Matukio ya ukatili wa kijinsia yanaongezeka. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema mwaka jana kulikuwa na matukio 41,000; kati ya hayo matukio 13,000 yaliwalenga watoto.

Wizara inasema asilimia 27 ya wasichana wenye umri wa miaka 15 -19, ama wamejifungua au ni wajawazito.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk. Faustine Ndugulile, amesema mikoa ya Mara na Shinyanga – kwa takwimu za mwaka 2015/2016 ndiyo inayoongoza kwa matukio ya ukatili kwa kuwa na asilimia 78.

Waziri Ndugulile alikuwa akijibu maswali kwenye ‘group’ la Whatsapp la Tanzania Yetu, yaliyolenga ukatili wa kijinsia, mimba na ndoa za utotoni.

Mkanganyiko wa sheria na umri wa ndoa vimeelezwa na Dk. Ndugulile kuwa miongoni mwa vyanzo vya ndoa na mimba za utotoni.

“Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inasema mtoto wa umri wa miaka 16 anaweza kuolewa. Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inamtambua mtu yeyote aliye chini ya miaka 18 kuwa ni mtoto,” amesema.

Baadhi ya mila zinaruhusu ndoa baada ya msichana kuvunja ungo; kama ilivyo kwa baadhi ya maandiko ya dini.

Amesema umaskini na uduni wa elimu ni vikwazo vingine katika kukabiliana na mimba za utotoni.

 “Takwimu zinaonyesha kadiri ya elimu na uwezo (kifedha) wa kifamilia unavyopanda, umri wa kuolewa ndivyo unavyopanda na idadi ya watoto kupungua,” amesema.

Serikali imeandaa mpango wa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. Mpango huo ni wa mwaka 2017/2018 – 2021/2022. Imekusudiwa kuwa ifikapo mwaka 2020 – 2022 asilimia 50 ya ukatili itakuwa imeondolewa Tanzania; na kuumaliza kabisa ifikapo mwaka 2050.

“Niwahakikishie, sisi wizara tunafuatilia kwa karibu matukio yanayoripotiwa na vyombo vya habari. Navipongeza vyombo vya habari kwa kufuatilia matukio ya ukatili wa kijinsia.

“Ujenzi wa mabweni unasaidia kupunguza ujauzito na kuongeza ufaulu. Nakiri kuwa kumekuwa na ucheleweshaji wa kesi za ukatili unaochangiwa na mhalifu kumalizana kifamilia na mwathirika.

“Ucheleweshaji wa uchunguzi kwenye Jeshi la Polisi na mashauri kuchukua muda mrefu,” amesema Dk. Ndugulile na kuongeza:

“Tunatarajia kukaa na Jeshi la Polisi na Mahakama ili mashauri ya ukatili wa jinsia yaharakishwe na haki ipatikane haraka.”

Ameshauri jamii na wadau wa maendeleo waendelee kushirikiana na serikali kukomesha matukio yote ya kihalifu nchini.

Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini, Yassin Ally, anasema ukatili wa kijinsia unawaathiri zaidi watoto kwa kufeli mitihani, kupata mimba na kuathirika kiafya na kisaikolojia.

Ally amesema kati ya kaya 10, nane zinafanya vitendo vya kikatili kwa mikoa ya Mara na Shinyanga. Mkoa wa Manyara unaongoza kwa ukeketaji.

“Bunda [Mara] tumeambiwa baadhi ya watoto wa shule wanalala milango wazi katika ma-ghetto waliyopanga, kama kivutio cha wanaume. Wengine wanalala kwa wanaume halafu asubuhi wanakwenda shuleni. Aibu gani hii? Hili tatizo lazima likomeshwe kabisa.

“Kule Shinyanga, baadhi ya nyumba za kupanga zinatumiwa na vijana kuingiza wasichana wadogo kufanya ngono, wakiwamo wanafunzi,” anasema Ally.

Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Jogoro Kiswalo, anasema watoto 563 wakiwamo wanafunzi wa sekondari wamepata ujauzito wilayani humo. Mimba hizo ni kuanzia mwaka 2013 hadi Oktoba, mwaka huu.

Anasema ni watu wawili pekee ndio waliohukumiwa kwenda jela kwa hatia ya kuwatia mimba wanafunzi. Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inasema kufanya ngono na mwanafunzi ni kosa la jinai.

Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989 ambao Tanzania imeridhia mwaka 1991 unasisitiza wazazi, walezi, jamii na serikali kumlinda mtoto.

“Inashangaza sana. Wanafunzi 563 wamepata mimba, halafu waliofungwa ni wawili tu. Wengine wako wapi? Polisi si mpo?

“Hapa polisi hawajawajibika vizuri. Mahakama zinahitaji ushahidi usioacha shaka,” anasema Kiswalo.

Shirika la Kivulini linalopiga vita ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana limeitisha kampeni ya kuzua vitendo hivyo katika wilaya za Bunda na Tarime (Mara), Shinyanga na Misungwi mkoani Mwanza.

Mkazi wa Mihongo, Joseph Sarya, ambaye ni mzee wa kimila anasema watoto wadogo hufanyishwa ngono kwa malipo ya Sh 500.

 Mariam Chacha, mkazi wa Mihingo yeye ameutaja ulevi wa pombe, uzinzi, mmomonyoko wa maadili na utandawazi ndiyo chanzo cha ukatili huo wa kingono.

Ameshauri serikali, wadau, wazazi na mashirika ya kutetea haki za binadamu waongeze kasi ya uchukuaji wa hatua dhidi ya wanaotenda ukatili huo wa kijinsia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Amos Kusaja, hakutaka kuzungumzia suala hili licha ya kuombwa na JAMHURI.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, Neema Ibamba, anasema kuna tatizo kubwa la mimba za utotoni.

 “Kwa kabila la Wakurya lipo tatizo la nyumba ntobhu [mke kuoa mke], ingawa linazidi kupungua kutokana na elimu inayotolewa juu ya madhara yake.

Kwa mila za makabila ya Wakurya na Wazanaki mke ambaye hakujaliwa kupata watoto kwa idadi anayotaka, huoa mke na kumkabidhi ndugu mwanaume wa karibu kiukoo ili amzalie. Watoto wanaozaliwa wanakuwa wa mwanamke aliyetoa mahari.

“Mwanamke akishamuoa, kazi ya aliyeolewa amzalie watoto. Anafanya mapenzi na mwanamume yeyote ilimradi tu abebe mimba na kuzaa.

 “Akiachisha anatembea tena na mwanamume mwingine yeyote ili apate mtoto. Watoto wote wanaozaliwa wanakuwa mali ya huyu mwanamke aliyemtolea mahari. Hata majina wanaitwa ya mama aliyeoa,” anasema.

Ofisa wa Dawati la Jinsia wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara, Fatuma Mbwana, anasema polisi inafuatilia matukio ya uhalifu kwa kufungua majalada ya upelelezi na kuwakamata watuhumiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Mara, Juma Ndaki, amesema tatizo linalokwamisha kesi nyingi mahakamani ni upande wa mtoto aliyetiwa mimba kukataa kuendelea na kesi.

Anasema wazazi na walimu ndio wanaochangia kuharibu watoto, kwani wengi wao hawawajibiki kuwalinda kimaadili.

 “Ingawa hapa nilipo sina takwimu, lakini kwa upande wetu takwimu za ukatili mwaka huu zimepungua kuliko za mwaka jana.

“Tunakamata mwanamke, tunakamata mwanamume aliyempa mimba. Lakini suala likifika mahakamani mtoto wa kike anakataa tena kuendelea na kesi.

“Anatishwa kwa kuambiwa, ukizaa huyo mtoto atalelewa na nani kama baba yake atafungwa?” anasema RPC Ndaki.

By Jamhuri