Tusipotoshe kauli tukaiharibu nchi (2)

Sehemu iliyopita, mwandishi wa makala hii alinukuu maneno kutoka kwenye kitabu kilichoandikwa na Mohammed Said, yaliyohusu hofu aliyokuwa nayo mmoja wa wana TANU, Sheikh Takadir, juu ya TANU kumezwa na Ukristo. Endelea…

Hapo waweza kuona mbegu ya uhasama wa kidini ilipokuwa inaibuliwa.

Lakini mwandishi Mohammed Said katika uk. 246 anaendelea kutuandikia hivi; “… It was at the TANU old office as we were waiting for a meeting of the National Executive. All of a sudden Sheikh Takadir stood up holding his walking stick pointing it out to Nyerere as he spoke: ‘This man will never come to favour us, he would come to favour his brethren. A stitch in time save nine” Sheikh Takadir repeated these words twice. All of us in that meeting room were flabbergasted as to the meaning of those words. I saw Nyerere crying…” (Mohamed Said uk. 246).

Nini kilichomliza Mwalimu siku ile? Ni kule kuona Sheikh Mzee wake aliyekimtumaini na kumwamini sana anatamka suala la udini – “he will favour his brethren” maana yake awatapendelea wenzake!

Kuanzia siku ile Mwalimu aliamua kuzuia wananchi wa Tanganyika wasianze kufikiria tofauti za UDINI katika chama cha TANU.

Kwa hofu na taharuki aliyoipata Mwalimu siku ile kama Rais wa TANU, ndipo alianza kuchukua hatua thabiti za kuzuia SUMU ya UDINI isiingie katika chama cha TANU. Sumu namna hii ingeweza kuwagawa wanachama wa TANU na hata kuwagawa Watanganyika wote kwa ujumla wao katika makundi hatarishi.

Kungeweza, hapo baadaye, kutokea kundi la Watanganyika wafuasi wa dini tofauti na pili kungeweza kutokea kundi la Watanganyika wasomi na wasio wasomi. Wasomi wangekuwa wale aliowaita Sheikh Takadir “mission -educated Christians” – his brethren na wasio wasomi ndio hao aliowaita “will never come to favour us”– waislamu.

Basi, ili kuondoa kabisa dhana ya UDINI katika chama na serikali, Mwalimu alipoingia tu madarakani kama Rais, Desemba 1962 alitoa msimamo thabiti juu ya ubaguzi wa aina yoyote katika nchi yetu.

Mwaka 1962 alipochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, miongoni mwa vitu alivyovivalia njuga ni suala la UBAGUZI uwe wa DINI au wa KABILA au RANGI.

Nirejee kwenye ile hotuba yake aliyoitoa bungeni Desemba 10, 1962 alitamka haya, “…There is no quick way to cancel out the present difference between our Africans and non-African citizens; there is no easy way to remove the existing disparity in education between Christians and Muslims…”(Uhuru na Umoja uk. 181). Basi, alikuwa anadhamiria kuondoa ubaguzi wa aina yoyote katika Taifa jipya la Tanganyika.

Dhamira ya Mwalimu ilikuwa kujenga umoja wa wananchi wote wa Taifa huru la Tanganyika. Ilipofika mwaka 1970, tunajua Mwalimu na serikali yake walitaifisha shule zote za msingi, sekondari pamoja na vyuo vya ualimu na kuwa za serikali.

Jambo hili liliwachoma sana viongozi hasa wale wa Wakristo, lakini ilikuwa ni njia pekee kuwapatia watoto wote wa nchi hii elimu sawa. Inajulikana wazi enzi zile ndugu zetu wasiokuwa Wakristo hawakubahatika kuwa na shule zao nyingi hapa nchini, hivyo wasomi wengi walitokana na shule za misheni.

Si hivyo tu, bali kutokana na lile tamko la Sheikh Takadir lililomliza Mwalimu pale kwenye ofisi ya TANU, Mwalimu alitaka kuwaonyesha kuwa yeye na chama tawala walidhamiria kujenga Taifa moja la wananchi huru na sawa.

Lakini tunaojua mambo ya elimu enzi za ukoloni tuliona shule nyingi za misheni zilitapakaa Uchagani, Uhayani na Unyakyusa kumbe ukanda wa Pwani au huko Ugogoni na Umasaini wakoloni hawakuwa na habari nako. Ndiyo kusema kungezuka malalamiko makubwa katika nchi kuwa kuna UKABILA na UDINI.

