‘Turejeshe Ujamaa, ubepari tumeshindwa’

Mkutano wa Nane wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma, umekuwa na michango mingi na yenye mvuto kutoka kwa wabunge mbalimbali. Ifuatayo ni sehemu ya michango hiyo.

 
IBRAHIM MOHAMED SANYA (Mji Mkongwe-CUF)

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tujaribu kuangalia hili Shirikisho la Afrika Mashariki litatusaidiaje kiuchumi, tuende na hili jambo dogo tu. Tanzania ni nchi pekee katika Afrika Mashariki inayopakana na nchi zote za Afrika Mashariki. Tanzania inapakana na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi lakini tumetumiaje mipaka hii kusafirisha bidhaa zetu,  tumechangamshaje masoko yaliyo karibu na mipaka kuwaruhusu wa jirani kuingia nchini mwetu na kununua bidhaa.

Tanzania ni nchi kubwa. Ukishindanisha hizi nchi, Tanzania ukiichukulia kwa kilomita za mraba watu wa Tanzania 47 kwa kila kilomita moja za mraba, wakati Kenya ni watu 70, Uganda 139, Burundi 301, Rwanda 403. Hatuoni tuna kila sababu ya kuitumia ardhi yetu tukavuna uchumi wa nchi jirani, tukainua maslahi ya watu wanaoishi vijijini na mipakani, hatulioni hilo? Tukainua uchumi kwa njia ya bidhaa, kwa njia ya kilimo, kwa njia ya utalii, tukashirikiana na hizi nchi za Afrika Mashariki?

Hii gesi ambayo tunasema tunataka kuzalisha, hii hii tunaweza tukafua umeme na tukaziuzia nchi zote ambazo zimepakana na sisi, lakini ni nani anafikiria mambo hayo? Kila mmoja anafikiria kuingia mikataba na watu wanaochimba madini, watu wanaokuja na mikataba mibovu ili apate, ukishakupata itakusaidia mali mbovu!

Wale wote walioibadhirifu nchi hii kwa njia ambazo si halali, walahi zitawatokea puani pesa zile, kwa sababu “majority” ya watu ni masikini, watu wanazaliwa hawawezi kununua dawa, hawana hospitali za kisasa, hawana nguo bora, hawana chochote kinachowasaidia. Sisi leo tumebaki tunadai mishahara minono kwa viongozi wa Serikali pamoja na sisi kwa nini tufiche, kwanini tusiwatetee wale walio wengi, waliotuchagua wakatuleta hapa?

Kuna pamba hii hapa. Utakapomwambia mtu yeyote kwamba pamba inazalishwa Tanzania, lakini Tanzania hawaproduce vitambaa ni jambo la ajabu. Mauritius hawana pamba wanasafirisha nguo kupeleka Italia, kupeleka Ureno, kupeleka Uhispania na kupeleka nchi nyingine za Ulaya. Na hutasikia wala hujasikia watu wa Sychelles, Mauritius, kufanya maandamano ya kupinga Serikali kwa jambo lolote kwa sababu wana uchumi imara.

Leo viwanda vipo nchini, hatuwasaidii wenye viwanda tuka-subside wakazalisha pamba wakatengeneza nyuzi, wakatengeneza majora ya vitambaa, wakatengeneza vitambaa vikatumika nchini, matokeo yake zinaingizwa nguo kutoka Pakstan, Bangladesh, China, India kwa mlango wa nyuma bila ya kulipiwa ushuru halali – wakaua viwanda vya ndani kwa nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, piga marufuku mara moja bandarini pale, TRA itafute wataalamu watakaoweka database ya kuona namna gani nguo zinazalishwa nje na bei gani, na zinaletwa vipi ndani na zinalipiwa ushuru kiasi gani ili tulinde viwanda vya ndani. Ukiinyanyua pamba utai-save pamba, umem-save mkulima, ume-save mtu aliyeajiriwa kwenye kiwanda, umei-save nchi inapoagizia kutumia pesa za kigeni nchi za nje. Polisi wetu wanavaa nguo kutoka nje, wanajeshi wetu wanavaa nguo kutoka nje, JKT wanavaa nguo kutoka nje ya nchi, pamba tunayo ndani si aibu!

