Kampuni ya Usafirishaji wa Vifurushi (DHL) imeelezwa kutumiwa na wafanyabiashara haramu ya dawa za kulevya, kwa kusafirisha dawa hizo ndani na nje ya nchi.

Vyanzo vya habari vya uhakika vimeliambia JAMHURI kuwa wauza unga wamekuwa wakitumia kampuni ya DHL kusafirisha dawa za kulevya bila kushtukiwa na vyombo vya dola.

JAMHURI limepata taarifa za kuwapo kwa mtandao wa kusafirisha dawa za kulevya kwenda nchi za Nigeria, Uturuki, Uholanzi na Afrika Kusini kupitia kwenye viwanja vikubwa vya ndege hapa nchini.

Mtandao huo umekuwa ukiwahadaa au kuwarubuni baadhi ya watumishi wanaohusika na ukaguzi wa mizigo hasa katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam.

Wauzaji unga wanatumia mbinu ya kuonesha wanasafirisha nguo na urembo kwenda nje ya nchi, kumbe wanapitisha dawa za kulevya zinazokamatwa nje ya nchi.

Kampuni ya DHL baada ya kupokea mizigo huipeleka uwanja wa ndege kwa ukaguzi kisha kupakiwa kwenye ndege na kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Huwezi kuamini kuna mizigo inaletwa mpaka DHL inachukuliwa na kupakiwa kwenye ndege, lakini ikifika Nairobi na kukaguliwa hugunduliwa kuwa ni dawa za kulevya,” anasema mtoa taarifa.

DHL imekuwa ikipata taarifa za kuwapo kwa vifurushi vya dawa za kulevya ambavyo vinapitishwa kwenda nje ya nchi, lakini haichukui hatua yoyote.

Januari 24, mwaka huu, kampuni ya DHL-Kenya kupitia kwa mmoja wa maafisa wake, James Mwangi, aliwasiliana na DHL-Tanzania kwa barua pepe, kuwaeleza kuwapo kwa mzigo uliokutwa na dawa za kulevya na ukiwa umepitishwa kwenye ukaguzi na kampuni hiyo kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.

Baadhi ya mizigo iliyotajwa kubeba dawa za kulevya ni pamoja na mzigo namba 5333406374 uliotumwa Januari 21, mwaka huu ukiwa na uzito wa kilo 2, huku mtumaji akiwa ni Roblam Ally Eden mkazi wa Kariakoo Jijini Dar es Salaam. Mzigo huo ulitumwa kwa Hamdi Ali aliyeko nchini Uholanzi.

Mzigo mwingine wenye namba 3050869356 wenye uzito wa kilo 3, ulitumwa na Adam Kidume Denge, mkazi wa Zanzibar. Mzigo huo alikuwa anatumiwa Ike Ijeoma aliyeko nchini Nigeria.

Mzigo namba 7342211354 wenye uzito wa kilo 3 nao ulikuwa unasafirishwa kwenda nchini Canada. Nyaraka zilizotumika kusafirisha mzigo huo hazikuwa kwenye ubora mzuri, hivyo kutoonesha jina la mtumaji wala mpokeaji wa mzigo huo.

Mzigo namba 7343262603 wenye uzito wa kilo 3 ulitumwa na Ramadhani Gumbo, mkazi wa Kigamboni Dar es Salaam. Mzigo huu ulikuwa unatumwa kwa Sean Makoena ambaye anuani yake ni Flat 6, Reflex Apartment, Famagusta Mersin, Uturuki (North Cyprus).

Katika mzigo huo, nyaraka kutoka ofisi ya DHL Dar es Salaam zinaonesha kwamba alikuwa anasafirisha fulana tisa zilizokuwa na uzani wa kilo 3, lakini baada ya kufika kwenye ukaguzi kwenye mashine za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta ikagundulika ni dawa za kulevya.

JAMHURI kwa kushirikiana na wanahabari wa nchini Kenya, limezungumza na Mkuu wa Kitengo cha Mizigo, James Mwangi, ambaye ameliambia anakumbuka kukamatwa kwa dawa za kulevya, lakini wamekuwa wakiwasiliana na vyombo vya ulinzi na usalama vya nchini humo.

“Suala hilo sasa liko mikononi mwa vyombo vya ulinzi na usalama hapa Nairobi… sisi kazi yetu ni kutoa taarifa kwa mamlaka tu,” amesema Mwangi.

