Uamuzi wa Busara (3)

Wiki iliyopita katika kitabu hiki cha Uamuzi wa Busara, tulisoma kuhusu uamuzi wa TANU kwenda Umoja wa
Mataifa (UNO). Wajumbe wa Kamati Kuu ya TANU waliandika ujumbe kwa wajumbe wa Baraza la Umoja wa Mataifa waliotumwa nchini kuja kuchunguza hali ya nchi ambavyo katika ujumbe huo walitilia mkazo mambo haya.
Endelea tulipoishia…

  1. Ardhi ambayo ilikwisha kuchukuliwa na serikali wakapewa wageni wasiokuwa Waafrika ilikuwa ni kubwa mno.
    Ikaombwa kwamba ardhi isichukuliwe tena kwa Waafrika wakapewa wageni.
  2. Mishahara waliyokuwa wakilipwa Waafrika ilikuwa midogo mno. Ingefaa Waafrika nao wapewe mishahara ambayo ingewezesha kuishi vizuri.
  3. Ushuru wa pamba haukuwa wa haki kwa sababu ulikadiriwa bila ya kufikiria pato la mkulima na gharama za ukulima.
  4. Kupunguzwa ngombe kwa lazima kungekubaliwa kama kweli ingeonekana kwamba ni hatari kuwa na ngombe wengi. Lakini ngombe walipunguzwa kwa lazima hata mahali ambapo hapakuwa ni kweli kwamba ngombe wamezidi mno. Tena ulikuwa ni wajibu wa serikali kuwaonyesha wafugaji kwa mifano kwamba ngombe wachache wafugwao vizuri walikuwa bora kuliko ngombe wengi wasiofugwa vizuri. Jambo hili halikufanywa.
  5. Kodi ya ngombe ilikuwa ni kodi ya mtaji. Kwa desturi raia alikuwa akitozwa kodi ya pato lililokuwa likitokana na mtaji
    wake. Kumtoza raia kodi kwa mtaji wake kungepunguza mtaji huo na nguvu ya kuchuma zaidi. Kwa hiyo ingefaa zaidi kuwatoza wafugaji kodi kwa mali waliyokuwa wakipata kwa kuuza maziwa, siagi na kadhalika, si kwa kuhesabu vichwa vya ngombe.
  6. Baraza la Kutunga Sheria lingekuwa na wajumbe sawasawa na upande usiokuwa wa serikali kutoka kila taifa. Waafrika
    walikubali shauri hilo kwa sharti moja tu, kwamba halingedumu, na kwamba kwa sababu Waafrika walikuwa wengi zaidi, siku moja Waafrika wangekuwa na wajumbe wengi zaidi katika baraza hilo.
  7. Jambo la mwisho lilikuwa kubwa zaidi, TANU ilidai kwamba ingawa Tanganyika ilikuwa nchi iliyokaliwa na watu wa mataifa mbalimbali, ilikuwa ni nchi ya Waafrika na ilisimamiwa na kuongozwa ili baadaye itawaliwe zaidi na Waafrika. TANU ikaliomba Baraza la Udhamini na serikali iliyokuwa ikitusimamia watamke kwamba hivyo ndivyo.
    Wajumbe hao walipokwisha kuikagua Tanganyika kwa majuma yapatayo saba hivi wakaendelea na safari yao kwenda
    Somaliland vilevile kwa sababu ya ukaguzi.
    Walipotoka Somaliland walirudi Amerika, wakaandika taarifa ya mambo waliyoyaona Tanganyika na mambo ambayo wangependa yafanyike katika Tanganyika. Baadhi ya mambo hayo yalikuwa:-
  8. Waliona kwamba katika miaka minane iliyokuwa imepita Tanganyika ilikuwa imefanya maendeleo makubwa sana na
    kwamba kama lisingetokea jambo la kuzuia maendeleo nchi ingeendelea kwa upesi sana katika miaka iliyokuwa ikifuata.
  9. Kwa hiyo wakaomba itamkwe kwamba Tanganyika ingeweza kujitawala katika muda uliokuwa chini ya miaka 20 au 25.
  10. Tanganyika itakapojitawala mamlaka yawe mikononi mwa Waafrika.
  11. Tangu wakati huo mpaka wakati ambao Tanganyika ingejitawala ungefanywa mpango maalumu kwa mambo
    ambayo yangefanywa kuiwezesha Tanganyika kujitawala kwa muda huo.
  12. Baada ya miaka mitatu Baraza la Kutunga Sheria lingekuwa na Waafrika wengi zaidi kuliko upande ambao haukuwa wa
    serikali.
  13. Wajumbe wa baraza hilo wangechaguliwa na wenyeji wenyewe.
  14. Ardhi iliyokuwa imechukuliwa wakapewa wageni ilikuwa ni kubwa mno. Wageni wasipewe tena ardhi. Muda wa miaka 99 ambao wageni walikuwa wakikodisha ardhi ulikuwa ni mrefu mno; ingefaa upunguzwe na kufikia miaka 25.
