Unyama polisi

*Mahabusu aliyejifungulia polisi hatimaye azungumza

*Polisi wawa ‘miungu-watu’, wananchi wakosa mtetezi

*Mbunge afichua rushwa, unyanyasaji, kubambikia kesi

 

KILOMBERO,

NA CLEMENT MAGEMBE

“Mungu ndiye kimbilio hatuna tena mwingine”, haya ndiyo maneno yaliyoandikwa kwenye kanga iliyotumiwa na mahabusu Amina Mbunda (27), aliyetelekezwa akiwa na uchungu na hatimaye kujifungua bila msaada nje ya Kituo cha Polisi Mangula mkoani Morogoro.

Mtoto aliyezaliwa amepewa jina la Swaumu, likiendana na tukio la Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Ni tukio lililomfanya Amina asiisahau Juni mosi, mwaka huu kwa kuwa ni siku ambayo kwa nchi iliyo huru, anasema hakutarajia kuona polisi wakimtendea kama vile alikuwa Afrika Kusini ya zama zile za ukatili wa makaburu.

Ni tukio ambalo sasa limewaamsha wananchi wa Mang’ula na pande zote za nchi wapaaze sauti kulaani matukio ya utesaji yanayodaiwa kufanywa na baadhi ya polisi wa Kituo cha Mang’ula.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mang’ula kilichopo Kilombero mkoani Morogoro, Iddi Masumira (Makambale), amefanya mahojiano maalumu na JAMHURI na bila kusita anasema unyanyasaji unaofanywa na polisi dhidi ya wananchi sasa umevuka mipaka.

Hata Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali, anaungana na Masumira, akisema hata kwa tukio la Amina kuteswa hadi kujifungulia kwenye majani bila msaada wowote, sasa polisi wamejipanga kutochukua hatua zozote za kinidhamu kwa waliohusika na udhalimu huo.

 

AMINA ALIVYOKAMATWA

 

Mwenyekiti Masumira anaeleza kwamba Mei 31, mwaka huu, saa 11 jioni akiwa anacheza drafti katika Kitongoji cha Ilovo alifuatwa na polisi Andrew Mapunda wa Kituo cha Mang’ula na kumweleza kuwa polisi wanataka kufanya upekuzi nyumbani kwa Abdallah Mrisho.

“Alikuwa na fomu ya upekuzi iliyoandikwa Mei 31, mwaka huu wakidai kuwa kuna mali za wizi zilizoibwa kutoka kwa fundi seremala ajulikanaye kwa jina la Mdei anayefanyia shughuli zake katika Kitongoji cha Posta, Mang’ula.

“Walidai kuwa Mdei aliibiwa kochi, kitanda na meza ndogo na kwamba Mrisho amenunua kitanda kilichokuwa kimeibwa kwake, taarifa hiyo wameipata kutoka kwa mtuhumiwa aliyefahamika kwa jina la Ridhiwan.

“Baada ya maelezo hayo niliwaeleza kwamba iliwapasa kuwasiliana na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ilovo, Costantine Mkude, lakini wakajibu kuwa wamemtafuta bila mafanikio na hata kwenye simu yake ya kiganjani haipatikani.

“Tukaondoka na askari huyo aliyekuwa ameongozana na mgambo Tyson Mkondya na Mdei [mlalamikaji] na tulipofika nyumbani kwa Mrisho tukawakuta wanawake watatu nje wakiwa wamekaa na wote hao ni wapangaji wa nyumba ya mwanamke mmoja – Asha.

“Nikauliza Mrisho yupo? Nikajibiwa na mmoja wao kuwa Mrisho hayupo. Aliyejibu ni mke wake [Amina]. Polisi tuliyekuwa naye akasema Mrisho amenunua kitanda cha wizi, lakini akajibiwa na Amina kuwa kitanda walichonacho walikinunua muda mrefu sana.