We eat what we don’t produce and we produce what we don’t eat. kwa nini tusiwe na viwanda vya kisasa vikazalisha nguo tukawapa polisi wetu tuka-save pesa ya kigeni, kwenye bajeti tukapunguza matumizi. Kwa nini tusitengeneze nguo za kijeshi, za polisi, za JKT, mablanketi ya hospitali, nguo za wanafunzi wetu? Ninachotaka kusema hata Tanzania mwaka huu mzima imesafirisha bidhaa za dola milioni 400 Kenya, lakini Kenya na udogo wake wametuuzia dola milioni 393, tofauti iliyopo ni dola milioni 21, wakikazana kidogo tu wale Wakenya kule watatushinda kiuchumi na watasafirisha bidhaa zao nyingi zaidi. Turejeshe siasa ya Ujamaa katika nchi ya Tanzania, ndiyo solution yetu, ubepari umetushinda na hii kazi tunayokwenda nayo tutawakandamiza kiuchumi wananchi walio wengi.
 
‘Wananchi wa Tanzania wamekata tamaa’

JOELSON MPINA: (Kisesa-CCM)
 
Naomba kusema la kwanza kabisa siungi mkono bajeti hii iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, kwa sababu kuu zifuatazo:

La kwanza, mapato yetu ya ndani kufikia mwezi wa tatu yalikuwa asilimia 98, mapato yanayotokana na mikopo na misaada yalifikia asilimia 62 kwa mwaka. Lakini matumizi yetu yalifikia asilimia 87 kwa kipindi hicho, lakini fedha zinakoenda asilimia ziko chini, Halmashauri zilikuwa chini ya asilimia 30 kwenye mashirika ya umma na taasisi zilikuwa chini. Sasa haya matumizi yanayozungumzwa ya asilimia 87 hayawiani na matumizi yalivyo katika fedha zinakopolekwa. Kwa hiyo Serikali kama Serikali ilitakiwa kuondoa utata huu.

Kwa kuleta maelezo ya ya kutosha kwenye Bunge ili lithibishe kwamba fedha zilizokuwa zimetengwa kwa matumizi ya mwaka jana, zimeenda kwenye maeneo gani kama hazikuenda katika maeneo ambayo tulikubaliana kwenye bajeti ziko wapi na kwa idhini ya nani?

La pili, kwanini sikubaliani na bajeti hii, hoja za Mdhibiti na Mkaguzi na Mkuu wa Hesabu za Serikali mpaka tunaingia za mwaka 2009/2010 mpaka tunaingia kujadili bajeti hivi leo Bunge lako halijaona majibu ya Serikali dhidi ya hoja hizo za ukaguzi za mwaka 2009/2010 ni kinyume cha sheria ya nchi ambayo tuliipitisha the public audit ya act ya 2008 kifungu cha 40 ambapo nasema kifungu cha 40(1) the Accounting Officers shall respond to the Controller and Auditor General’s Annual Audit Reports and prepare action plan of the intended remedial action for submission to the Pay Master to the General.

Kifungu kinachofuata cha pili kinasema, on receipts of the responses and actions the Pay Master General shall submit to (a) Minister who shall lay it before the National Assembly in the next session. (b) Controller and Auditor General a copy of consolidated response and action plan.

Haya yote hayajafanywa na Serikali. Kwa hiyo si halali Bunge hili kuanza kujadili Bunge bajeti mpya wakati hoja zilizozungumzwa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali hazijajibiwa kwa kufuata sheria yetu ya ukaguzi ya mwaka 2008 kifungu cha 40 ukisoma 1 mpaka 3, kwa hiyo Serikali imevunja sheria ya kutolitendea haki Bunge hili ili kwamba lijiridhishe, fedha za Watanzania ambazo tumezigawa tulikozipeleka zimefanyaje kazi na kama kuna malalamiko ambayo yalionyeshwa na mkaguzi je, Serikali imeyajibu vipi, ili Bunge hili liwe na uhakika sasa hata linapoingia kwenye bajeti leo liwe na uhakika kwamba kule linakotaka kuzipeleka tena kuziidhinisha fedha za Watanzania zitaenda kufanya kazi.

Kwa kuvunja sheria namna hii Serikali ingeweza kuwa imeshapelekwa mahakamani kwa sababu ukivunja sheria na sheria hii inasema unapoivunja unatakiwa ufanye nini?

La tatu, umbile la bajeti na matarajio ya Watanzania, umbile la bajeti na matarajio ya Watanzania, bajeti hii tuliyowasilishiwa siyo sahihi kwa mujibu wa mpango wa maendeleo na kwa mujibu wa Bunge tulivyokubaliana mwaka 2011 mwezi wa sita. Umbile la bajeti tulikubaliana mambo ya msingi la kwanza katika mpango wetu wa maendeleo tutautekeleza vipi.

