Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, anasema: “Dunia ni makazi yetu ya pamoja.” Mwalimu na gwiji wa theolojia wa Kanisa Katoliki, Yohane Krisostom, naye anasema: “Dunia imeumbwa na Mungu ili kumtunza mwanadamu.”

Jamii yoyote ile inayopuuza mustakabali mwema wa mazingira na uumbaji wake, ni jamii isiyojijali na isiyojali hatima ya vizazi vyake. Uharibifu wa mazingira ni aina mpya ya vita ambayo maskini na tajiri wanashirikiana.

Binadamu anabaki kuwa kiumbe wa pekee katika uumbaji, lakini atathibitisha upekee katika uumbaji kama anaishi kwa kuyatunza, kuyalinda na kuyapenda mazingira anayoishi na asiyoyaishi. Tuamshe tabia ya kuyapenda mazingira yetu.

Naomba tufundishane somo la ustaarabu. Kuna mtoto mmoja alifungua chumba cha wazazi wake bila kubisha hodi. Baba hakupendezwa na kitendo kilichofanywa na mtoto wake.

Akamwita, akamwambia hivi: “Kila unapotaka kufungua mlango wowote ule lazima ugonge mlango kwa kusema, hodi!” Ni jambo bora na lenye hekima tufundishane, tuonyane, tupongezane katika suala zima la utunzaji bora wa mazingira yetu.

Lengo letu ni kuyapendezesha mazingira yetu, kwa msingi huo, unapokunywa maji mgahawani au mahali pengine popote pale usitupe chupa ovyo, itafutie mahala pake. Unapokwangua vocha yako na kuitumia, usitupe karatasi ovyo, itafutie mahala pake.

Unaponunua hindi la kuchoma ama lililochemshwa, usile ukiwa njiani, subiri ufike nyumbani ama hotelini. Usijisitiri haja kubwa ama haja ndogo mahali ambapo hapajatengwa kwa ajili ya huduma hiyo.

Kwa wale tulio na utamaduni wa kujisitiri vichakani, mitoni, kwenye majumba yaliyotelekezwa, nawasihi tuache utamaduni huo. Rafiki msomaji, unatakiwa kuwa nadhifu katika mazingira yako, binafsi naamini kwamba, kama unajipenda ni lazima uyapende mazingira unayoishi, unatakiwa kuyapenda mazingira yako.

Wafundishe wanafamilia wako, marafiki zako, wafanyakazi wenzako, wanafunzi wako, waamini wako umuhimu na faida za kutunza mazingira.

Papa Francis anatukumbusha kwa ujumbe huu: “Tumeupokea ulimwengu huu ukiwa ni urithi kutoka kwa kizazi kilichopita, lakini pia ni kama mkopo wa kizazi kijacho, ambao tunapaswa kuukabidhi kwao ukiwa salama.”

Hatupaswi kukubali kuitafuta dunia nyingine ya kuishi, lakini tunalo jukumu la kuiweka dunia hii tunayoishi katika hali ya ulinzi na salama. Tuipende dunia tunayoishi, tuyapende mazingira yetu.

Kutunza mazingira ni suala la kimaadili, bahati mbaya inayotukumba binadamu wa leo ni kwamba, hatuna maadili ya kutunza mazingira tunayoishi. Sura ya dunia imebadilika kwa sababu ya uharibifu wa mazingira.

Mwandishi wa Marekani, Sallie Mcfague, ameandika hivi: “Kutokutunza mazingira ni kuangamiza maisha yetu.” Ukiyaangamiza mazingira nayo yatakuangamiza. Ukiyakomoa mazingira nayo yatakukomoa, ukiyatunza mazingira nayo yatakutunza.

Mazingira yetu yanahitaji kutunzwa, kulindwa na kupendwa, dunia yetu inaelekea kuwa jangwa. Tutaishi wapi kama dunia yetu itageuka jangwa? Tutalima wapi kama dunia yetu itageuka jangwa?

Leo tunashuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira katika mataifa yote, ni vema kila taifa likatafuta jawabu.

Ni bahati mbaya kwamba uelewa wa sayansi unavyozidi kuwa mpana, ndivyo sayansi inavyozidi – uharibifu unazidi. Mwandishi Kornrad Lorenz alimnukuu Papa Paul II akisema: “Mwanadamu yu karibu kujiangamiza mwenyewe.” Jamii yetu kwa kujua au kutokujua imeshindwa kutunza mazingira kwa kisingizio cha sayansi na teknolojia.

Francisco wa Asizi, ni Mtakatifu anayeheshimika sana ndani ya Kanisa Katoliki. Mtawa huyu enzi za uhai wake alikuwa rafiki wa mazingira. Francisco wa Asizi alitunga utenzi wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya mazingira.

Utenzi huo aliupa jina la ‘Kaka na dada mazingira’. Francisco aliyatazama mazingira kama dada yake na kaka yake, aliyapenda mazingira aliyoishi. Aliyatazama maajabu ya Mungu kupitia mazingira aliyoishi. Tunalo jukumu la kuyatazama mazingira kama ndugu yetu.

By Jamhuri