NA BARUA YA S.L.P.
Mzee Zuzu,
C/O Duka la Kijiji Kipatimo,
S.L.P. Private,
Maneromango.

Mtanzania Mwenzangu,
Yahoo.com/hotmail.com/excite.com/www.http,
Tanzania Yetu.

Yah:  Tusicheze danadana dakika za majeruhi itatugharimu
Ni siku nyingine ya Jumanne wanangu tunapokutana katika waraka wangu wa barua hii, kuwakumbusha yale ambayo sisi tuliobahatika kula chumvi ya kutosha, tuliyaona na kuyaasisi katika taifa hili lililokuwa la Ujamaa na Kujitegemea.

Moja ya barua zangu nilizowaandikia  niliwahi kuwatajia tuzo mbalimbali nilizowahi kukabidhiwa, kwa kazi nyingi nilizofanya kwa jamii yangu na kuitwa mtukuka. Japo nakaa katika kibanda changu cha mbavu za mbwa lakini nimebandika ukutani ili kila ajaye apate kuuona ushahidi huo na kunipa kongole kwa kazi hiyo.

Wanangu, naandika barua hii kwa mara nyingine nikiwa na hasira, tena ya uzeeni. Kama hujui hasira ya uzeeni inafananaje basi niseme kuwa inatosha kukuombea maisha marefu ili nawe ufikie uzee kama wangu na kuona jinsi vitu vidogo vinavyokukera seuze hayo makubwa yatakuwa yanakukera kiasi gani.

Uzee ni dawa lakini wakati mwingine uzee ni hasara kwa taifa na hasa kama uzee wenyewe unakuwa tegemezi kwa taifa. Nashukuru Mungu uzee wangu hadi leo najitegemea yaani sipo ‘boarding life’ bali nipo ‘day life’. Sili cha mtu nabangaiza kwa akili yangu, siitegemei serikali najitegemea mwenyewe katika mambo mengi sana kama matibabu na kadhalika.

Wanangu, niwape machungu kidogo niyapatayo kutokana na kujitegemea kwangu. Kwanza sipati matibabu ya kisasa, naishi vile Mwenyezi Mungu anavyopenda niishi.

Siku atakayogoma kuyafungua macho yangu na kuweza kuona hiyo miti shamba ambayo ndiyo tiba yangu, hapo ujue ndiyo mwisho wa maisha ya Mzee Zuzu, maana sina hiyo mnayoita bima ya maisha wala matibabu muhimu kwa wazee. Hii ndiyo nchi yenu mliyoipokea kutoka kwetu.

Nchi tuliyowakabidhi hadi tunaamua kufunga mikanda miezi 18, ilikuwa kila mtu anapata matibabu bure na tulihakikisha kila kata ina zahanati yenye mganga wa awali na mkunga kwa ajili ya uzazi salama.

Tulihakikisha vijiji vingi vina shule ya msingi yenye walimu wa kutosha na vitendea kazi muhimu kama madaftari, kalamu vitabu vya kiada na ziada, rula, chaki na kila kilichokuwa muhimu katika taaluma hiyo. Kama unabisha naomba muulize yeyote aliyesoma miaka ile kabla ya Vita ya Uganda.

Nayapenda sana maisha yale, lakini kamwe ni asali tusiyoweza kuirudia tena kwa mfumo huu wa maisha tunaokwenda nao.

Mfumo huu ni wa kila mtu kuangalia tumbo lake na familia yake, tofauti na wakati wetu tuliokuwa tunafanya mambo kwa faida ya wenzetu wote kwamba chetu ni chetu na si chao ni chao.

Niliwahi kuandika katika barua yangu fulani kuwa hakuna kitu kinachonikera kama siasa. Wengine wanaposema siasa ni mchezo mchafu sielewi wana maana gani.

Lakini ukweli uko palepale kwamba kwa umri wangu sipendi siasa kwa sababu leo naona ni kama kuchefuana akili, kwa usanii unaofanywa na hao wanaoitwa wanasiasa kuanzia mwenyekiti wetu wa mtaa, mtendaji wa kata na wengine ambao ni wakubwa wao.

Leo naandika barua hii nikiwa na hasira, kuwaona hao  wabunge wetu wakiwa wanatukumbusha machungu ya kuliwa hela za Serikali na watu wachache, ilhali sisi wazee tukiwa hatujui hatima yetu ya maisha bora tuliyoahidiwa na mkuu wa nchi  kabla ya kuingia Ikulu.

