Tusikubali kuibiwa tena

Kwa miezi miwili sasa tumekuwa tukishuhudia taarifa zenye kupasua mioyo ya Watanzania wanaoishi kwa mlo mmoja na kuishi katika umaskini wa kutupwa. Watanzania wamesikia taarifa za nchi hii kuibiwa wastani wa Sh trilioni 108 kupitia makinikia yaliyosafirishwa nje ya nchi tangu mwaka 1998 hadi mwaka 2017.

Shukrani kwa Rais John Pombe Magufuli aliyezuia usafirishaji wa mchanga nje ya nchi na kuunda Kamati mbili zilizobainisha hayo. Watanzania tumepata kufahamu utajiri wa nchi yetu, wanavyotutenda wawekezaji si tu katika sekta ya uziduaji, bali hata katika nyanja nyingine.

Wakati mjadala wa makinikia ukiendelea, wiki iliyopita Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ametupa mshtuko mwingine mkubwa baada ya kulieleza taifa makubaliano kati ya Serikali na Kampuni ya Huduma za Makontena ya Kimataifa (TICTS).

TICTS imekubali kubadili masharti katika mkataba kati yake na Serikali na kujiongezea wajibu wa kulipa kodi kutoka dola milioni 7 (Sh bilioni 15.4) kufikia dola milioni 14 (Sh bilioni 30.8) kwa mwaka. Prof. Mbarawa amesema ni kwa mara ya kwanza ameshuhudia mpangaji anakubali kodi iongezeke asilimia 100.

Si hilo tu, kodi hiyo itaendelea kuongezeka kwa asilimia mwaka hadi mwaka kadri mizigo na huduma za makontena zinavyoongezeka. Tunafahamu upo mgogoro kati ya Serikali na Kampuni ya Acacia ambayo makontena yake zaidi ya 277 yamezuiwa kusafirishwa nje ya nchi.

Tumeushuhudia mchakato uliofanywa na Serikali kutunga sheria zinazodhibiti taratibu za kutoa leseni, uchimbaji, uhifadhi, usafirishaji, faida kwa uchumi, umiliki na biashara ya madini nchini. Serikali inastahili pongezi kwani hatua ilizochukua kupitia sheria hizi, hata kama wawekezaji hawatazipenda, ni za kimapinduzi.

Bila kutaahari, tunaisihi Serikali kuwa kwa mustakabali wa utulivu wa uchumi wa taifa letu, isisite kutuma wawakilishi katika majadiliano au kesi itakayokuwa imefunguliwa na wawekezaji hawa. Tayari tumesikia kuwa Acacia wamefungua kesi nchini Marekani.

Maafisa wetu Serikali itakaowatuma waende na hoja thabiti, zitakaloliwezesha taifa letu kueleza msingi wa hatua hizi tulizozichukua kuwa ni ustawi wa nchi yetu na wenye nia ya kuwaondoa watu wetu katika umaskini uliotopea. Tusikubali kuwa wanyonge, ilhali sisi ndiyo wamiliki wa madini. Mungu ibariki Tanzania.