Msanii wa Bongo Fleva, Ibrahim Musa aka Roma Mkatoliki, aliyetoweka baada ya kudaiwa kukamatwa mapema siku ya Alhamisi katika mji wa Dar es Salaam, amepatikana na amekuwa akihojiwa kwa saa kadhaa baada ya kupatikana.
Taarifa zinasema Roma Mkatoliki alirudi kwake Jumamosi alfajiri, na baadaye kuelekea kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam, ambako alifanyiwa mahojiano na baadaye kupelekwa Hospitali ya Mwananyamala, jijini.
JAMHURI halikuweza kubaini mara moja sababu ya msanii huyo kupelekwa Hospitali ya Mwananyamala hasa baada ya kuhojiana na Polisi. Bado hakuna maelezo ya kutosha kuhusiana na wapi walipokuwa na nani waliokuwa wamewashikilia.
Kupatikana kwao kumefuatia wito mkubwa wa wasanii wenzake na mashabiki kuhusu kuachiliwa huru – ndani na nje ya mitandao ya kijamii.
Awali, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alinukuliwa akisema bado walikuwa wakiendelea na upelelezi wa tukio la kupotea (kutekwa) kwa msanii Roma Mkatoliki na wenzake.
Akizungumza kuhusu kupatikana kwa Roma Mkatoliki, wakili wake, Jebla Kambole, amesema hawakupewa fursa ya kushuhudia mahojiano baina ya mteja wao na Polisi
“Hatukuruhusiwa kushuhudia mahojiano baina ya mteja wetu, tulipaswa kupata fursa hiyo ili kujiridhisha kama haki zake zimelindwa…nimemuona ana mikwaruzo-mikwaruzo, wenzake wanaonekana wako vizuri. Ngoja tuendelee kusubiri ripoti ya daktari,” amesema Kambole.
Roma Mkatoliki ameongea na waandishi wa habari baada ya kutoka Hospitali ya Mwananyamala, huku akithibitisha kwamba yeye ni mzima pamoja na wenzake watatu.
“Kutokana na mazingira yalivyo, hatutakuwa na maneno ya kuzungumza. Tuko kwenye taratibu za uchunguzi, hatuwezi kusema chochote…nadhani Jumatatu (jana) tutakuwa na mkutano na waandishi wa habari.
“Ninawashukuru Watanzania wenzangu, wasanii…sijapata muda wa kuingia kwenye mitandao ya kijamii ila nimeambiwa kila kilichokuwa kinaendelea,” amesema Roma.
Akizungumza na JAMHURI, msanii wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Ney wa Mitego’, amesema kukamatwa kwa Roma Mkatoliki na watu wasiojulika kunajenga hofu kubwa ndani ya moyo wake pamoja na muziki wa Hip-hop kwa sababu hali hiyo haizoeleki.
Amesema kuwa Tanzania ni nchi ya amani, hivyo ni vyema vyombo husika vikachukua hatua ili kudhibiti vitendo vinavyoendelea kujitokeza na kuacha madoa katika amani iliyopo.
“Kukamatwa na kutekwa kwa Roma ni viashiria vya uvunjifu wa amani, kwani haileti picha nzuri katika tasnia ya muziki hapa nchini,” amesema Ney.
Msanii huyo wiki mbili zilizopita naye alijikuta mikononi mwa Polisi, baada ya kuachia wimbo wake wa ‘Wapo’, kabla ya Rais John Magufuli kuingilia kati na kusema msanii huyo aachiwe, huku akishauri maudhui ya wimbo huo kuongezwa.
Ney amesema baada ya kukamatwa kwa msanii huyo, amekuwa na maumivu, wasiwasi ndani ya moyo wake, huku akieleza kuwa ni vyema vyombo husika kuwa makini na kuwachukulia hatua wahusika.
Msanii huyo amesema mpaka sasa hajui sababu ya kukamatwa ama kutekwa kwa msanii mwenzake.
 “Serikali inatakiwa kuwa makini ili kudhibiti vitu vinavyoendelea kutokea kwa sababu vinaweza kujenga watu sugu ndani ya mioyo yao, kwa kuzoea kuona watu wanafanya vitendo vibaya,” amesema Ney.
Hata hivyo, amesema baada ya kupata taarifa ya kupatikana kwa msanii huyo, anaweza kupata usingizi kwani kabla ya hapo ilikuwa vigumu kulala.
Naye Rais wa Shirikisho la Filamu nchini, Simon Mwakifwamba,   amesema kuwa taarifa ya kukamatwa kwa msanii Roma kumeleta majozi makubwa kwa wasanii hapa nchini.