La kwanza tukakubaliana bajeti yetu kila mwaka wa fedha tutahakikisha tunatenga fedha zetu za ndani trilioni 2.7 kwa ajili ya miradi ya maendeleo fedha za ndani. Lakini vile vile tukasema walau asilimia 35 ya fedha zetu za bajeti ziende kwenye miradi ya maendeleo.

La tatu, fedha zinazotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo zisitumike kwa aina nyingine yoyote link fence. Sasa nasema bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha imekiuka Azimio ya Bunge kwa sababu haikuzingatia hayo yote, badala ya kutenga trilioni 2.7 kwa ajili ya shughuli za maendeleo, bajeti ya Serikali imewasilishwa ikiwa na trilioni 2.2i kwa ajili ya shughuli za maendeleo. (Makofi)

Lakini vilevile, uwiano wa 35 kwa 65 haukuzingatiwa. Asilimia iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha matumizi ya kawaida ni asilimia 70 na matumizi kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni asilimia 30 na ni kinyume cha maazimio ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, kibaya zaidi ni kwamba katika mwaka huu wa fedha mapato yetu ya ndani yameongezeka kwa trilioni 1.5. Matumizi ya Serikali yakapanda kwa trilioni 1.9 wakati miradi ya maendeleo ikipunguziwa fedha katika bajeti bilioni 397.8. Hii siyo haki na ndiyo maana nasisitiza kwamba  bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha imekinzana na Azimio la Bunge na imekinzana na yale tuliyokubaliana katika mpango wetu wa maendeleo.

Mheshimiwa Spika, ukifanya utafiti utagundua kwamba katika matumizi yetu ya kawaida Sh trilioni 3.6 ndiyo fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, lakini katika Sh trilioni 3.6 yapo matumizi ambayo hayaepukiki na mimi nakubaliana nayo; yapo Sh trilioni 2. Lakini trilioni 1.6  inaweza kabisa ukai-adust ukapata fedha ukapeleka kwenye miradi ya maendeleo. Kinachokosekana ni nia ya dhati tu, wakati Watanzania wakisubiri tuongeze utoaji kasi ya utoaji wa huduma, tuongeze uwekezaji, lakini leo hii tunakusanya mapato yasiyolingana na mahitaji ya Taifa hili.

Tumekuwa na mipango yetu ya namna hii ya siku nyingi na Serikali ilituletea mpango huu, Baraza la Mawaziri liliupitisha mpango huu, lakini leo tunaingia kuu-deny mpango huu sisi wenyewe, kama Mheshimiwa Rais amekosa watu wa kumsaidia serikalini, basi Bunge hili limsaidie  kwa kuikataa bajeti hii mpaka pale watakapokubaliana na maazimio tuliyokubaliana na Sh trilioni 2.7 kupangwa kwenye shughuli za maendeleo. Hatuwezi kuendelea na mzaha wa namna hii.

Nina kitabu cha dira ya maendeleo, soma ukurasa wa 13. Watanzania wamejijengea sifa ya kutayarisha na kujitangazia mipango, programu na malengo ambayo mara nyingi yamekuwa hayana mpangilio mzuri wa utekelezaji. Uratibu na taratibu za tathmini, matokeo yake utekelezaji umekuwa dhaifu. Hali hii imesababisha kupungua kwa imani na matumaini ya wananchi kwa viongozi wao, ni dhahiri kwamba wananchi hivi sasa hawana hamasa ya kushiriki katika mipango ya kitaifa, bali wananchi wamekata tamaa.

Hiki ni kitabu ambacho kimefanyiwa research na wataalamu wetu. Tunaleta mzaha leo wa kutekeleza mpango wa maendeleo ambao tuliukubali, mimi naomba Bunge hili limsaidie Rais wetu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Alikuwa na nia ya dhati kabisa kutuletea mpango huu, lakini leo pesa za kwenda benki tulikubaliana kwamba Benki ya Kilimo, leo tunazungumzia Sh bilioni 100 lakini Benki hiyo tuliizungumzia kuanzia mwaka jana na mwaka huu kwenye bajeti hii tunazungumza Sh bilioni 40 za kupeleka kwenye benki hiyo. TIB tulizungumza bilioni 30 badala ya Sh bilioni 70.
 
