Wiki iliyopita, makala hii ilianza kuchambua kwa kina baadhi ya mambo yanayotokea katika Tanzania na kuwataka Watanzania kusoma alama za nyakati. Leo, mwandishi anaendelea kuchambua kinachotokea na mwelekeo wa taifa la Tanzania. Endelea…
Mungu hawawezi kuja mwenyewe kufanya unabii, la hasha, bali anawatumia wanadamu tena wadhaifu hasa viongozi wa dini.  Tumeshuhudia baadhi ya viongozi wa dini waliojitoa mhanga kuufanya unabii kipindi cha sikukuu ya Noeli, Desemba, 2017, lakini kinyume chake walionekana ni wakorofi, wamekosa, ni wasaliti wa nchi yetu, wamekosa uzalendo, wamepotoka mbele ya jamii.
Je, ni kweli? Tujiulize kwa nini Watanzania na hasa watawala wanaogopa ujumbe wa Mungu mithili ya Mfamle Herode? Tutambue kwamba Mungu hawezi kudhibitiwa na mtu yeyote hata kama ana mamlaka yote ya dunia hii.
Waswahili husema, “Wacha Mungu aitwe Mungu.” Je, ni nani awezaye kumpinga Mungu? Nani ajuaye njia na mipango ya Mungu?  Zaburi 113 msitari wa 4-6 unasema; “Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote, nani aliye mfano wa bwana, Mungu wetu aketiye juu?”
Basi kitu kimoja tu kinatakiwa kwa mwanadamu yaani kuwa wanyenyekevu mbele ya mwenyezi Mungu. Tusome alama za nyakati. Je, nyakati hizi kwa taifa letu ni zipi, na Mungu anasema nini juu yetu? Je, ni nani awezaye kuizimisha sauti ya Mungu?
Tujikumbushe tena kwamba; “Yesu alipoingia mjini Jerusalemu kwenda kuteswa na hatimaye kutimiza ukombozi wetu, Wakuu wa Mayahudi walitaka kuwanyamazisha mitume na wafuasi wake wasimshangilie na kupiga makelele, lakini Yesu aliwajibu kuwa “hawa mkiwanyamazisha mawe yatapiga kelele.”
Kwa hivi katika jamii sauti ya Mungu, lazima isikike tutake tusitake, ukiwamo wajibu wa kukemea maovu mbalimbali bila kuogopa kama isemavyo zaburi ya 23 kwamba “Bwana ndiye mchungaji wangu sitapungukiwa na kitu.”
Manabii walitambua kwamba; “Bwana yupo upande wangu sitaogopa, mwanadamu atanitenda nini, kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa,” (Zaburi 118:6-7).
Ili kutekeleza wajibu wetu ipasavyo ni vema viongozi wa dini wakatafakari zaburi 118 yote kwani inaelezea umuhimu wa kumtegemea Mungu mshindi badala ya mwanadamu anayeshindwa katika mipango yake ya kibinadamu. Hii ni moja ya alama ya nyakati tosha kwetu.
Tukisoma alama za nyakati tunaona kwamba katika taifa letu sauti ya Mungu imeanza kunyamazishwa kwa sababu kuna watu inawaudhi. Je, hii itawezekana?
Nabaki kuamini kwamba “ukimya wa viongozi wa dini yatakuwa ndiyo mauti ya wananchi wa Tanzania.” Sauti ya Mungu lazima isikike nyakati zote na ndiyo usalama, amani, furaha, upendo, umoja, mshikamano na mstakabhali wetu unaomtegmea mwenyezi Mungu toka enzi ya Baba wa taifa ambaye sasa ni Mtumishi wa Mungu.
Je, jambo hili linasema nini kwa Watanzania na viongozi wetu? Kama tunafikiri Mwalimu JK Nyerere alipotoka kumtegemea Mungu katika uongozi wake basi huko mbele tutakwenda kukwama kama taifa na tutapoteza mwelekeo ama dira yetu.
Ndiyo maana nabii alikuwa ametumwa kutoa mwongozo kwa taifa la Israeli. Sauti ya Mungu inaonya, inakemea, inatahadharisha, inajenga na kuiunda jamii katika maisha ya upendo, heshima na utu kwa kila mmoja.
Tukiendelea kusoma alama za nyakati kwa maovu na migogoro inayojitokeza nchini mwetu kwa tabaka mbalimbali katika nyakati hizi, najiuliza kuwa je, hiyo siyo alama wazi ya uhitaji wa Katiba Mpya? Itaendelea wiki ijayo.
1795 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!