    Na muda huo wa miaka 25 iwapo ungekwisha mgeni asingekubaliwa kukodisha tena ardhi hiyo ikiwa ardhi yenyewe ilikuwa ikitakiwa na Waafrika wenyewe.
    Taarifa hiyo ilipotangazwa Tanganyika ikawa kama mtu amekanyaga siafu. Magazeti ya Kizungu yakaanza kusema
    kwamba mambo hayo yalikuwa ni ya kipumbavu, watu waliyoyaandika walikuwa hawaaminiki, maoni yenyewe
    waliyapokea kutoka kwa Chama cha TANU na kwamba TANU kilikuwa ni chama cha watu wachache sana tena wafitini.
    Magazeti hayo yakaendelea kudai kwamba watu wengine wote wa Tanganyika, Wazungu, Wahindi na Waafrika kuondoa
    wachochezi wa TANU, walikuwa bado ni washenzi sana na ulikuwa upumbavu kufikiri kwamba wangeweza kujitawala
    katika muda uliokuwa umetajwa na kwamba ilikuwa vigumu kukisia ni lini watu kama hao wangeweza kujitawala.
    Yakaendelea kudai kwamba kama mambo hayo yangekubaliwa yangeleta ugomvi katika mataifa mbalimbali ikiwamo
    Tanganyika na kwamba maendeleo ya nchi yangeharibika kwa sababu watu ambao wangependa kuja Tanganyika au kutumia fedha yao kwa maendeleo ya Tanganyika wangeogopa, iwapo wangeambiwa kwamba baada ya muda huo Tanganyika ingejitawala.
    Viongozi wa TANU walipoona mambo hayo, na kwa sababu hawakuwa na gazeti lao wenyewe la kueleza maoni yao juu ya taarifa hiyo, waliliomba Baraza la Udhamini liwaruhusu wapeleke ujumbe wao Amerika ulieleze baraza hilo maoni yao na Waafrika wenzao.
    Habari hii ilipojulikana, wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria ambao hawakuwa upande wa serikali wakakubaliana kwamba wao pia wapeleke wajumbe huko Amerika kwenda kuipinga TANU.
    Hili lilikuwa jambo la kushangaza kidogo, maana baraza hilo lilikuwa na Waafrika 4, Wahindi 3 na Wazungu 7. Na TANU haikuweza kuamini kwamba wajumbe hao wote wangekubali kupeleka watu Amerika kwenda kuipinga TANU.
    Haikujulikana wangekwenda kuipinga TANU kwa jambo gani.
    TANU haikujali magazeti wala wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria, ikakusanya fedha na kumpeleka mjumbe wake Amerika.
    Mjumbe huyo wa TANU alikuwa ni Mwalimu Julius K. Nyerere ambaye aliondoka mjini Dar es Salaam tarehe 17.2. 1955 na kuhutubia kikao cha Baraza la Udhamini tarehe 7.3.1955. Katika hotuba yake alizidi kusisitiza na kufafanua maoni ya TANU kuhusu taarifa iliyokuwa imetolewa kwa wajumbe wa ukaguzi.
    Kuhusu wageni katika nchi, Mwalimu Nyerere alizidi kusisitiza:-
    “…Hawa wote ni Watanganyika wenzetu. Si haki hata kidogo kuwaambia wahame au kuwanyima haki ambazo raia wa
    Tanganyika anazistahili. Hatuna budi tushirikiane nao katika haki na wajibu wetu. Mradi tu tuwe sawa kweli na walio wachache wasifanywe kuwa sawa na wale walio wengi, usawa huo wa jumla si usawa wa kweli.
    “Usawa wa jumla ni kuwafanya Wazungu 22,000 na Wahindi 80,000 waliomo Tanganyika wawe sawa na Waafrika 8,000,000.
    Hatuukubali usawa huu. Tunakubali kwamba Mhindi mmoja ni sawa na Mwafrika mmoja.”
    Kuhusu wageni na ardhi alisema:-
    “Hatupendi wafukuzwe au wafanyiwe ubaguzi wa namna yoyote, lakini Wahindi na Wazungu tuliowakubali ni wale
    ambao wamekwisha kukubali kukaa Tanganyika daima. Mhindi ambaye bado yuko India au Pakistan si Mtanganyika.
    Kadhalika Mzungu aliye Uingereza au Ugiriki si Mtanganyika.
    Hao hatuwataki. Hatutaki nchi yetu iwe mahali pa kupunguzia Wahindi, Wazungu au Waamerika waliozidi katika nchi zao. Tutakaribisha wageni wanaokuja kufanya biashara nasi au kuanzisha viwanda maalumu ambavyo ni vya faida kwa nchi nzima…Lakini hatutaki wageni wanaohamia nchini kwa ajili ya kuchukua ardhi walime, ambao mara nyingi ni Wazungu au wale wanaokuja kutafuta maskani ambao hutoka Bara la Hindi, wageni wa namna hiyo hatuoni faida yao katika nchi na kuwakaribisha ni kukaribisha ugomvi kati ya mataifa yaliyomo Tanganyika.”
    Itaendelea…