Tuweke vipaumbele 2017

Leo zimesalia siku nne kuhitimisha mwaka 2016. Kwa wazazi wengi wiki hii na ijayo si wiki za furaha sana. Wakati watoto wanafurahi kuongeza umri wa kuishi duniani, wazazi wengi wanajiuliza ada za shule inakuwaje. Mwezi Desemba, 2016 umekuwa tofauti na miaka mingine. Watu wachache waliosafiri kwenda nyumbani kusherehekea siku kuu.

Kila uliyekutana naye katika kipindi hiki amekuwa akitoa kilio cha ukosefu wa fedha. Ukosefu huu wa fedha umetokana na Serikali ya Awamu ya Tano kubadili ghafla mfumo wa maisha uliozoeleka kwa miaka 10. Maisha ya ‘dili’ yamefutika katika ramani ya Tanzania. Rais John Pombe Magufuli mara kadhaa amesisitiza kuwa asiyefanya kazi na asile.

Maneno haya si utani tena, kwani yanashuhudiwa bayana. Watu waliozoea uchuuzi, udalali na ulanguzi, maisha yao ni hoi bin taabani. Kwa watu walio na biashara halali waliokuwa na ugumu wa kupata soko, kwa sasa wanamshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na ujio wa Rais Magufuli. Bidhaa nyingi ‘feki’ katika soko zimedhibitiwa, hivyo wenye bidhaa halali wanapata fedha ya uhakika.

Kuna baadhi ya wamiliki wa shule hawajasoma alama za nyakati. Wakati maisha yakizidi kuwa magumu, shule hizi zimengeza ada kutoka wastani wa Sh 2,300,000 kwenda Sh 3,000,000 kwa mwanafunzi. Hapana shaka wanafanya hivyo kufidia pengo la upotevu wa mapato wanalolishuhudia, ambalo hawakulizoea.

Ni bahati mbaya tu kuwa kwa kuongeza karo, wazazi wengi sasa wanahamisha watoto wao kutoka shule zilizoongeza ada bila kusoma alama za nyakati na kuwapeleka katika shule zenye ada ndogo. Si zenye ada ndogo tu, wengine wanawapeleka kwenye shule za serikali, ambazo kipindi cha nyuma zilidharauliwa na kuitwa St. Kayumba. Ubora wa shule za umma umeimarika na pato limewapiga chenga wazazi inabidi watoto wao wote wasomee katika shule hizi za kitaifa.

Kinachotokea sasa kinapaswa kuwamsha Watanzania. Kama mtu alikuwa anafanya kazi kwa saa 8, sasa ajiongeze na kufanya kazi kwa saa kati ya 12 na 16. Kwa nchi za Ulaya watu wanalala saa 4 -6 kwa siku na hiyo ndiyo ratiba yao milele. Watu wanafanya kazi bila kuzibagua. Yeyote anayefanya biashara huu ndiyo wakati wa kubembeleza wateja na kuwekeza.

Kwa mwaka 2016 Watanzania walio wengi wamelalamikia ukosefu wa fedha mkononi. Sisi tunachokiona hali hii haitarejea kama ya miaka mitano iliyopita. Wenye viwanja waliokuwa wanauza bei za kujikadiria, sasa watauza kwa bei halisi. Hii ni fursa kwa kila Mtanzania kukaa na familia wakapanga jinsi ya kupata fedha na jinsi ya kuzitumia zikipatikana. Bila kubadili mikakati 2017 maisha yatakuwa magumu kuliko jiwe. Tujiandae na tubadili mbinu. Mazoea hayana naasi tena Tanzania. Tunawatakia heri ya mwaka mpya 2017. Mungu ibariki Tanzania.

1595 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons