Kupatikana teknolojia ya kukausha tumbaku kwa kutumia nishati jadidifu inayotokana na jua nchini China ni jambo la kuigwa na wakulima wa tumbaku kutoka katika mikoa inayolima tumbaku hapa nchini ili kuinusuru misitu inayoteketea.

Teknolojia hiyo iliyogunduliwa katika nchi za China na Italia, endapo italetwa hapa nchini itachangia kulinda misitu ya asili katika kuhifadhi mazingira. Misitu inateketea kutokana na wakulima kukata miti kwa ajili ya kukaushia tumbaku ambapo ekari moja inahitaji kuni meta za ujazo 5 hadi 24 kukaushia.

Ekari moja ya tumbaku kwa Tanzania inakadiriwa kuzalishwa kilo 450 inayotumia kiasi hicho cha kuni kuikausha wakati China ekari moja wanakadiriwa kuzalisha kilo 847 kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kilimo Duniani (FAO).

Endapo itatumika teknolojia hiyo ya kukausha tumbaku kwa kutumia nishati jadidifu ya jua hapa nchini itaokoa ekari zaidi ya 99,000 za misitu ya asili inayokatwa kwa mwaka kwa ajili ya kukaushia tumbaku.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa nishati jua kwa ajili ya kukausha tumbaku kutoka asasi isiyokuwa ya kiserikali inayoshughulika na nishati jadidifu Tanzania (Tanzania Renewable Energy Association (TAREA), Godwin Msigwa, teknolojia hiyo ya mabani yaliyotengenezwa kwa ajili ya kukaushia tumbaku kwa kutumia nishati jadidifu kwa sasa inatumika katika nchi mbili ambazo ni Italia na China.

Ugunduzi wa teknolojia hiyo ulitokana na kukabiliana na uharibifu wa mazingira ambapo amesema katika Bara la Afrika asilimia 90 ya tumbaku inazalishwa katika maeneo ambayo yana miti aina ya miyombo, ambapo hekta milioni 1.9 ina miti hiyo ambayo ni sawa na asilimia 51 ya misitu yote Afrika.

Amesema katika Afrika Mashariki; Tanzania, Kenya na Uganda hakuna nchi inayotumia teknolojia hiyo kukaushia tumbaku isipokuwa kwa Afrika ni nchi ya Zimbabwe ndiyo imeanza kutumia mabani hayo yanayochangia kwa kiasi kikubwa uhifadhi wa mazingira.

“Zimbambwe hivi sasa wamepiga hatua kubwa katika kuilinda misitu ya asili kutokana na kuachana na matumizi ya kuni kukaushia tumbaku, hiyo ni  baada ya kuingiza teknolojia ya mabani yanayotumia nishati jadidifu kukaushia tumbaku, jambo ambalo linafaa kuigwa na wadau wa tumbaku hapa nchini,” amesema Msigwa.

Msigwa amesema Tanzania tumbaku inalimwa zaidi upande wa Magharibi, ukiwemo Mkoa wa Tabora ambako asilimia 60 ya tumbaku hapa nchini inazalishwa na asilimia 40 inazalishwa upande wa Kusini Mkoa wa Ruvuma na Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania Mkoa wa Mbeya na Iringa, maeneo ambayo hivi sasa yanakumbwa na changamoto za kuteketea kwa misitu ya asili.

Mwaka 2017 ulifanyika utafiti kuhusiana na namna ya kutumia nishati isiyotokana na mafuta, gesi na makaa ya mawe (Biomas Energy Conservation) kwa uhifadhi wa mazingira uliofanywa na Kampuni ya PROBECE ambayo iliwashirikisha taasisi ya serikali ya utafiti wa zao la tumbaku (TORITA) na kampuni za ununuzi wa tumbaku hapa nchini  (ALLIANCE ONE) na Muungano wa Wafanyabiashara ya Tumbaku Tanzania (Association of Tobacco Traders Tanzania (ATTT) kwa lengo la kuwashawishi kutumia nishati jadidifu kukaushia tumbaku.

Amesema mwaka 2006 ulifanyika uchunguzi Songea na kuonyesha kwamba asilimia 88 ya kuni kavu inatoka kwenye misitu ya asili na kuni asilimia 12 zinatoka kwenye misitu wa kupanda, wakati mwaka 2017 kwa Mkoa wa Tabora utafiti uliofanywa na kamati ya wataalamu ilionyesha kwamba asilimia 91 wakulima wa tumbaku wanategemea kuni kutoka katika misitu ya asili na asilimia 9 wanategemea misitu ya kupanda.

Kutokana na uchunguzi huo, ndiyo maana ipo haja sasa ya kuweka mkazo kwenye teknolojia hiyo ya mabani yanayotumia nishati jadidifu kutoka nchini China ambayo itaokoa misitu ya asili inayoteketea.

Msigwa amesema kwamba moja ya sifa ya mabani hayo, unaweza kurekebisha kiwango cha joto linalotakiwa kukaushia tumbaku kulingana na uhitaji wa soko la dunia ambalo linaweka viwango vya ukaushaji wa tumbaku.

Mabani hayo hayapotezi ubora wa tumbaku kwani hutoa ubora unaofanana kama ni daraja la pili, basi yote inakuwa hivyo na kama daraja la kwanza yote inakuwa daraja hilo, jambo ambalo kwa Tanzania yakitumika mabani hayo hakuna tumbaku itakayoachwa kwenye soko na kipato cha wakulima kitaongezeka  kutokana na ubora utakaopatikana.

“Mabani ya kisasa yatapunguza vifo vinavyotokana na wakulima kufia kwenye mabani yaliyotengenezwa kienyeji, maarufu kwa jina la matembe, wakulima kutoathirika mapafu na macho kutokana na moshi mkali ndani ya matembe.