“Anayedai kaibiwa akaonyesha picha ya kitanda chake aliyokuwa ameipiga kupitia simu yake ya kiganjani muda mfupi baada ya kukitengeneza, lakini Amina akasema hakilingani na kitanda chao ambacho kimetengezwa kwa mbao na vyuma.

“Amina akasema utofauti wa picha hiyo waliyoonyeshwa na kitanda chao ni mkubwa, isipokuwa ubao wa mbele (shoo) unafanana na kitanda ambacho walikinunua muda mrefu kwa fundi seremala ambaye hakumtaja jina.

“Baada ya maelezo hayo alitukaribisha ndani ili tujiridhishe kwa kukiona kitanda hicho, ndipo Mdei akasema shoo ya mbele ya kitanda ni mali yake na vingine havimhusu. Polisi (Andrew) akamwagiza mlalamikaji huyo aende kwa fundi baiskeli jirani na nyumba hiyo anayefamika kwa jina la Ndengamo kuazima spana ili afungue sehemu hiyo ya kitanda. Akafungua kitanda hicho na kuitoa nje ili shoo ya mbele anayodai kuwa ni mali yake, ndipo askari huyo akaandika kwenye fomu ya upekuzi aliyokuwa amekuja nayo kuwa mali ya wizi (ubao wa mbele wa kitanda) imepatikana.

“Akanipa fomu hiyo niisome kama Mwenyekiti wa Kijiji niliyekuwa nimeambatana nao, na baada ya kumaliza kuisoma tukasaini wote wanne tuliokuwa tumekwenda kwa Mrisho kufanya huo upekuzi isipokuwa mke wa Mrisho [Amina] hakusaini kwa madai kuwa yeye hajui kusoma,” anasema Masumira.

 

ASKARI ALIVYOMCHUKUA AMINA

 

Masumira anaendelea kusema, “Akamwambia kwa sababu mumeo hayupo unapaswa ujiandae twende kituo cha polisi. Mimi kwa nafasi yangu ya uongozi baada ya kuona hali ilivyokuwa ya mwanamke huyo nilimweleza askari kwamba asimpeleke mahabusu mama huyo na badala yake amsubiri mume wake atakuja kituoni hapo. Nilifanya jitihada za kumpigia simu Mrisho na kuiweka kwenye spika ili kila mmoja asikilize tulichokuwa tunazungumza naye. Nikamweleza kuwa nyumbani kwako imepatikana mali ya wizi na kwamba mkeo anapelekwa katika kituo cha polisi.

“Akajibu, ‘mwambie huyo askari polisi amwache huyo mwanamke, mimi niko kijiji cha jirani cha Mang’ula ‘B’ nakuja, pia kitanda hicho ni mali yetu na tulinunua kihalali’ pia polisi aliposikia maelezo hayo akasema, ‘mimi siwezi kumwacha mtu’. Polisi Andrew akasema mumewe akija kituoni watabadilishana na mkewe na kwamba hata kama ni mjamzito atakwenda na anachofuata ni sheria.

Mwenyekiti Masumira anasema alimshauri polisi huyo kwamba huyo mjamzito aachwe kwa kuwa hali yake si nzuri, lakini alikataa kusikiliza na pia hata mama huyo alipojieleza kuwa yeye ni mdhaifu – hawezi kwenda kituoni, akamwambia, “Nitakuchukua kwa nguvu”.

“Kutokana na kauli hiyo ya askari polisi nikamshauri kuwa aende huko kituoni ili atakapokuja mumewe aende huko. Pia niliwashauri kuwa wasimbebeshe mzigo huo huyo mwanamke na hilo likasikilizwa, akabeba mlalamikaji. Ilipofika saa 9 usiku, Juni 1, mwaka huu nilipigiwa simu na Melinda Mbwagaye ambaye ni askari mgambo kuwa amepigiwa simu na polisi Andrew Mapunda kuwa Amina amejifungua mtoto katika Kituo cha Polisi Mang’ula alikokuwa amewekwa mahabusu.