‘Wakulima wa pamba wanaweza kuamua nani awe rais’

SELEMANI NCHAMBI (Kishapu-CCM)
 
Naomba katika mambo haya yote tuwekane sawa, maji ya Ziwa Victoria tuhakikishe kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi mwaka jana ungeanza, mwaka huu mradi huu uanze. Visima virefu vichimbwe kwenye maeneo ambayo maji hayo hayatafika. Akina mama wa Kishapu wanahitaji kupendeza nywele zao kama alivyo Sara Msafiri hapa, lakini hawawezi, wanabeba maji kichwani.

Akina mama wa Kishapu wanachoka hata jioni migongo, viuno vinauma kwa kubeba maji umbali mrefu, kwa hiyo naomba sana maji ya Ziwa Victoria, Waziri wa Fedha yuko hapa, ndiyo anayemsaidia Rais kwenye mambo haya ahakikishe fedha zinatengwa na tayari tumeshakamilisha michoro. Mabwawa, marambo, (miradi) “scheme” za umwagiliaji hatuna hata asilimia moja tutazalisha vipi tutaongeza vipi kipato wakati watu hawazalishi.

Hospitali ya Wilaya: Nimeingia katika Jimbo la Kishapu hakuna hospitali ya wilaya, akinamama hawa wanapata tabu wakitaka kujifungua kwa operesheni. Vituo vya afya tunavyo vinne, havikidhi wala havitoshelezi mahitaji. Wanapotaka kujifungua wanakwenda kilomita 125 kutoka Magarata hadi Shinyanga mjini, hii siyo haki na mimi sikubaliani na hili. Kwa hiyo iangaliwe uwezekano, tumeleta maombi maalumu zaidi ya mara tatu yanarudi. Je, umuhimu wa afya za wananchi wa Kishapu haupo?

Nimeangalia bajeti nzima ya afya, sisi Kishapu tunahitaji zaidi ya Sh bilioni 6.5. Tuna zahanati 47; zinazokidhi kiwango ni 17 katika zahanati 117 za vijiji vyangu. Vituo vya afya tunahitaji 20; tunavyo vinne, lakini kimoja ndiyo walau kinaweza kikaitwa kituo cha afya. Mgawo wa dawa tunaoupata wa Jimbo la Kishapu ni Sh 348,281 tunapata mgawo wa kituo cha afya hizi dawa zingine wananchi wanapata wapi? Pamba yenyewe itauzwa Sh 460, dawa wajinunulie, gari la wagonjwa hakuna, mtandao wa mawasiliano haupatikani, …wauze ng’ombe wakodishe gari la wagonjwa kukimbia Shinyanga Mjini, mimi sikubaliani na haya naomba kwa kweli marekebisho yafanyike.

Ni aibu, Kishapu hatuna mochwari. Mtu anapofariki dunia anawekwa stoo kama mchele ama pamba, mimi sikubaliani na haya ninaomba “special request” iliyokuja ya hospitali yetu ikamilike.

Sikubaliani na akina mama kupata tabu, wazee wangu kupata tabu na wakiugua viongozi wakuu wa kiserikali wanapokuja Kishapu wasipelekwe India kama shemeji yangu Zitto (Zitto Kabwe), watibiwe pale pale kwenye zahanati zetu za Kishapu waonje machungu. Ili kuboresha uzalishaji nchi hii barabara ya lami ya kutoka Kolandoto kwenda Meatu, naomba iingie kwenye mpango na ipatiwe fedha. Tunalima sana, tuna mifugo mingi, tuna mambo mengi sana, naomba sana barabara ya lami hiyo iingie kwenye mpango – ni ahadi ya Mheshimiwa Rais.

Lakini jambo jingine katika miji yangu mitatu ya Ukenyenge, Maganzo na Muhuze, hatuna hata kipande cha lami au kwa sababu sisi ni Wasukuma, hatutakiwi kuwa na lami katika miji yetu? Tunahitaji daraja la Karitu, Manonga, tunahitaji daraja Kiloleli kwenda Idisa, tunahitaji daraja la kwenda Shinyanga Itirima, mazao kunakolimwa mpunga – Itilima tunalima  mpunga mwingi sana, lakini usafirishaji ni wa bodaboda, gunia linabebwa kwa bodaboda, naomba sana.

Tukija kwenye elimu, fedha zangu zimefanyiwa ubadhirifu, kwenye elimu mimi wanafunzi wanakaa chini, walimu nyumba hakuna, tunakwenda kwenye madarasa hazitoshelezi, fedha za MMEM zimeliwa, tunakwenda kwenye maabara zimeliwa, hosteli wanafunzi wangu hawana – watoto wa kike wanapanga kwenye nyumba vijijini, mimba zimeongezeka. Kishapu nataka nikueleze watoto wa kike baadaye kama akinamama Anne Kilango hapa hatutakuja kupata watetezi kama utaratibu ni huu, lazima fedha ije.