Basi, ile taifisha ya shule iliwezesha watoto wa nchi hii kusoma shule yoyote na katika mkoa wowote ule na hivyo kufutilia mbali mawazo ya ukabila na ya udini.

Hii ikafanya Mwalimu akazie kusema “NCHI YETU HAINA DINI”, lakini wananchi wake wana dini hata ikiwa ni kuabudia chini ya mti wa msoro au katika mapango, dini ambazo kistaarabu tunaita dini za asili.

Basi, maelezo haya ni kuonyesha tu kuwa KATAZO la serikali ni KUCHANGANYA DINI NA SIASA. Ni hatari, vitu viwili hivi havichanganyiki jamani ni kama maji na mafuta.

Sijawahi kusikia katazo la uhusiano kati ya DINI na SIASA kuhusiana ni jambo la heri sana na kuchanganyika ni kitu tofauti kabisa kabisa. Naomba Padri Titus Amigo afunguke (efeta) atofautishe maneno UHUSIANO NA MCHANGANYO.

Kuna utani kule kusini kati ya makabila ya pwani na Wangoni. Utani wenyewe hasa unatokana na watu wa pwani kuita Wangoni “MAKWANGWALA” na Wangoni wanawaona watu wa pwani kama watu wasioeleweka kilugha. Mathalani, Wamakonde. Wamakonde hawana herufi “S” wala “Th” katika msamiati wa lugha yao. Ndiyo maana utawasikia ile nchi jirani ng’ambo ya Mto Ruvuma sisi tunaita ‘MSUMBIJI’ basi wao wanatamka ‘NCHUMBIJI’. Wakati mtu anaitwa ‘ATHUMANI’ wao watamwita ‘ACHUMANI’. Hata ile silaha yao maarufu wanayotumia kwenye ulinzi sisi tunaita ‘MSHALE’ eti wao wanaita ‘NCHALE’  wenye ‘CHUMU’.

Kwa mantiki ya kukosekana herufi katika maneno yao, naamini basi mwandishi wa habari ile ni wa asili ya Wamakonde na hivyo hana utamaduni wa utofautisho wa maneno ndiyo maana nahisi alidhamiria neno mchanganyo akaangukia kuandika neno uhusiano. Lakini huenda yeye ana maana tofauti na nielewavyo mimi, basi asaidie kutoa ufafanuzi wa ile makala yake.

Katika nchi yetu tumetahadhalishwa kuchanganya DINI na SIASA – hilo viongozi wote wa dini na wa siasa wanalijua. Hakuna sababu ya kuwa na woga wowote katika kuhubiri NENO la Mungu. Mwalimu alitokwa machozi pale alipoona kama kiongozi mkuu wa dini tena mwasisi wa chama cha TANU anaongelea udini katika siasa. Udini una sumu kali ya kuwagawa wananchi. Kwa kuelewa hilo, basi kila jitihada zinafanywa kujenga uhusiano mwema kati ya dini za hapa Tanzania.

Ninaamini mwandishi wa habari ile ataweza kutafuta kile kijitabu cha NYUFA angalau ajiridhishe na kauli ile ya kuwa NCHI YETU HAINA DINI bali sisi wananchi tuna dini zetu na tuna uhusiano mzuri kabisa miongoni mwetu. Kule Tunduru, asilimi 95 ya wakazi wake ni wafuasi wa dini ya Kiislamu; asilimia 5 iliyobaki ni wafuasi wa Ukristo au dini asilia. Lakini amini usiamini, tunaishi kwa amani kabisa. Utashangaa kusikia kuwa Mwadhama Baba Kardinali Pengo alipokuwa Askofu kule Tunduru, alikuwa na ‘MJOMBA’ Mwislamu kutoka maeneo ya Mkwanda pale. Hata fundi aliyemjengea Groto la Bikira Maria pale Uaskofuni alikuwa Mwislamu! Kuna uhusiano gani mzuri kuliko huo? Nadhani mwandishi hajui tofauti kati ya maneno, akatumia neno lisilofaa hapa.

Naomba tusipotoshe kauli na hasa tujaribu kutumia maneno ya kujenga uhusiano miongoni mwetu badala ya kuandika maneno ya kutatanisha kama vile “NI UONGO KUSEMA DINI ISIHUSIANE NA SIASA”. Baba Titus Amigo, je, ulimsikia nani akitamka kauli kama hiyo hapo nchini?

ADIOS

MUNGU IBARIKI TANZANIA.