Hata hivyo, imethibitika kwamba mizigo hiyo ambayo imekuwa ikitumwa nchi mbalimbali kwa kutumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, imekuwa si mizigo halisi isipokuwa ‘unga’.

Moja kati ya mifano, ni mzigo uliopitishwa Dar es Salaam kwamba zilikuwa ni fulana, lakini baada ya ukaguzi Nairobi, ikabainika ilikuwa ni bangi na mirungi.

Chanzo cha habari kimeliambia JAMHURI kuwa kampuni hiyo imekuwa ikipata taarifa za kuwapo kwa vifurushi vyenye dawa za kulevya, lakini haichukui hatua.

Imeelezwa kuwa DHL inao mtambo mahsusi wa kukagua mizigo, lakini wanashangaa dawa hizo zimekuwa zinapitaje kwenye mashine.

Mmoja wa watuhumiwa wa kusafirisha dawa za kulevya, Ramadhani Gumbo, amezungumza na JAMHURI na kusema hajawahi kutuma mzigo wowote nchini Uturuki, huku akisisitiza kwamba yeye ni miongoni mwa watu wanaopinga matumizi ya dawa za kulevya.

JAMHURI: Unakumbuka kutuma mzigo wowote nje ya nchi, siku za hivi karibuni?

GUMBO: Duh! hii ni kesi braza, nimewahi kutuma mzigo nje ya nchi, lakini ilikuwa zamani sana. Mzigo huo niliutuma nchini Marekani. Unajua mimi natengeneza ‘culture’ na kuziuza. Lakini tangu nitume mzigo huo wa ‘culture’ nchini Marekani sijawahi kutuma mzigo mwingine tena. Sikutuma unga.

JAMHURI: Namba hii ya simu 0745 440099 ni yako? Umeanza kuitumia lini?

GUMBO: Ni kweli namba hiyo ni yangu! Nimeanza kuitumia hivi karibuni baada ya kuacha kutumia namba yangu nyingine ya Tigo.

JAMHURI: Namba hiyo imetumika kutuma mzigo nchini Uturuki, mzigo huo ni dawa za kulevya, unafahamu chochote?

GUMBO: Oohh…braza wangu…hiyo ni kesi kabisa. Maana sasa unga ni ‘issue’. Lakini ngoja nikwambie ukweli kabisa, mimi najihusisha na muziki sasa, bahati mbaya sana wasanii wanahusishwa na dawa za kulevya, itaniharibia ‘future’ yangu. Maana sasa naishi na mchumba wangu Mzungu kutoka Ireland, akigundua hili bila kujali ukweli wake itakuwa mbaya sana kwangu.

JAMHURI: Uchumba wenu una muda gani? Mchumba wako mlikutana namna gani? Je, anajihusisha na shughuli gani hapa nchini?

GUMBO: Uchumba wetu sasa una miezi mitatu, nilikutana naye kwenye tamasha la sanaa huko Bagamoyo. Mwaka mpya 2017, nilimtambulisha kwa baadhi ya ndugu zangu. Huyu mchumba wangu ni fundi mzuri sana wa mashine kubwa za kufua umeme… ila sasa hafanyi kazi, tunaishi pamoja Kigamboni. Ni mama wa ndani. Lakini amekuwa ananiwezesha maisha yangu kwa asilimia 90. Unajua huyo binti, baba yake ni mkulima mkubwa sana huko Ireland. Amekuwa anatumia kadi yake ‘credit card’ kunihamishia fedha kwenye akaunti yangu, fedha ambayo imenisaidia kurekodi albamu ya muziki wa ‘reggae’.

JAMHURI : Hudhani kwamba mchumba wako anaweza kutumia jina lako kusafirisha huo ‘mzigo’?

GUMBO: Hawezi kabisa! Unajua yule kwao ni Wakatoliki safi. Mchumba wangu amekuwa akinisisitiza sana kuacha kuvuta bangi. Siamini kwamba anaweza kushiriki kusafirisha unga. Siyo siri mimi bangi naivuta brother…

Kwanza yeye hukaa ndani tu muda wote akijisomea vitabu, hana mawasiliano na mtu mwingine yeyote isipokuwa mimi tu. Lakini pia haongei Kiswahili, yeye anaongea Kiingereza tu.

“Mimi ni msanii wa kuimba na kutengeneza bidhaa za mikono, natengeneza ‘culture’ ambazo ninaziuza, sijihusishi wala sitarajii kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Pia huko DHL sijatuma huo mzigo unaousema labda kama kuna mtu katumia jina langu,” amesema Gumbo.

