Mahabusu wawili wamemwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, wakidai wanashtakiwa kwa kosa la kuua ilhali aliyefanya mauaji hayo na kukiri yuko huru uraiani.

Michael Laizer na Lucas Mmasi, wanashikiliwa katika Gereza Kuu Mkoa wa Arusha, Kisongo, tangu mwaka 2015 wakikabiliwa na shtaka hilo wanalodai kuwa ni la kubambikiwa.

Barua hiyo ambayo JAMHURI imeona nakala yake, ina maelezo ya Laizer na Mmasi wanaodai kuwa wamebambikiwa kesi ya mauaji P.I Na. 17/2015 lakini kesi hiyo hiyo inamkabili mtuhumiwa mwingine ikiwa imepewa P.I Na. 14/2015.

Watuhumiwa hao wanasema kinachothibitisha malalamiko yao ni kitendo cha kesi zote hizo mbili zinazohusu tukio moja kutajwa kwa hakimu mmoja katika mahakama iliyopo Arumeru mkoani Arusha. Jina la hakimu huyo tunalihifadhi.

“Tunayo huzuni kubwa, na kipekee kabisa tunapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia fursa hii ya kufikisha malalamiko yetu mbele yako [Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi] kwani tunaamini kabisa kwamba sasa haki yetu itapatikana,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Wanasema mtu ambaye wanatuhumiwa kumuua, Julius Tarangei, aliuawa na mtu mwenye kifupisho cha jina F.M.

“Mtu huyo (F.M) aliripoti mwenyewe Kituo cha Polisi na baadaye alifikishwa mahakamani na kusomewa shtaka la kuua bila kukusudia likiwa ni P.I Na. 14/2015 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arumeru. Katika kesi hiyo sisi tulikuwa mashahidi. Baadaye mtuhumiwa huyo alidhaminiwa na mpaka sasa [wakati wa kuandikwa barua] yuko nje kwa dhamana,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Laizer na Mmasi wanadai kuwa siku sita baada ya mtuhumiwa huyo kuachiwa, waliitwa kituo cha polisi na kuwekwa rumande; na siku iliyofuata wakapelekwa mahakamani na kusomewa shtaka la mauaji ya kukusudia. Kesi hiyo ni P.I Na. 17/2015.

“Ni jambo la kushangaza kwa polisi wakishirikiana na mawakili wa Serikali kufungua mashtaka mawili tofauti kwa mauaji ya mtu mmoja.

“Ni wazi kuwa baada ya kumfungulia F.M shtaka la kuua bila kukusudia sisi tungekuwa mashahidi katika kesi hiyo ila baada ya F.M kupewa dhamana na kutoroka, polisi wakaamua kutukamata sisi na kutufungulia mashtaka ya kuua kwa kukusudia…Hivyo, sasa kuna kesi mbili tofauti mahakamani zote zikiwa za kosa la kumuua mtu mmoja,” wanadai.

Mahabusu hao wanadai kuwa majalada yote mawili bado yanatajwa mahakamani yakimhusu marehemu mmoja, na upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Wanadai kuwa wamelalamika kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), lakini wamepewa majibu ya mdomo kuwa hawawezi kuachiwa hadi F.M akamatwe kwa kuwa hahudhurii mahakamani.

“Jeshi la Polisi linashindwa kumkamata mtu ambaye alidhaminiwa baada ya taarifa zake zote kuwepo? Tunaambiwa na ndugu na jamaa wanaokuja kutusalimu kuwa mtuhumiwa huyo yuko mjini Arusha anaendelea na biashara zake, japo taarifa hizi hatuna uhakika nazo, maana huu ni mwaka wa nne sisi wanyonge tuko gerezani tunateseka.

“Jambo jingine la kushangaza ni kuwa hadi leo [wakati wa kuandika barua] hatujawahi kutoa au kuchukuliwa maelezo, isipokuwa yale tu ambayo tuliyatoa kama ushahidi kwenye kesi ya kwanza ya kuua bila kukusudia P.I Na. 14/2015 inayomkabili F.M.

“Mheshimiwa, tunaamini kwa mamlaka mliyonayo mnaweza kuitisha majalada hayo na kuyapitia,” wanasema.

Mahabusu hao wanasema mtuhumiwa F.M baada ya kumuua Tarangei, alikwenda mwenyewe polisi kutoa taarifa.