“Niliuliza, ‘kajifungua mtoto gani?’ Akanijibu kuwa hata polisi wenyewe bado hawajafahamu amejifungua mtoto gani. Nikamshukuru kwa taarifa hiyo. Nikafuatilia katika Kituo cha Afya Mang’ula nilikoelezwa kuwa amepelekwa kwa matibabu ambako nilielezwa kuwa ameruhusiwa kwenda nyumbani siku hiyo hiyo saa 5 asubuhi.

“Mume wake hakwenda kituoni hapo hadi Juni 3, mwaka huu walipofika RPC [Mkuu wa Polisi wa Mkoa] na OCD [Mkuu wa Polisi wa Wilaya] na kuondoka naye kwa ajili ya mahojiano na muda mfupi alirudi nyumbani.

“Pamoja na tuhuma hizo bado wahusika wanaendelea na kazi zao licha ya kuelezwa kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo lililovuta hisia za watu.

“Kwa muda mrefu tunaelewa kuwa huyu Andrew na Mrisho kuwa ni marafiki hapa kijijini na hatuelewi kwa nini amefanya hivi,” anasema Masumira.

 

UBAMBIKAJI KESI

Mwenyekiti huyo anasema polisi wa kituo hicho wamekuwa na tabia ya kuwabambika kesi wananchi na kuwatoza rushwa ikiwa ni ‘mradi waliouanzisha’ na kuwa kero kubwa kwa wananchi.

Anasema mwaka jana alipewa taarifa ya tukio la kifo cha mwananchi wa kijiji hicho aliyefia shambani kwa Kijiko. Anasema aliwapigia simu polisi wa Kituo cha Mang’ula.

“Mtu aliyekuwa amefariki pembezoni alipokuwa amelala kulikuwa na baiskeli ambayo baadaye ilielezwa kuwa ilikuwa ni mali yake, ikaibwa. Hivyo nikawatangazia wananchi kuwa aliyehusika na wizi wa baiskeli hiyo airudishe. Baiskeli hiyo ikarudishwa eneo hilo hilo na polisi wakapewa taarifa kuwa baiskeli imerudishwa. Wakataka niwapelekee kwa madai kuwa hawakuwa na usafiri, na nilipowapelekea wakaipokea, lakini baada ya siku tatu wakaniita tena kituoni hapo.

“Nilipofika nikawekwa mahabusu kwa madai kuwa mimi na watu wengine watano tunahusika na kifo cha huyo mtu, hivyo tukatakiwa kila mmoja kulipa Sh 100,000 kwa kuwa gari la OCD halina mafuta, wote tukauza mpunga na kulipa kiasi hicho cha fedha.

 

AMINA AELEZA ALIVYOJIFUNGUA

 

JAMHURI limefika kijijini Mangula na kuzungumza na watu mbalimbali, akiwamo Amina aliyejifungua mtoto kwenye majani nje ya kituo cha polisi.

Amina anasema Alhamisi, Mei 31, mwaka huu saa saba mchana alifika nyumbani kwake mgambo aliyejitambulisha kwa jina la Waziri na kumweleza kuwa mumewe anatakiwa polisi.

“Saa 11 jioni akaja polisi Andrew, mgambo, mwenyekiti na mlalamikaji (Mdei) wakimwulizia mume wangu kama yupo. Na nilipowaeleza kuwa hayupo wakanieleza kuwa wamekuja kufanya upekuzi kwa kuwa kuna kitanda cha wizi tulichokuwa tumekinunua.

“Nikawauliza, ‘ni kitanda gani kilichoibwa?’ Wakanionesha picha ya kitanda ambacho hakifanani na hiki tulichokuwa nacho na wao walisema havifanani. Ndipo Andrew akaniambia lazima niende kituo cha polisi.

