Usafiri Dar es Salaam Rapid Transit (UDART) Buses parked at Kamata yard in Dar es Salaaam recently. PHOTO|FILE

NA MICHAEL SARUNGI
Katika siku za karibuni, pamekuwapo na usumbufu kwa abiria wanaotumia huduma inayotolewa
na mabasi yaendayo haraka (UDART) kiasi cha kufikia hatua ya kutumia tiketi zinazotumiwa na
wasafiri wa daladala.
Ingawa wahusika wamejitahidi kutoa utetezi wao kwa kusema usumbufu huo ulisababishwa na
mgogoro uliokuwapo kati yao mshirika wao katika kazi, Kampuni ya Maxcom.
Kwa mujibu wa utetezi wao, ukataji wa tiketi kwenye mabasi yao umerudi katika mfumo wa
awali wa kieletroniki baada ya Kampuni ya Maxcom Afrika kuachia ‘nywila’ (password)
waliyokuwa nayo.
Wamesema hatua hiyo ya Maxcom kushikilia nywila za mfumo huo wa ukataji tiketi kwa njia ya
kieletroniki, ndiyo uliosababisha kutumika kwa tiketi za kawaida kwa njia ya mkono.
Huu ni utetezi wa funika kombe mwanaharamu apite, kwani matatizo dhidi ya huduma
zitolewazo na kampuni hii ya (UDART) hayajaaza leo wala jana; yamekuwapo na yataendelea
kuwapo.
Tangu kampuni hii ianze kutoa huduma za awali (interim service) mwaka 2015, pamekuwapo
na malalamiko mengi juu yao huku wahusika wakiwa wameziba masikio yao.
Mradi huu una upungufu mwingi unaoleta ukakasi unaosababisha tujiulize; kama huu mradi
utakuja kufikia matarajio yanayotarajiwa ya kuhakikisha matatizo ya usafiri Dar es Salaam
yanaisha.
Kampuni hii iliyotegemewa kuwa mkombozi wa usafiri katika Jiji la Dar, imeanza kuwa
kichefuchefu huku hali ikizidi kuwa mbaya kila kukicha na wananchi wakiendelea kukaa muda
mwingi vituoni.
Katika vituo vya magari haya, abiria kukaa saa mbili au tatu wakisubiri usafiri ni jambo la
kawaida lisilokuwa na mjadala; achana na udhaifu wa huduma yenyewe kwa watumiaji.
Wamilikiwa wa usafiri huu wameshindwa kuelewa kuwa Dar es Salaam ni mji mkubwa wa
kibiashara nchini, wenye watu zaidi ya milioni tano wanaochangia
asilimia kubwa ya pato la Taifa kiuchumi.
Kitendo cha wananchi kuendelea kupoteza muda mwingi kituoni wakihangaikia usafiri ni sawa
na kudhoofisha maendeleo ya nchi ambayo tayari yameanza kushika kasi kuelekea kwenye
uchumi wa viwanda.
Kwa jinsi hali ilivyo, kuna haja ya mamlaka husika kutafuta mwekezaji mwingine atakayekuja
kutoa ushindani kumaliza changamoto za usafiri ndani ya jiji hili kuliko kuwaachia (UDART)
wanaoonekana kushindwa.
Ni wakati mwafaka kwa wahusika kutafuta mwekezaji mwingine atakayekuja kusaidiana na
UDART kutafuta ufumbuzi wa janga hili la usafiri ndani ya jiji hili la Dar es Salaam.
Mwisho……..

By Jamhuri