“Mabani hayo yanayotumia nishati jadidifu yanaweza kuhamishwa kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine kukausha tumbaku na yanajulikana kwa jina la Tobacco Curing Solar Photovoltaic,” amesema Msigwa.

Kwa upande wake, Ugo Mapunda, ambaye ni Mtafiti Mkuu wa masuala ya mbegu za tumbaku na namna ya kuikausha kutoka Taasisi ya serikali ya TORITA, amesema hakuna teknolojia hiyo hapa nchini lakini wanafanya mazungumzo na Wataalamu kutoka nchini China kuangalia uwezekano wa kuileta teknolojia hiyo.

Mapunda amesema mabani hayo ya kukaushia tumbaku kwa kutumia nishati jadidifu yatakuwa suluhisho la kudumu la tatizo la tumbaku kuwa adui wa misitu ya asili.

Amesema gharama za mabani hayo yanayotumia nishati jadidifu ni dola za Marekani 25,000 hadi 50,000 ambazo ni wastani wa shilingi milioni 57.5 hadi shilingi milioni 115 kulingana na ukubwa.

Takwimu zinaonyesha kwamba tumbaku inayolimwa hapa nchini inachangia asilimia 4 ya uharibifu wa misitu kwa mwaka kutokana na kuni za kukaushia tumbaku.

Afisa Misitu wa Manispaa ya Songea, Godfrey Luhimbo, akishirikiana na Afisa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Songea, Juma Mbwambo, wanasema zinatumika mita za ujazo 5 za kuni, sawa na miti 2 mikubwa yenye umri wa miaka 50. Miti hiyo inakuwa na kipenyo cha sentimita 30 hadi 50 na urefu wa mita 6 hadi 9 ambapo mti mmoja unatoa kuni mita za ujazo 3 hadi 4.

Kwa hiyo kuni mita za ujazo 12 hadi 24 zinatumika miti 4 hadi 10, ambapo kuni hizo zinaweza kubebwa kwenye lori tani saba au Fuso tani 3.5 kwa ajili ya kukaushia tumbaku kilo 450 tu.

Wanasema Songea na Namtumbo katika msimu wa kilimo 2018/2019, wakulima wanakadiriwa kuzalisha tumbaku kilo milioni moja kutoka katika ekari zisizopungua 2,222 ambazo zitatumia kuni mita za ujazo 11,110 kukaushia ambazo ni wastani wa miti 4,444 sawa na ekari 18 za msitu wa asili utakaoteketea Songea na Namtumbo, eneo linalolimwa sana tumbaku.

Salim Brashi, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Songea na Namtumbo (SONNAMCU), amesema kilimo cha tumbaku mkoani Ruvuma ni kama kinaanza upya baada ya kushuka uzalishaji kutoka tani 9,000 miaka ya 1996/1997 hadi wastani wa tani 49 mwaka 2014/2015, msimu ambao kampuni za ununuzi wa tumbaku TLTC na ALLIANCE ONE zisitisha kununua tumbaku mkoani humo.

Amesema kwa msingi huo mwaka 2015/2016 hapakuwa na uzalishaji wa tumbaku hadi ilipofika mwaka 2016/2017 ilipojitokeza kampuni moja ya tumbaku na kuhitaji tani 200 lakini zilizalishwa tani 160 tu.

Brashi amesema msimu wa kilimo 2018/2019 wameingia mkataba na kampuni hiyo yenye uhitaji wa tani 1,000 sawa na kilo milioni moja, ambapo wakulima 2,250 watatumika kuzalisha tumbaku hiyo.

Brashi amesema kampuni za nje zilisitisha biashara hiyo kwa walichodai kwamba wakulima walishindwa kutekeleza suala la upandaji miti kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira, lakini pia waliona wakulima hawapati manufaa kutokana na biashara hiyo ya tumbaku.

Amesema wanunuzi hao wa nje hawataki tumbaku ya moshi ‘Dark Fire Cured’ iliyokaushwa kwa nishati jadidifu kwa madai haiwezi kuwa na kionjo (ladha) wanachokitaka kinachotokana na moshi.

Mkulima Issa Ponera wa Kijiji cha Mgombasi, wilayani Namtumbo ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Tumbaku Tanzania anayewakilisha wakulima wa zao hilo, amesema hajawahi kusikia suala lolote kuhusiana na matumizi ya nishati jadidifu kukaushia tumbaku, bali tumbaku ya mvuke ‘Flue Cured Tobacco’ ambayo inazalishwa kwa wingi nchini.

“Suluhisho la kuteketea kwa msitu wa asili katika maeneo yanayolimwa tumbaku ni nishati jadidifu ambayo itasaidia kupunguza kama si kuondoa kabisa uharibifu wa mazingira unaotokana na kukata miti ovyo kwa ajili ya kupata kuni za kukaushia tumbaku,” amesema Ponera.

Kwa mujibu wa Meneja wa Bodi ya Tumbaku Tanzania Mkoa wa Ruvuma, Issa Issa, zao hilo linaharibu mazingira kutokana na kutumika kwa kuni nyingi wakati wa kukausha tumbaku na kwamba hadi sasa hapa nchini hakuna utafiti uliofanyika wa nishati jadidifu kutumika kukaushia tumbaku.

China wanaongoza duniani kwa kuzalisha tumbaku kutokana na taarifa za Shirika la Kilimo Duniani (FAO), ambapo China pekee wanazalisha tumbaku asilimia 42, Marekani asilimia 7, Umoja wa Ulaya asilimia 4 na nchi zingine zote kwa pamoja duniani zikiwemo Malawi, Zimbabwe, Tanzania, Brazil na India zinazalisha asilimia 47.

By Jamhuri