“Nilimweleza kuwa mimi ni mgonjwa, lakini akakataa kabisa akasema nitakwenda kwa lazima. Saa 12 jioni nikawekwa mahabusu, akaja Mkuu wa Kituo akauliza kwa nini nimewekwa mahabusu huku ujauzito wangu ni mkubwa? Je, nikizalia kituoni itakuwaje? Akanipa pole na kuondoka muda wa saa 2 usiku.

“Baadaye kidogo akaja askari aliyekuwa zamu (Selemani) akaniuliza, ‘vipi?’ Nikamweleza kuwa hali yangu siyo nzuri, akaniambia vumilia tu hadi kesho ndugu zako watakapokuja kukuwekea dhamana,” anasema.

Saa sita usiku Amina akaita tena kuomba msaada na akaeleza kuwa tayari maji (ya uchungu) yameshaanza kumwagika na anadhani kuwa atajifungua muda si mrefu, akaomba asaidiwe kukimbizwa kituo cha afya. Koplo Selemani akaanza kuwapigia simu askari wenzake kuwaomba ushauri ambao ulichukua saa mbili bila majibu.

Saa nane usiku Amina anasema akaomba tena msaada akiwa taabani, akamweleza askari wa zamu kuwa ni kweli anajifungua na atajifungulia hapo na akamuomba awaite wanawake walioko karibu wamsaidie ajifungue hapo mahabusu. Kuona hivyo, Koplo Selemani akawapigia tena simu wenzake na wakakubaliana kuwa amtoe Amina nje ya mahabusu na waone cha kufanya.

“Askari [Selemani] alikuwa anakuja mara kwa mara kuniangalia ndani ya chumba cha mahabusu kituoni humo. Alikuja kuniona mara nne, akaniangalia na kunitaka nilale. Baadaye ilipofika saa 9 usiku naye alikuwa amelala, uchungu ulikuwa umezidi sana na dalili za kujifungua zilikuwa wazi.

“Nikagonga mlango wa chumba cha mahabusu ili kumwamsha anisaidie, akaniambia nivumilie hadi mwisho na muda mfupi akaanza kuwapigia simu askari wenzake waliokuwa wamelala majumbani.

“Ilipofika saa 9:30 usiku akatafuta bodaboda ili nikimbizwe katika kituo cha afya, lakini hata alipofika, nilishindwa kupanda na kuanza kujifungua, mtoto akaangukia kwenye majani pembezoni mwa kituo hicho ambako kuna majani na uchafu mwingi,” anasema Amina.

Sehemu hiyo ambayo alijifungulia iko jirani na polisi na machinjio ya Mang’ula.

Anasema askari polisi wa zamu, Koplo Selemani hakusogea eneo hilo, alikaa mbali akisubiri aitwe na kila mara alikuwa akimuuliza [Amina], “Tayari mtoto ametoka salama?”

Amina akajifungua mwenyewe, mtoto akadondoka chini kwenye nyasi zilizochanganyikana na mchanga na yeye akapoteza fahamu.

Inaelezwa kwamba Koplo Selemani akaenda nyumbani wa Sajenti wa Polisi aitwaye Aron, akamgongea Aron na mke wake na akaomba mke wa Sajenti Aron atoke kwenda kumsitiri Amina na mwanaye mchanga. Mke wa Sajenti Aron akakataa.

Koplo Selemani akaenda kwa mfanyakazi wa TAZARA iliyeko jirani na Kituo cha Polisi Mang’ula upande wa Mawasiliano nyumbani kwa Fredrick Kipangule. Mke wa Kipangule anayeitwa Emeta Nyenza akakubali kuamka na kanga zake akaenda kumsitiri Amina na kichanga.

Inaelezwa kuwa Emeta alipofika pale akakuka Amina anapata fahamu kwa mbali, yuko mtupu, na kile kitoto kichanga kiko chini kwenye nyasi na mchanga kikipigwa baridi, ndipo akawasitiri wote wawili na kisha wakapelekwa zahanati iitwayo Mama Tuli kwa kutumia bodaboda.

