Ufafanuzi kuhusu tuhuma dhidi ya Prof Faustine Bee

Na Mwandishi Wetu

Gazeti la JAMHURI linamwomba radhi Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Prof Faustine Bee, kutokana na habari zilizochapishwa katika matoleo ya kati ya Aprili na Septemba, 2016, habari zilihusu ufisadi katika Chama cha Akiba na Mikopo cha Wazalendo (Wazalendo SACCOS LTD) cha watumishi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

 

Uongozi wa gazeti la JAMHURI, unamwomba radhi Prof Faustine Bee, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, kwa usumbufu aliopata.

 

Ni kweli iliyokuwa Bodi ya Chama cha Akiba na Mikopo ya Wazalendo inatuhumiwa kwa upotevu wa fedha za Chama hicho kiasi cha Sh bilioni 3.381 uliotokea kati ya mwaka 2008 na 2012 na siyo Sh bilioni 6 kama ilivyoripotiwa awali.

 

Ukaguzi uliofanywa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania mwezi Aprili, 2012 ndio ulioibua upotevu huo na kesi kufunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi dhidi ya watuhumiwa wa ubadhilifu huo.

 

Katika taarifa ya ukaguzi huo, hakuna kiongozi yeyote wa Chuo, akiwemo Makamu Mkuu wa Chuo Prof Bee, aliyetuhumiwa kwa ufisadi uliofanywa katika Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Wazalendo.

 

MUCCoBS iliongozwa na Mkuu wa Chuo (Principal) kwa kiswahili sanifu “Ras wa Ndaki” na si Makamu Mkuu wa Chuo (Vice Chancellor) kama ilivyooelezwa kwenye makala zilizotolewa. Wakati upotevu huo wa fedha unatokea mwaka 2008, Prof. Faustine K. Bee hakuwa Makamu Mkuu wa Chuo.

 

Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kwa kifupi “MoCU” na Chama cha Akiba na Mikopo cha Wazalendo ni taasisi mbili tofauti kisheria na zenye uongozi wake kila mmoja. MoCU ni Chuo Kikuu cha umma kilichoanzishwa chini ya Sheria ya Vyuo Vikuu Tanzania, 2005 sura ya. 246 na kupewa Hati Idhini yake mwaka 2015; Wazalendo SACCOS LTD ni chama cha ushirika kilichoanzishwa na kupewa nambari ya usajili KLR 2065; na kuandikishwa chini ya Sheria ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013 na inasimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi inayochaguliwa na wanachama kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirka ya mwaka 2015, Kanuni za Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo za mwaka 2015 na Masharti ya Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo Wazalendo ya mwaka 2017.

 

Matatizo ya utopevu wa fedha katika Chama cha Wazalendo SACCOS, hayana uhusiano wowote na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi. Matatizo hayo yanashughulikiwa na Bodi ya Chama hicho kwa kushirikiana na Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania, vyombo vya Usalama na Mahakama.

 

Uongozi wa Chuo hauna mgogoro wowote wa kikazi na watumishi wake kuhusiana na matatizo ya Wazalendo SACCOS LTD bali umewasaidia wanachama kutatua sintofahamu hiyo na kuifanya Wazalendo SACCOS kuwa kati ya vyama vya ushirika vinavyofanya vizuri.