Siku nyingi zimepita tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa ulipoasisiwa na kufanya demokrasia kuwa kubwa zaidi. Lakini kwa bahati mbaya wale waliokuwa katika vyama vingine vya siasa ambavyo si kutoka chama tawala waliitwa wapinzani.

Mimi niliwahi kukataa kwamba hawa si wapinzani, kwa sababu kuwa wapinzani maana yake si wamoja na sisi, na kama wanataka jambo fulani kwa manufaa ya taifa litaonekana linatoka kwa wapinzani. Kwa hiyo haliwezi kukubalika kwa hao wa chama tawala.

Kwa akili yangu ndogo niliona hiyo ni kero namba moja kwa sababu hata likiwa jambo muhimu litapingwa, kwa hoja ileile ya kutoka kwa wapinzani. Maana wapinzani wanaonekana si wenzetu katika kuleta maendeleo na hiyo ilikuwa ikinikera sana pale hoja ya msingi inapotolewa kwa manufaa ya taifa.

Zamani kidogo mwaka 1958 tulikuwa na wapinzani kama wa leo akina Joseph Kasella Bantu, Mzee Mapunda. Miaka michache baada ya Uhuru walijitokeza wengine kama marehemu Oscar Kambona na kadhalika. Hawa walikuwa na mwono wao kisiasa hivyo wakatofautiana na kijana mwenzao Julius.

Kutokana na hilo waliwekwa ndani lakini Oscar alikimbia. Athari zake hadi leo tunaziona kwamba wao tuliwana si wenzetu katika kujenga taifa na kwamba walikuwa wapinzani.

Kwa hawa wa wakati ule, naweza kukubaliana na uamuzi wa Julius kuwaweka kizuizini kwa sababu walikuwa wanapinga Serikali ya umoja kwa maana ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Hili lilikuwa ni sahihi kabisa na ndiyo maana tulifika pale mahala tukawa tunaweza kujidai kila mmoja kwa wakati wake, kwamba hiki ni chetu na si chao – ulikuwa mfumo mzuri uliotuweka mahala tulipokuwa na heshima mbele ya mataifa mengine.

Leo tumehama kutoka katika Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Tupo katika utandawazi na siasa za vyama vingi. Kila chama kina mwono wake katika kuliletea tija taifa, lakini pia tuna mawazo tofauti kutoka katika marika tofauti pia.

Ilikuwa busara kuwasikiliza hata hao tunaowaita wapinzani ili kupata hoja zao na kuzipima kwa vitendo, tuone kama zina tija badala ya kuweka masuala ya masilahi ya chama mbele na kutuacha wananchi tukiwa hatujui hatima yetu.

Wanangu nimeandika barua hii ya leo baada ya kuona wale wa chama tawala wanaungana leo na kusema hapana katika matumizi makubwa ya Serikali. Nakumbuka kuna wakati katika vikao vya bunge wenye chama tawala waliwahi kukataa hoja ya matumizi makubwa ya Serikali.

Japokuwa jambo hili linafurahisha, lakini linanipa tabu kutokana na muda wabunge hawa chama tawala walipoamua kuchukua uamuzi wa kukubaliana na wale wanaoitwa wa upinzani. Huu ndiyo ule usemi wa kwamba ‘siasa ni mchezo mchafu’ na madhara yake.

Nachelea lakini naomba mniwie radhi wanangu, kwamba hizi danadana zinaweza zikawa nzuri sana katika dakika za mwisho wa mchezo wa siasa, lakini pia zinaweza zikatugharimu Watanzania kwa sababu hujui aliye na mpira atacheza vipi! Anaweza akautoa nje au akanyang’anywa.

Hapo ndipo utakapokuwa umewadia muda mwingine wa uchaguzi, tutakapogundua kuwa wachezaji wetu ndiyo walewale wa msimu uliopita. Itabidi tusubiri dakika nyingine 90 za kusubiri matokeo. Hapo ndipo mashabiki tutakapobaki na masikitiko kwa timu yetu kushindwa siku zote.

Mimi ningeunga mkono ushirikiano wa wachezaji katika siasa, kwani naamini kuna siku tunaweza tukapata kikosi bora kitakachotupa ushindi na hapo akina Mzee Zuzu wataacha kutumia miti shamba, kuagua, kuishi kwa bahati, kupata mafao yao, kupata huduma bora za kijamii na kadhalika.

Wasalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo

By Jamhuri