Hapo zahanati wakapewa huduma ya kwanza na kukatwa kitovu na kisha wakapelekwa Kituo cha Afya Mang’úla saa 11 alfajiri kwa kutumia bodaboda. Hapo kituoni walihudumiwa na Dk. Msomba. Amina anasema aliruhusiwa kurejea nyumbani Juni 3, mwaka huu.

Amina alionyesha JAMHURI mahali alipojifungulia, na punde akajawa hisia na kuanza kulia kwa uchungu.

 

Mama mzazi wa Amina azungumza

Fatuma Fundi ambaye ni mama mzazi wa Amina amesema tukio hilo ni kero kubwa, na hawezi kulisahau maishani. Anaiomba Serikali ichukue hatua dhidi ya wahusika.

Fatuma ambaye ni mjane na mkazi wa Shamba Kaloleni katika Kijiji cha Mwelule, Kata ya Mwaya, anasema Amina ndiye mtoto wake wa kwanza; na kitendo cha polisi kumkamata bila kosa ni nia chafu waliyokuwanayo ya udhalilishaji.

“Nimeumia sana baada ya kusikia taarifa ya uongo iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro kuwa alijifungua akiwa njiani wakati anapelekwa katika Kituo cha Afya Mang’ula,” anasema mama huyo.

 

ABDALLAH MRISHO ANENA

 

Mume wa Amina, Abdallah Mrisho, anasema aliitwa polisi baada mkewe kutoka kituo cha afya alikokuwa anapatiwa matibabu baada ya kujifungulia kwenye majani.

Anasema aliandika maelezo polisi na kuelezwa arejee nyumbani kwa kuwa tukio hilo ni la “kawaida”, hivyo atulie.

Mrisho anaeleza kuhusu kitanda, na kusema alikinunua Aprili, mwaka huu kwa seremala Ridhiwan aliyekuwa akiuza vitanda alivyoweka nje ya karakana yake.

“Nasikitika sana kwa ukatili huu uliofanywa kwa makusudi na polisi hawa, sasa tunalala chini na mke wangu baada ya kuchukuliwa sehemu ya kitanda hicho,” analalamika.

 

ASKARI ANAYETUHUMIWA

 

JAMHURI limemtafuta na kumpaya polisi aliyemkamata Amina, lakini amekataa kueleza chochote kwa madai kuwa suala hilo wenye mamlaka ya kulielezea ni viongozi wa ngazi za juu wa Polisi.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, ACP Barnabas Mwakalukwa, anasema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa liko kwenye mihimili miwili tofauti yaani Bunge ambalo linataka uchunguzi ufanyike; na Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Spika Job Ndugai ameelekeza Kamati ya Bunge ya masuala ya Ulinzi na Usalama imhoji Amina ili kupata ukweli juu ya madai hayo.

 

KAULI YA MBUNGE WA KILOMBERO

Mbunge wa Kilombero, Lijualikali amezungumza na JAMHURI na kusema, “Ni kweli kabisa yule mama jana [Juni 15, mwaka huu] tumekula naye chakula. Wakati nilipokuwa naongea nao vizuri kuna kitu waliniambia sijui walikuwa hawajakisema.

“Waliniambia shida kubwa si wizi wa kitanda, kulikuwa na ugomvi mwingine wa fedha kati ya yule askari ambaye alimfuata yule dada mjamzito.

“Kwamba yule mume wa yule dada mjamzito alikuwa na mdogo wake kwa maana mtoto wa dada yake alikuwa anafanya kazi na mtu, akasababisha hasara, akawa anadaiwa Sh milioni moja.

“Alipelekwa kituo cha polisi wakafika mwafaka na huyo mtu anayemdai mdogo wake kwa maana ya mume wa Amina.

