NA MICHAEL SARUNGI
Nchi yetu ilipopata uhuru kutoka kwa wakoloni mwaka 1961 wananchi walipata madaraka ya
kisiasa, hata hivyo sehemu kubwa ya uchumi bado ilibaki mikononi mwa wageni na baadhi ya
Watanzania.
Hali hiyo ilileta kero na ikawa mojawapo ya sababu muhimu zilizochangia kutangazwa kwa
Azimio la Arusha tarehe 5/2/1967. Azimio hilo lilikuja na mkakati muhimu wa kuhakikisha
wananchi kwa pamoja wanashika njia kuu za uchumi.
Shughuli zote za uzalishaji na utoaji wa huduma ziliundiwa mashirika ya umma, lakini mashirika
mengi yaliendeshwa kwa hasara na yaliendesha shughuli za kiuchumi kwa kutumia mtaji na
ruzuku kutoka Serikalini.
Kabla na baada ya uhuru kuna vyombo vilivyoongeza chachu ya
wananchi kushiriki katika shughuli za uchumi ambavyo kwanza ni vyama vya
ushirika hasa katika uzalishaji.
Kutokana na matatizo mbalimbali mwaka 1972, Serikali za Mitaa vilivunjwa na badala yake
ukawekwa Mfumo wa Madaraka Mikoani uliotegemea zaidi Serikali Kuu kuliko nguvu za
wananchi na hapa ndipo matatizo ya kuwatenga wananchi na maendeleo yalipoanzia.
Kama hiyo haitoshi, vyama vya ushirika vilivunjwa mwaka 1976 na badala yake ulianzishwa
mfumo wa Washirika kama Jumuiya ya Chama ambayo iliendeshwa na kiserikali na matokeo
yake kila mmoja alishuhudia kufa kwa vitegauchumi vingi vilivyokuwa chini ya Serikali.
Ilipofika mwaka 1992, Serikali ilichukua hatua ya kuunda upya Serikali za Mitaa na kurudisha
Vyama vya Ushirika mikononi mwa wananchi mwaka 1984 ikiwa ni sehemu ya kutambua
makosa yaliyofanyika hapo awali.
Serikali ya Awamu ya Tano inaingia katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa
Miaka Mitano wa mwaka 2016/2017 – 2020/2021 unaojikita katika ujenzi wa uchumi wa
viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.
Lengo kuu la Mpango huo ni kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati inayoongozwa
na viwanda ifikapo mwaka 2025. Ni dhahiri, Tanzania kama zilivyo
nchi nyingine duniani inahitaji uchumi wa viwanda ili kuleta mageuzi ya haraka na kujenga
msingi imara wa uchumi.
Ni wazi kuwa katika kufanikisha malengo haya ni muhimu kwa mamlaka husika kuhakikisha
wananchi wanajumuishwa katika utekelezaji wa mpango huu na kuhakikisha maendeleo haya
yanaakisi na kujadili maendeleo ya watu.

By Jamhuri