Walimu hawatoshi, chakula shuleni, tumeanza na shule 20 katika shule 126 na watoto hawa wanatembea kilomita nyingi, naomba sana. Ukija kwenye kilimo pamba… kama hakuna elfu (Sh 1,000 kwa kilo moja ya ya pamba) pamba wakae nayo kwanza. Watu wamehangaika, wamepigwa jua wamekwenda kwenye tope, wamevuna wamepiga dawa, dawa zimechakachuliwa wamepewa maji, lakini bado bei tunaambiwa Sh 500.

Pamba itaendelea kushuka kila mwaka. Leo Geita Mining turnover ya mwaka mmoja ni zaidi ya Sh bilioni 400 mafuta unayotumia kwa mwezi mmoja ni lita milioni moja na nusu, milioni mbili. Lakini bajeti ya afya ni Sh milioni 576. Turnover ya mgodi mmoja inasogelea bajeti ya wizara moja, mimi sikubaliani na hili. Shinyanga sisi… naomba nianze kukuhesabia neema tulizonazo: tuna pamba nyingi, tuna dhahabu nyingi, almasi nyingi, tuna mifugo mingi, tuna tumbaku nyingi, tuna idadi ya watu kubwa kabla ya kugawia Simuyi, Shinyanga ilikuwa na watu milioni 4.2.

Tuna  vyanzo vingi vya maji, tuna mpunga mwingi, lakini naomba nianze kukuhesabia matatizo ya mkoa wa Shinyanga. Kiwanja cha ndege mvua ikinyesha hakishukiki, Mheshimiwa Rais zaidi ya mara mbili anataka kushuka kiwanja kimejaa maji, hospitali ya rufaa hatuna, watu milioni 4.200 kwa neema zote hizi, chuo kikuu chochote, kwa neema zote hizi, maji ya Ziwa Victoria tunashukuru sana Serikali ya CCM imeyaleta, lakini Kishapu lazima yafike kwa neema hizi.

Bado nakwenda kwenye matatizo tu, matatizo hayo vyanzo vya maji, lakini maji ni haba, akinamama nimelieleza sana, tatizo la pamba, neema ya pamba, Shinyanga inatoa pamba asilimia 62 ya pamba ya nchi hii – mkoa mmoja.

Hatuna kiwanda chochote kiwanda chochote, leo nashangaa mashirika yetu ya Serikali ya NSSF wanajenga maghorofa ya Sh bilioni 100 Dar es Salaam yamewaajiri Watanzania 30, wanashindwa ku-invest kwenye viwanda vya nyuzi na nguo ambako wataajiri Watanzania milioni 14. Pamba inaajiri Watanzania milioni 14 wakulima wa pamba wakiamua Serikali gani ikae madarakani, inakuwa.

Lazima sasa Serikali ifanye yafuatayo, kwenye pamba isiwe ni agenda za kuongea; (i) Bodi ya pamba imeonekana imeshindwa kusimamia pamba. Pamba tumeanza kulima kabla ya Uhuru, ivunjwe iundwe bodi mpya. Uingereza kabla ya kuanzishwa bodi wajumbe wanakwenda kusomea namna ya kuendesha bodi, sisi hawasomei imekuwa kama ni takrima wewe utakuwa mkurugenzi wa bodi, haiwezekani awaburuze watu milioni 14, kikao kinakaa kwa ajili tu ya kupanga bei ya pamba, hakikai kwa ajili ya mikakati ya kuimarisha zao la pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ifute kodi zote kwenye zao la pamba, Serikali itoe dhamana kwa matajiri wawekezaji, Watanzania wanaotaka kuwekeza kwenye mazao ya pamba, itoe “guarantee” kwa viwanja hivyo. Serikali gani isiyosikia Watanzania milioni 14 wanalia sasa wamefika 16, NSSF wanajenga maghorofa yanapangisha watu 40, watu 50 badala ya kwenda ku-invest kwenye ajira ambako wataajiriwa Watanzania milioni 16 fedha za nje zitakuja madola kwa madola tutaacha hata kwenda kukopa nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, na waheshimiwa wabunge nataka niwatahadharishe na kuwaomba, kama tunawadharau Watanzania milioni 16 wanaolima pamba, tutakuja kukumbuka maneno yangu.