“Askari aliyesimamia hilo zoezi [kazi] ni huyo Andrew, sasa akawa anadai kupewa fedha baada ya huo mwafaka. Baba wa mtuhumiwa akasema yeye hela hana, naye Andrew akamhakikishia kwamba atamfanyia kitu ambacho yeye hatoamini, sasa siku hiyo likawa limetokea suala la kitanda, yule Andrew akaenda kumchukua huyo mwanamke makusudi kabisa.

“Mume wa huyo mwanamke akawa amempigia simu Andrew akimsihi kumwachia mke wake kwani yeye atajileta mwenyewe kituoni. Andrew akamjibu kuwa lazima amchukue mke wake ili amkomeshe kwa sababu anajifanya mjanja sana.

“Kwa hiyo hoja kubwa ni visasi, siyo tena utuhumiwa, kwa hiyo kuna hivi vitu vya kubambikiwa bambikiwa. Huyu Andrew niliambiwa ana ndugu yake yupo sijui (anataja ofisi kubwa ya Serikali), lakini sasa cha ajabu huyu Andrew ni mzaliwa wa hapo hapo Mang’ula na amesoma huko huko yaani ni kwao kabisa.

“Nasikia hata askari wenzake waliopo kituoni wanamwogopa kwa sababu hiyo, nimeshindwa kuelewa inakuwaje afanye kazi kwao aliposomea na hapo hapo ndipo alipokulia. Kwa hiyo kama kuna nguvu basi ndio hiyo.

“Kingine ambacho watu hawakijui baada ya tukio hilo walimfuata huyo mama ili wampe hela akakataa, walimfuata kumhonga ili anyamaze akawakatalia.

“Kuhusu RPC kusema kwamba huyo mama hakujifungulia kituo cha polisi ni uongo, ukimtafuta Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani (Masauni) yeye ameongea vizuri kabisa kwamba yule mama amejifungulia nje ya kituo wakati wakiwa kwenye pilika pilika akiwa mahabusu ndipo walimtoa akajifungulia nje.  Na huo ndio uhalisi.

“Sasa baada ya kauli ya Naibu Waziri ndipo Kaimu RPC, naye akatoa kauli kwamba huyo mama alijifungulia kituo cha afya, na eti alipewa bodaboda ilimpeleka hadi kituo cha afya kujifungua.

“Mimi nimeongea na yule mwanaume aliyemruhusu mke wake akamsaidie yule mama, anaongea ukweli kabisa kwamba mke wake alimkuta huyo Amina akiwa nje ya kituo cha polisi, akiwa hajitambui na hiyo ni baada ya kama dakika 40 baada ya kuwa ameshajifungua.

“Sasa wanachokifanya hawa askari wa kituo ni kwenda kwa huyo mama aliyemsaidia kumdanganya danganya na kumtishatisha ili asiseme huo ukweli wakati jamii yote ya pale haitishiki tena kwani inaujua ukweli.

“Mimi binafsi nimefikiria nataka kuhamishia makazi yangu hapo Mang’ula ili nifanye kazi ya kuchunguza mambo kama hayo, kwani nimeambiwa kuna kesi nyingi za watoto wa kike kupata mimba, lakini zikifikishwa kituoni zinaishia juu kwa juu.

“Yaani kuna ka-kikundi pale kamekaa kwa ajili ya kupanga na kutenda haya mambo, shida watu wengi wa huko wanaogopa kusema kwa sababu wanahisi wakisema watafanyiwa vibaya.

“Askari waliopo kituoni hapo wamekaa muda mrefu hawahamishwi na hata wakihama wanarudishwa tena na ki-eneo hiki kina watu wengi sana kwa hiyo askari wanakuwa wanajinufaisha kutokana na uhalifu unaotokea katika eneo hilo, ndio maana kesi haziishi,” anasema Lijualikali.

 

MWISHO.

 SOMA GAZETI LOTE LA JAMHURI HAPA

1429 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!