Desemba 9, mwaka huu, Watanzania tumeadhimisha miaka 51 ya Uhuru wa nchi yetu, huku wengi wetu wakikabiliwa na maisha magumu kupindukia. Binafsi ninaamini kuwa ni unafiki kusema Tanzania haina cha kujivunia, lakini pia ni unafiki kusema Serikali kupitia Uhuru huu, imeboresha maisha ya wananchi.

Ni ukweli usiopingika kwamba Uhuru umewaondolea Watanzania kero za kudhalilishwa na wakoloni kwa kutandikwa viboko, kuuzwa minadani na utumwa wa kushurutishwa kufanya kazi ngumu. Uhuru pia umetuwezesha Watanzania kuunda Serikali yetu, wananchi kuwa huru kutoa mawazo binafasi, kuchagua dini ya kuabudu, kutembea, kufanya kazi na kuishi kihalali sehemu yoyote nchini.

 

Licha ya mafanikio machache yanayoonekana wazi, taswira halisi inaonesha kuwa maisha ya Watanzania yamezidi kuwa magumu tofauti na walivyotarajia kabla ya Uhuru.

Baada ya mizizi ya wakoloni (Wajerumani na baadaye Waingereza) kung’olewa nchini kwa juhudi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na wenzake, Watanzania walitarajia neema ya maisha bora. Hata hivyo, dalili za kuyeyuka kwa matarajio hayo zilianza kuonekana miaka michache baada ya Mwalimu Nyerere kung’atuka madarakani (alistaafu urais mwaka 1985).

 

Misingi ya uongozi bora iliyojengwa na mwasisi huyo wa Taifa letu imeendelea kumomonyoka siku hadi siku. Kiwango cha uadilifu na uaminifu katika matumizi ya rasilimali za umma kimeendelea kupungua kwa viongozi wengi tunaowakabidhi dhamana mbalimbali.

 

Matokeo yake, unafuu tulioutarajia baada ya Uhuru umeendelea kubaki kitendawili kigumu. Uhuru wetu umeyeyusha matarajio yetu ya kupata maisha bora. Ugumu wa maisha ndio kilio kikuu cha Watanzania wengi.

 

Leo kati ya Watanzania zaidi ya milioni 45, wanaofaidi matunda ya Uhuru nchi hii kwa ujumla wao wanaweza wasifike asilimia 10. Maisha ya wengi ni ya kubahatisha tu.

 

Nchi yetu ilipojinasua kutoka katika makucha ya wakoloni Watanzania tulitarajia maisha bora. Tulitarajia kupata huduma bora za afya na elimu kwa usawa. Leo wanaonufaika na huduma hizo ni viongozi na matajiri wachache wanaoneemeshwa na kodi za wananchi wanyonge!

 

Tulitarajia kupata huduma nzuri za maji safi na salama bila kuweka kando miundombinu ya barabara za lami na changalawe zinazopitika kirahis muda wote. Leo nchi ya Tanzania ni huru kwa miaka 51 lakini wananchi wengi wanaoishi mijini na vijijini wanakunywa maji machafu yasiyo salama!

 

Sekta ya kilimo inayotajwa siku zote kuwa ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu imetelekezwa, wakulima wadogo ambao ndiyo wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula na biashara hawajawezeshwa ipasavyo. Wajanja wachache ndiyo hunufaika na ruzuku ya pembejeo inayotolewa na Serikali kwa ajili ya wakulima hao.

 

Wakati wakulima wakichezewa ‘kekundu’ hako, wafanyakazi wa ngazi ya chini serikalini na katika kampuni binafsi, wameendelea kukandamizwa na waajiri wao kwa kulipwa ujira duni usiokidhi mahitaji ya msingi ya binadamu. Serikali inalijua hilo lakini imeendelea kukaa kimya.

 

Lakini pia wananchi wengi wameendelea kukosa ajira na kukabiliwa na uchumi duni, huku viongozi na matajiri wachache wakizidi kujiimarisha zaidi kiuchumi kupitia migogo ya wanyonge. Haya ni matokeo ya viongozi wetu wengi kutanguliza maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya umma.

 

Baada ya kupata Uhuru, nchi yetu iliridhia maazimio mbalimbali ya kimataifa yakiwamo ya utawala bora wa kisheria na kuheshimu haki za binadamu. Lakini kimsingi mambo hayo hayatekelezwi kwa vitendo nchini.

 

Utawala bora na unaoheshimu haki za binadamu hauwezi kufumbia macho matatizo ya wananchi wengi kukosa huduma bora za afya, elimu, maji na barabara. Haya ni miongoni mwa matatizo tuliyotarajia yangebaki historia baada ya nchi yetu kupata Uhuru lakini matokeo yamekuwa kinyume.

 

Inashangaza kuona na kusikia viongozi wa Serikali yetu ni hodari wa kubuni na kuweka mipango mizuri ya maendeleo ya wananchi, lakini utekelezaji wake siku zote si wa kuridhisha.

 

Viongozi na wataalamu wengi wanaopewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa mipango hiyo, mara nyingi wamekuwa wa kwanza kutumia mwanya huo kujimegea mali za umma kwa ajili ya kunjineemesha na familia zao.

 

Bado Serikali haijaonesha dhamira ya kweli ya kudhibiti mfumko wa bei za bidhaa nchini, licha ya kufahamu ukubwa wa tatizo hilo kwa Watanzania wanyonge wasio na uwezo wa kujigharimia milo mitatu kwa siku. Hili tatizo ni miongoni mwa matatizo yaliyostahili kudhibitiwa kwa nguvu kubwa katika nchi yetu huru.

 

Viongozi wa Serikali watambue kuwa Uhuru wa nchi yetu ulilenga kuboresha maisha ya Watanzania na kwamba hadi kipindi hiki cha miaka 51 ya Uhuru bado lengo hilo halijafikiwa. Serikali inapaswa kuwa macho isijejikuta inatoa mwanya kwa Watanzania kutamani maisha ya utumwa wa kikoloni kuliko ya Uhuru wao.

 

Serikali ijitambue kwamba ndiyo mzee wa mji wa Watanzania, hivyo ihakikishe inakuwa na mikakati thabiti ya kuboresha maisha ya wananchi ikiwa ni pamoja na kuwezesha huduma bora za afya na elimu kwa wote. Miaka 51 ya Uhuru wa nchi yetu iwe chachu ya kurejesha matarajio ya Watanzania huru.


847 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!