HALI ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu inaendelea kuimarika huku akiendelea na mazoezi ya viungo katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako anapatiwa matibabu ya majeraha aliyoyapata baada ya kushambuliwa kwa risasi nyumbani kwake Area D, mjini Dodoma mnamo Septemba 7, 2017.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Kituo cha Runinga cha Azam TV, Lissu ameeleza namna alivyoshambuliwa huku akisema kuwa watu waliotekeleza tukio hilo la kinyama dhidi yake aliwaona japo hawajui.

“Watu walionishambulia kwa risasi niliwaona lakini siwafahamu, nilikuwa ninajitambua mpaka muda nafikishwa Hospitali ya Dodoma, na mtu wa kwanza kumpigia simu alikuwa ni Mwenyekiti wangu wa Chadema, Freeman Mbowe. Dereva wangu ndiye alinisaidia kuwasiliana naye pamoja na watu wengine kuwapa taarifa hizo,” alisema Lissu.

Aidha Lissu amewashukuru madaktari wa Dodoma na  Hospitali ya Nairobi kwa kufanya jitihada zao kuokosa maisha yake.

“Nisingefika Nairobi bila msaada wa kwanza wa madaktari wa Dodoma.  Nilipofika Nairobi Hospital madaktari walifanya kazi kubwa sana kunitibu na kuokoa maisha yangu hadi kufikia hapa nilipo leo. Madaktari wametoa risasi kumi na sita mwilini mwangu tangu nimefika hapa Hospitali ya Nairobi, risasi moja bado ipo mwilini na risasi zingine kumi na sita zilinikosa siku hiyo ya tukio,” alifafanua Lissu.

Akizungumzia pesa za matibabu kutoka Bungeni, Lissu amesema:  “Mpaka sasa tunapoongea, Bunge halijatoa hata senti moja kwa ajili ya matibabu yangu, hili jambo si la mimi au familia yangu kuliomba Bunge kunilipia matibabu.  Hii ni kwa mujibu wa sheria. Isitoshe,  hakuna Ofisa wa Bunge yeyote aliyekuja kuniona hospitali tangu Septemba 7, 2017 niliposhambuliwa, si Spika, Naibu Spika wala Katibu wa Bunge.”

Kuhusu uimara wa Chadema kufuatia hamahama ya wanachama wake alisema Chadema haiwezi kufa akiwataja watu wengi walioondoka wakiwemo Kafulila na Masha.  Alisisitiza chama hicho kiko imara na kitaendelea kuwa imara.  Aliwahakikishia Watanzania kwamba hawatatarudi nyuma, akisema pindi akipona ataendelea na harakati zake za ubunge, kazi ambayo anaipenda kutoka moyoni.

2472 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!