“Alipopelekwa mahakamani na kupewa dhamana ndugu wa marehemu wakaanza kulalamika ndipo sisi Mmasi na Laizer tukaitwa polisi na kuwekwa rumande. Taarifa tulizonazo ni kuwa F.M ametuma ndugu zake na kwenda kwa ndugu za marehemu kuona namna ya kumaliza tatizo hili.

“Tunaomba vyombo vya haki vinavyohusika vije gerezani vituhoji ili vipate ukweli kamili kuhusu kesi hii ambayo tumebambikiwa.

“Tunaomba sana mtusaidie tuondokane na haya mateso huku gerezani. Hali ya huku ni mbaya sana, hakustahili kuishi binadamu hasa asiye na kosa. Familia zetu zimesambaratika, tunaomba tutendewe haki,” wamesema.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lugola, amezungumza na JAMHURI na kuomba muda afuatilie malalamiko ya mahabusu hao.

“Hiyo barua yao sijaipata, lakini kama mnayo naomba mnisaidie – mniletee niifanyie kazi,” amesema Waziri Lugola.

Machi 14, mwaka juu, DPP Biswalo Mganga, akiwa mjini Dodoma, alizungumza na waandishi wa habari na kutangaza kumwachia huru mwananchi aliyebambikiwa kesi ya mauaji mkoani Tabora.

Alisema hatua hiyo ilitokana na uchunguzi ulifanywa kwa maagizo ya Rais John Pombe Magufuli, aliyesoma barua ya msomaji iliyochapishwa kwenye Gazeti la Majira la Machi 6, mwaka huu.

Baada ya kuisoma barua hiyo, Rais aliiagiza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ifuatilie malalamiko ya mwananchi huyo kwa haraka ili kujua ukweli.

Kwenye barua hiyo, mlalamikaji Musa Sadiki, alieleza jinsi askari wa Kituo cha Polisi Tabora Mjini walivyomkamata na kumnyang’anya Sh 788,000, simu ya mkononi na mali nyingine alizokuwa nazo kabla ya kumfungulia mashtaka ya mauaji katika Mahakama ya Tabora.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, baada ya kupitia nyaraka mbalimbali zikiwemo kitabu cha kuzuia wahalifu (detention register), ilibainika Sadiki alikamatwa Juni 21, mwaka jana kwa tuhuma za kuvunja nyumba usiku na kuiba, na kuwekwa mahabusu saa 9 alasiri siku hiyo hiyo.

Kitabu hicho kilionyesha kuwa Juni 29, mwaka jana mlalamikaji alitolewa mahabusu na kufikishwa mahakamani kujibu shtaka la mauaji ya Jackson Thomas, yaliyotokea Juni 6, 2018, Barabara ya Kazima, Tabora Mjini; jambo ambalo lilibainika kuwa halina ukweli wowote.

Mbali ya kumbambikia kesi ya mauaji Sadiki, pia ilibainika mkazi mwingine wa mji huo, Edward Matiku, aliyekamatwa Julai 1, mwaka jana kwa kosa la kuvunja nyumba na kuiba aliunganishwa kwenye shauri hilo la mauaji namba 8/2018.

Kutokana na uchunguzi huo, DPP Mganga aliwafutia mashtaka yote na kuachiwa huru na Mahakama Machi 8, mwaka huu.

Kuhusu Mwendesha Mashtaka wa Polisi aliyepeleka shauri hilo mahakamani, wakati akijua ni la kutunga, DPP Mganga alisema tayari amekwishamfuta kwenye orodha ya maofisa wa polisi waliokasimiwa kuendesha mashauri ya jinai kwa niaba ya ofisi yake.

DPP Mganga alitoa rai kwa mawakili wote wa Serikali wanaofanya kazi katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Waendesha Mashtaka wote nchini waliokasimiwa mamlaka ya kuendesha mashauri ya jinai na vyombo vya upelelezi, kufanya kazi kwa mujibu wa sheria bila kumwonea mtu na kuzingatia masilahi ya taifa.

Kumekuwapo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi walio katika mahabusu za vituo vya polisi na magerezani ya kubambikiwa kesi za mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Kumekuwapo mwito wa wananchi kwa serikali kuunda chombo mahususi kwa ajili ya kupokea malalamiko ya watuhumiwa wanaodai kubambikiwa kesi.

835 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!