Alipoulizwa imekuwaje mzigo huo umeandikwa jina lake kamili ikiwa ni pamoja na namba za simu, Gumbo amesema hajui chochote kwani siyo yeye aliyehusika na mzigo huo.

Akizungumza na JAMHURI ofisini kwake, Meneja Usafirishaji wa kampuni ya DHL-Tanzania, Simon Mutebi, amesema jambo kama hilo ni geni kwake na hajawahi kulisikia kwa miaka yake zaidi ya 10 ya utumishi wake ndani ya kampuni hiyo.

Amesema tuhuma hizo zinaweza kuwa zinatolewa na watu waliojaa maslahi yaliyojificha katika ajenda ya kile kitu wanachokijua wao, na wanataka kuichafua kampuni.

“Tuhuma kama hizo ni nzito… zinahitaji umakini wa hali ya juu unapotaka kuzitoa hasa katika kipindi hiki ambapo Serikali ya Rais Magufuli imetangaza vita dhidi ya dawa za kulevya,” amesema Mutebi.

Kuhusu uimara wa Idara ya Ukaguzi, amesema Idara ya Ukaguzi ndani ya kampuni hiyo iko vizuri kuanzia walinzi wa milangoni hadi mashine zinazotumika katika ukaguzi wa mizigo inayoingia na kutoka ndani ya kampuni hiyo hali inayowafanya wasihofu chochote.

“Sisi viongozi tunapogundua ama kuhisi uwepo wa mfanyakazi yeyote anayezembea katika idara yake, tumekuwa tukichukua hatua kali dhidi ya watu kama hao kwa ajili ya usalama wa kampuni na kulinda heshima ya nchi,” amesema Mutebi.

Mutebi ameliambia JAMHURI, mpaka sasa kuna wafanyakazi zaidi ya watano ambao kampuni imeamua kuwasimamisha kazi baada ya kubainika kutenda makosa mbalimbali na uchunguzi unaendelea dhidi yao. Wakibainika kuwa na matatizo hatua za kinidhamu zitachukuliwa.

Akizungumza na JAMHURI, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, ameshangazwa na taarifa hizo na kusema kuwa atafuatilia kwa kina na atakayebainika kuhusika atachukuliwa hatua za kisheria.

“Kwa sasa niko Zanzibar, na Jumatatu (jana) ninaanza ziara ya kutembelea viwanja vya ndege kwa lengo hilo hilo la kupamba na hii biashara haramu, hivyo tunaomba ushirikiano wenu katika mapambano haya,” amesema Masauni.

Wakati huo huo, Februari 2, mwaka huu, Lilian Bernard Martin na Bakari Kari Bakari walikamatwa jijini Mombasa, nchini Kenya, kwa tuhuma za kukutwa na kilo 15 za dawa za kulevya aina ya ‘heroin’ na pesa taslimu Sh milion 18 za Kenya na kufikishwa katika Mahakama ya Shanzu katika Kaunti ya Mombasa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Diana Muchachi.

Lilian na ambaye ni raia wa Tanzania na mkazi wa Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam, aliondoka nchini Februari 26 mwaka huu kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kuelekea Kenya ikiwa ni mara yake ya pili katika kipindi cha miezi miwili.

Lilian na Bakari walikamatwa katika hoteli ambayo walikuwa wamefikia siku moja baada ya kufika Mombasa. 

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga, amesema kuna wakati wafanyabiashara wa dawa za kulevya walikuwa wakisafirisha dawa hizo kupitia DHL.

“Kuna wakati walikuwa wanasafirisha through DHL, inawezekana kabisa kufanya hivyo kwani yupo raia wa Nigeria alikuwa akitumia mbinu hizo, lakini alishaondolewa nchini na haruhusiwi kuingia tena nchini kwetu. Ila nitafuatilia kwa karibu taarifa hizo,” amesema Sianga.

Tangu Januari mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alipoanzisha vita dhidi ya dawa za kulevya, watuhumiwa zaidi ya 1,000 wametiwa mbaroni na kufunguliwa mashtaka kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Mmoja wa watuhumiwa wa kilimo cha bangi, amefariki dunia akiwa mahakamani mjibu Bukoba baada ya kutuhumiwa kukutwa na bangi kinyume cha sheria.

By Jamhuri