata nyakati za kiangazi lakini pia ardhi/udongo kuhifadhiwa. Hivyo, kutokuwepo uoto wa asili wa kutosha athari kwa ardhi/udongo na upatikanaji wa maji nyakati za kiangazi ni kubwa sana.
Ongezeko la watu au mifugo kwa mtazamo wangu havijawa tishio kwa maisha yetu, hasa tukizingatia kuwa Tanzania Bara inalo eneo kubwa takriban hekta zaidi ya milioni 88. Kwa idadi ya watu milioni 55 ni sawa na kila mtu kumiliki hekta karibu 1.6 na familia ya watu 10 watakuwa na hekta 16.
Kwa idadi ya mifugo takriban milioni 35, ni sawa na mtu mmoja kuwa na mfugo mmoja. Hii inaonyesha kuwa kiuhalisia bado ardhi inatosha isipokuwa matumizi yake si endelevu. Sehemu mbalimbali nchini tunalima kwa kufyeka misitu ya asili (kilimo cha kuhamahama), hatufugi, tunachunga mifugo.
Ardhi inatumika kama haitakiwi kwa vizazi vijavyo. Matokeo yake ni kutoweka uoto wa asili, hivyo maji ya mvua kusababisha mmomonyoko mkubwa wa udongo.
Matokeo yake ni ukame na njaa kutokana na kilimo duni. Maji ya mvua yakishindwa kuingia taratibu ardhini, hivyo kusomba udongo na kila aina ya takataka na kupelekwa mabondeni na kwenye mito.
Hali hiyo inasababisha vina vya mito kupungua kutokana na kujaa udongo, mchanga, matope na takataka za kila aina, zikiwemo plastiki.
Mfano, Mto Msimbazi (jijini Dar es Salaam) umesheheni mchanga na uchafu wa kila aina. Hivyo, maji ya mvua husambaa haraka na kusababisha mafuriko wakati wa mvua. Madaraja na barabara kubomoka ni matokeo ya maji ya mvua kutoingia ardhini na badala yake kujaza mito haraka. Isitoshe njia za asili ambazo maji ya mvua hupita zimezibwa, hivyo kusababisha maji kuzagaa sehemu ambazo hayastahili kuwapo.
Maji yanapokuwa mengi yanapata nguvu sana na yanapofika kwenye madaraja na kwa sababu kina cha mto kimepungua sana, maji hupita kwa shida, hivyo kusambaa juu ya daraja na wakati huo yakimomonyoa udongo ulioshikilia nguzo za madaraja, hatimaye hubomoka na kusababisha hasara kubwa sana.
Tukubali kuwa sasa hali ni mbaya kutokana na kutoishi kirafiki na mazingira ambayo yamegeuka kuwa mwiba kwetu kiasi cha kusababisha madhara makubwa kwa jamii na taifa zima. Tujirudi, turekebishe tulikokosea.
Tuzingatie matumizi sahihi ya rasilimali ardhi, tulime kitaalamu na kilimo kiwe kijani, kingo za mito zihifadhiwe na sheria zisimamiwe ipasavyo.
Tuwe wafugaji bora badala ya mazoea ya kuchunga mifugo na tuhakikishe tunazalisha mazao ya kilimo au mifugo kwa tija kubwa kwa kutumia eneo dogo la ardhi. Kwa ufupi: Tufanye yote kwa kuzingatia umuhimu wa kuishi kirafiki na mazingira ili tuepuke vifo na kupoteza mali kwa sababu mazingira yakiharibiwa yanalipa kisasi bila huruma.
Tuchukue hatua sasa na kutimiza wajibu wetu ipasavyo kwa kufanya kazi kwa bidii huku tukitunza mazingira kwa faida yetu na vizazi vitakavyofuata.
 
Dk. Kilahama ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Uhifadhi wa Maliasili na Mazingira (WCST).
 
Caption
Sehemu ya misitu ya Uluguru mkoani Morogoro ambayo imeanza kubaki bila miti kutokana na shughuli za kibinadamu.

Mwisho