Tujenge Uzalendo Kupitia Uchumi

Wiki iliyopita nchi yetu imesherehekea miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara). Wakati tunapambana kupata uhuru, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyeongoza harakati hizo, alisema nchi yetu ilikuwa inapambana na maadui watatu; ujinga, maradhi na umaskini. Na alisema ili nchi ipate mafanikio inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Ukipima kigezo cha siasa za kufanya uchaguzi, naamini Tanzania tunapasi. Ila usiniulize kura zinahesabiwaje. Lakini angalau kila miaka 5 tunaionyesha dunia kuwa tunafanya uchaguzi. Angalau tunazo awamu tano sasa zilizoingia na kutoka madarakani kwa njia ya sanduku la kura. Watanzania tunapaswa kupongezana kwa hili.
Watu wapo. Leo nchi yetu inakadiriwa kuwa na watu wasiopungua milioni 56. Idadi hii ni nguvu kazi ya kutosha na ni soko la kutosha. Ila tu, tabu ninayopata ni kila ninapoingia dukani kutokuta bidhaa iliyoandikwa “Made in Tanzania”. Sisi tumekuwa wachuuzi, tunachukua bidhaa kutoka nje ya nchi na kuongeza cha juu kisha tunauza tukidhani tunajenga uchumi wa taifa letu.
Ardhi ipo, ila ardhi yetu hatujaitumia vyema. Nilitaraji tuwe na kilimo kikubwa na cha kisasa. Tunahitaji mtu au kampuni moja kuwa na shamba linalozalisha mahindi tani 300,0000 hadi 1,000,000. Nikisema hivi, watu wanashangaa. Leo tuna kilimo cha muhogo kutoka China. China wanataka tani 1,200,000 kwa mwaka. Nchi yetu haina uwezo wa kuzalisha kiasi hiki.
Sitanii, nafahamu sisi vyombo vya habari tunapata wakati mgumu chini ya uongozi wa Rais John Magufuli ambapo magazeti yemefungiwa au kufutwa kuliko wakati wowote. Bunge live imezuiwa. Mikutano ya hadhara kwa wanasiasa imesitishwa. Hii ina maana hata CCM wamejinyima fursa ya kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara.
Hata hivyo, ukiniuliza mimi kama mimi nasema nakubaliana na Sera ya Rais Magufuli ya Tanzania ya Viwanda. Anachagiza sera hii kwa kusema “Hapa Kazi Tu.” Niliamini, hata leo naendelea kuamini kuwa nchi yetu haiwezi kufuta umaskini ikiwa tutaendelea kutokuwa na viwanda. Viwanda vinazaa uzalendo. Uzalendo kwa maana kwamba vijana watakuwa wanafanya kazi, wanapata fedha na kujenga nchi.
Ni vigumu mtu aliyelala njaa kumhamasisha awe mzalendo. Serikali iweke mazingira wezeshi kuwafanya Watanzania waipende nchi yao. Tukijenga viwanda vya kutosha. Tukapata ajira za kutosha na zenye malipo mazuri, basi nchi yetu watu wataanza kuimba nyimbo za sifa na mapambio. Ni bahati mbaya kuwa hadi sasa baadhi ya viongozi wasaidizi wa Rais Magufuli hawafahamu wafanye nini kutuondoa katika umaskini.
Maradhi tunapambana nayo kwa kasi kwa kujenga hospitali, vituo vya afya na zahanati, lakini tungeweza kuwa na watu wenye afya zaidi kwa kuwawezesha wakawa na kipato kikubwa wakala mlo kamili iwapo tutakuwa na viwanda vingi vikazalisha ajira tukauza bidha ndani na nje ya nchi.
Uchumi imara ni kichochoe cha kujenga uzalendo. Rais Magufuli amewahi kusema kuwa “hivi hao wanaomiliki viwanda wana DNA za aina gani?” Ninachokiona sisi sote tunaweza kumiliki viwanda na kujenga uchumi imara tukiamua kuwezesha. Miaka 56 sasa tumekuwa na uhuru wa bendera inapeperuka, lakini si haki kabisa kampuni moja ya Bombardier kuwa na uchumi mkubwa kuliko taifa letu.
Sitanii, tukatae unyonge huu. Nchi yetu haiwezi kujikomboa kiuchumi ikiwa haina viwanda. Nchi zilizotuzunguka ikiwamo Malawi, Msumbiji, Zambia, DRC, Rwanda na Burundi ni soko kubwa ajabu kwa bidhaa tunazoweza kuzalisha. Naomba kuhitikisha kuwa wakati tunashrehekea miaka 56 ya Uhuru, tuongeze moto katika safari ya ujenzi wa viwanda.