Amesema kwa upande wake, bado hajajua sababu ya kukamatwa kwa msanii huyo, licha kupata taarifa yupo katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay.
Amesema kuwa baada ya kupata taarifa ya kupatikana kwa msanii huyo, amekuwa miongoni mwa watu wenye maswali mengi kuhusu mazingira ya kupatikana kwake.
“Nimekuwa nikijuliza kama wamepotea walifikaje Kituo cha Polisi cha Oysterbay? Walifika kwa kutumia usafiri gani? Nani aliwaona? Nani kawaleta Oysterbay Polisi?” amesema Mwakifwamba.
Amesema kuwa wanashukuru Mungu baada ya kupata taarifa ya kupatikana kwa msanii huyo, ambapo kama wapo hai ni jambo jema ambalo tunapaswa kuendelea kumshukuru Mungu.
“Tunasubiri taarifa za kutoka Jeshi la Polisi hapa kituo cha polisi Oysterbay ili tuweze kuwaona ndugu zetu,” amesema Mwakifwamba.
 Naye msanii wa nyimbo za asili, Mrisho Mpoto ‘Mjomba’, akiwa katika eneo la kituo cha Polisi cha Oysterbay, amesema kuwa amemuoa msanii Roma ndani ya kituo hicho cha polisi akifanya mahojiano na polisi.
Mpoto amesema kuwa amefurahi kumuona akiwa hai, huku akieleza kuwa bado hajajua alikuwa wapi na amepatika katika mazingira gani.
Roma akiwa na wasanii wenzake, wanadaiwa kutekwa juzi Alhamisi na watu wasiojulikana wakiwa kwenye Studio za Tongwe Records, Masaki jijini Dar es Salaam, walipokuwa wakifanya shughuli zao za kawaida.
Mbali na Roma, wengine wanaodaiwa kutekwa ni msanii Moni Centrozone, Bin Laden na Imma ambaye ni mfanyakazi wa mama mzazi wa mmiliki wa studio hizo, Junior Makame.
Jana, baadhi ya wasanii waliitisha mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa ufukwe wa bahari wa Coco na kueleza juhudi ambazo wamezifanya za kuwasaka akina Roma pasipo mafanikio.
Akizungumza katika mkutano huo, Junior amesema hadi sasa bado haijajulikana wasanii hao walipo pamoja na jitihada za kuripoti na kukagua katika vituo vya polisi.
“Tunaomba Serikali itusaidie na wananchi, huu si wakati wa kulalamika na kushutumu mamlaka zozote kwa kuwa hakuna anayejua wasanii hawa walipo,” amesema Junior.
Katika mkutano huo uliojumuisha wasanii mbalimbali nchini, Junior alisema lengo la mkutano huo si kumlaumu mtu wala vyombo vya Serikali, isipokuwa ni kuomba ushirikiano kwa jamii.
Akielezea tukio hilo, Junior amenukuliwa akisema siku hiyo alishinda studio na ilipofika muda wa jioni, Roma alimpigia simu na kumwambia kuwa anakuja kurekodi.
Amesema baada ya simu ya Roma, alipigiwa simu kutoka nyumbani kwake akielezwa kuwa mtoto wake anaumwa na anatakiwa kufikishwa hospitali, hivyo alilazimika kuondoka.
“Nimetoka, nimefika tu nyumbani, baada ya muda kuna dada alinipigia simu ambaye na yeye kwa muda huo ndiyo alikuwa anaingia studio na kunieleza kuwa kuna watu wamekuja wakiwa kwenye gari aina ya Noah walimhoji Roma, baadaye waliwahoji watu wengine kisha wakaingia studio na kuchukua televisheni pamoja na kompyuta,” amenukuliwa Junior.
Amesema baada ya kupata taarifa hizo, alilazimika kurudi tena studio kabla ya baadaye kuanza kufanya mawasiliano na watu mbalimbali akiwamo Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba.
“Baada ya kupata taarifa hiyo kwa undani nilimpigia simu kaka yangu Ruge nikamwelezea yaliyotokea studio, akanishauri niende kutoa taarifa polisi nikaenda Oysterbay polisi, nikaripoti lakini sikupaswa kutoa maelezo kwa sababu sikushuhudia tukio na kulazimika kuchukua maelezo kwa mtu ambaye alinipigia simu, baada ya kuchukua maelezo hayo walifungua shauri lenye RB namba 0B/RB/72/017,” alinukuliwa Junior na gazeti moja la kila siku.

By Jamhuri