‘Tumeuza kila tulichonacho, hatuwezi kutoka Muhimbili’

Mkazi wa Wilaya ya Songea Vijijini, mkoani Ruvuma, Sijawa Jafar, mwenye umri wa miaka 35 ameiomba serikali na wadau mbalimbali kujitokeza kumsaidia kulipia gharama za matibabu ya mumewe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zinazofikia Sh milioni 3.7, baada ya familia hiyo kushindwa kupata fedha hizo.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, Sijawa ameiomba serikali na wadau mbalimbali kumsaidia kulipa gharama hizo baada ya jitihada za kupata fedha hizo kushindikana.

Mama huyo amesema anakumbuka ilikuwa Juni 16, mwaka huu katika Kijiji cha Igela, Kitongoji cha Mnamali, wilayani Songea, mkoani Ruvuma, mumewe aitwaye Hassan Swalehe, mwenye umri wa miaka 30, aliondoka asubuhi kuelekea shambani kwao kwa ajili ya kuvuna ufuta na mahindi.

Mama huyo amezidi kusimulia mkasa uliomkuta mumewe, kwa kusema baada ya kupita muda tangu mumewe aondoke nyumbani, baadaye ikiwa imetimu saa nane mchana, akaona watu kadhaa wakija nyumbani kwake huku wamembeba mumewe kwenye pikipiki.

Amesema baada ya kuwahoji watu hao waliomleta mumewe, walimwambia kwamba walimwokota akiwa ameangukiwa pikipiki ndipo walipoamua kumpatia msaada wa kumleta nyumbani, kwa kuwa walikuwa wanajua anapoishi.

“Baada ya kumhoji mume wangu, aliniambia kwamba alipokuwa anakwenda shambani huku akiendesha pikipiki yake kwa lengo la kuangalia mazao ili ayalete nyumbani, ghafla akiwa kwenye mwendo alisikia sauti nyuma kama honi ya pikipiki nyingine inayohitaji kupishwa japokuwa hakuwa anaiona kwenye kioo chake, alipisha ili ipite ndipo alipopinduka hapohapo,” amesema mama huyo.

Ameongeza kuwa baada ya hapo wakiwa na ndugu na wanakijiji wengine wakampeleka katika Zahanati ya Matepwende ili kupata matibabu na walipofika hapo madaktari walisema ugonjwa wake ni mkubwa, hawawezi kuutibu, lazima apatiwe rufaa kwenda katika hospitali ya mkoa.

Sijawa amesema kuwa kutoka hapo kwenda katika hospitali ya mkoa ni mbali, kama kilometa 15, hivyo ilibidi wakodi gari kwa gharama ya Sh 155,000 kutoka katika zahanati hiyo.

Mama huyo amesema walipofika katika hospitali ya mkoa, mumewe alilazwa hospitalini hapo kwa takriban wiki mbili na kupatiwa matibabu na walipomfanyia vipimo waligundua amevunjika uti wa mgongo, na hapo walitumia Sh milioni moja kwa ajili ya gharama za matibabu.

Ameongeza kuwa matibabu yaliendelea na mwishowe madaktari walipoona hali yake inakuwa mbaya bila mafanikio, waliamua kumwandikia mgonjwa wake rufaa ya kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Walipopatiwa rufaa kwenda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili walikuwa hawana fedha za matibabu, hivyo wakalazimika kwenda kijijini kuuza mashamba na nyumba yao ili wapate fedha za kumudu kumsafirishia na kumhudumia mgonjwa.

Sijawa anakumbuka kwamba walipata mteja wa kununua mashamba yao na kuwalipa Sh milioni mbili ambazo hata hivyo hazikufua dafu kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa kuliko uwezo wa familia yao.

Baada ya kufika Muhimbili walikuwa na kiasi cha Sh milioni mbili ambazo zilitokana na mauzo ya shamba pamoja na mazao yaliyokuwa yamevunwa. Sijawa anakumbuka kwamba siku ya kwanza wakiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili walilipa Sh 100,000 ndipo wakapewa wodi na kesho yake wakatakiwa kulipa Sh 210,000 kwa ajili ya vipimo.

Mama huyo amesema baada ya hapo walilipa  Sh 50,000 za kipimo kingine na baada ya hapo wakalipia dawa Sh 200,000 kabla ya kutakiwa kulipa Sh 200,000 kwa ajili ya operesheni na baadaye dawa zenye thamani ya Sh 270,000.

Amesema baada ya hapo wakaandikiwa tena dawa zenye thamani ya Sh 145,000, na dawa maalumu kila siku zenye thamani ya Sh 20,000, sambamba na gharama ya chakula, pampers, maji pamoja na Sijawa ambaye amekuwa akimuuguza mumewe, matumizi yake kwa siku ameyakadiria kuwa Sh 20,000.

Baada ya kuishiwa fedha, Sijawa akaenda katika uongozi wa hospitali kuomba mgonjwa wake apewe chakula, wauguzi wakamwambia kwamba wanaostahili kupewa chakula ni wale wenye bima ya afya pamoja na wasiokuwa na ndugu na wale wanaotokea mikoani.

Sijawa ameliambia JAMHURI kuwa maisha ya kuuguza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili yamekuwa magumu kutokana na gharama za kula na kujihifadhi wanazolipia kwenye banda la Coca- Cola.

Mama huyo ameiomba serikali kuangalia upya suala la malipo kwa watu wanaopewa rufaa kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kuondoa adha ya mrundikano wa wagonjwa walioruhusiwa baada ya madaktari kujiridhisha kuhusu afya zao.

Amesema mgonjwa wake ameruhusiwa tangu Agosti 12, mwaka huu lakini hadi sasa amekwama kumtoa mgonjwa wake kutokana na uwezo wake mdogo wa fedha, hivyo kushindwa kumudu gharama anazotakiwa kulipa.

Ameongeza kuwa hali ya maisha huko nyumbani kwao kijijini sasa yamekuwa ya kutangatanga kwani wamewaacha watoto wanne ambao wamekuwa hawana msaada zaidi ya kusaidiwa na ndugu na majirani.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Igela, Athumani Nchimbi, amesema mgonjwa huyo alipokuwa katika hospitali ya mkoa mke wake alikwenda kuomba msaada na wao kama kijiji walichangia Sh 300,000  kwa ajili ya kusaidia gharama za matibabu.

Nchimbi ameiomba serikali kuwasaidia na kuwaangalia watu wenye kipato duni, wawasaidie kulipia gharama za matibabu au kufutwa kabisa gharama hizo, kwani ni mzigo kwa mwananchi wa kipato cha chini.

Kiongozi wa Idara ya Ustawi wa Jamii hospitalini hapo,  Emmanuel Mwasota, amesema kila mgonjwa mwenye shida anatakiwa kufuata utaratibu na sheria pindi anapokuwa anahitaji msamaha wa kulipiwa gharama za matibabu ya mgonjwa wake.

Mwasota amesema kama mtu anakwenda kwenye idara yake, atapatiwa utaratibu wa kulipiwa gharama za matibabu baada ya kuona hakuna kabisa uwezekano wa ndugu, jamaa na marafiki kumlipia gharama mgonjwa.