Uchovu mara kwa mara – 2

Karibu tena msomaji wangu wa Safu hii ya Afya. Leo tutaendelea na
mwendelezo wa mada yetu ya wiki iliyopita kama nilivokuahidi. Kwa
kukukumbusha tu msomaji, wiki iliyopita nilieleza kuhusu sababu zilizo
nyuma ya uchovu uliokithiri.
Uchovu ambao mara nyingi huwa unakuja bila kujua hasa chanzo
chake; na wiki iliyopita nilikueleza sababu mbili kati ya nyingi
tutakazoendelea nazo wiki hii ambazo ni kukosa muda wa kutosha wa
kupata usingizi, na sababu zitokanazo na mlo na mwenendo mzima wa
ulaji.
Hivyo, kama nilivyokuahidi wiki iliyopita, leo tunaendelea kuzijua sababu
nyingine zinazosababisha uchovu uliokithiri na moja kwa moja tunaenda
kuangalia tabia za kutofanya mazoezi ya mwili. Kwa mtu ambaye hana
kabisa utamaduni wa kufanya mazoezi ya viungo, ni vigumu sana
kuondokana na uchovu.
Kuna faida nyingi sana za kufanya mazoezi ya viungo zikiwamo pamoja
na kuimarisha mfumo wa upumuaji, kuuwezesha moyo kufanya kazi
yake kwa ufasaha, kusukuma damu kwa kasi inayostahili na hivyo
kuimarisha usambaaji wa hewa safi ya oksijeni mwilini ambayo hii
inasaidia kwa kiasi kikubwa sana kuupa mwili nguvu.
Lakini pia mazoezi ya mwili yanasaidia kuimarisha misuli na vyote hivi
kwa pamoja vinasaidia sana kuondoa uchovu. Hivyo, jenga tabia ya
kufanya mazoezi au shughuli ndogondogo na hasa kama kazi zako za
kila siku zinakufanya uwe umekaa sehemu moja kwa muda mrefu.
Kitu kingine ambacho huenda hukuwahi kukifikiria kama kingeweza
kuwa chanzo kikubwa cha uchovu uliokithiri ni sababu za kisaikolojia.
Hapa namaanisha matatizo kama msongo wa mawazo na sonona au
depression kama wengi walivyozoea kuuita.
Ni kawaida kuwa na mawazo ya hapa na pale, lakini mawazo yakizidi
yanakuwa adui kwa afya ya akili na hata mwili kwa ujumla; na kwa
upande wa mwilini, mara nyingi sana kuwaza kupita kiasi kunaweza
kusababisha hali ya homa na uchovu wa mwili uliopitiliza.

Hivyo, nashauri ni vyema kuvitambua vitu vinavyokusababishia mawazo
ya kudumu na kukusababishia kuwa na msongo wa mawazo ili uweze
kukabiliana navyo. Tumia muda mwingi kufanya mambo ambayo
yanakupa furaha kama vile mazoezi ya viungo, kucheza na kuangalia
aina mbalimbali ya michezo.
Kwa kufanya hivyo, utakuwa unajiepusha na uchovu unaotokana na
msongo wa mawazo lakini pia utasaidia kuimarisha afya yako ya akili
na kujiepusha na matatizo ya kisaikolojia.
Lakini pia kama ukiona umefanya yote haya niliyokuelekeza na bado
uchovu umeendelea kudumu mwilini mwako, basi ni dhahiri uchovu huo
utakuwa umesababishwa na tatizo jingine la kiafya.
Yaani kuna uwezekano uchovu huo umesababishwa na homa ambayo
huenda bado hujaigundua na hapo ndipo unapolazimika kuwaona
wahudumu wa afya na kupatiwa vipimo na si kunywa dawa za kutuliza
maumivu pasipo kushauriwa na daktari.
Matatizo ya kiafya ambayo mara nyingi huambatana na uchovu
uliokithiri ni pamoja na anaemia, kisukari, sonona, maambukizi ya
kwenye njia ya mkojo, magonjwa yanayoshambulia mfumo wa
mmeng’enyo wa chakula na magonjwa ya moyo.
Ends

1263 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons