*Mataifa yanayochimba mafuta yapuuza maagizo ya Marekani

RIYADH

Saud Arabia

Leo ni siku ya 40 tangu Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alipotangaza na kuanzisha kile anachokiita ‘Operesheni ya Kijeshi’ nchini Ukraine; huku jumuiya ya kimataifa ikikitafsiri kama ni uvamizi wa kijeshi.

Ndani ya siku 40 dunia sasa imeanza kutambua nguvu ya Urusi katika uchumi, ambapo mataifa kadhaa yameonekana kupuuza ‘maelekezo’ yanayotolewa na utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani.

Wakati uchumi wa Ulaya unaotegemea gesi na chakula kinachozalishwa Urusi na Ukraine ukitikisika na bei ya nishati ya mafuta ikipanda kwa kasi, mataifa wanachama wa OPEC+, jumuiya ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani, yameahidi kuendelea na utaratibu wa kawaida wa uzalishaji mafuta, na kuongeza uzalisha ifikapo Mei mwaka huu kufidia pengo lililopo.

Biden anataka uzalishaji wa mafuta uongezeke mara moja kufidia kiwango kilichokuwa kikizalishwa na Urusi ambayo imewekewa vikwazo vya kiuchumi; wito ambao sasa unapingwa.

Urusi ni mzalishaji mkubwa wa nishati ya mafuta duniani na kwa mafuta yake kutoingia kwenye soko la dunia, kumesababisha upungufu wa mapipa milioni 12.

Takwimu zinaonyesha kuwapo kwa upungufu wa idadi hiyo ya mapipa ya mafuta duniani kila siku; Marekani ikiahidi kutoa mapipa milioni moja kufidia upungufu uliopo, kiasi ambacho hakitoshi mahitaji. 

Mawaziri wa mafuta wa mataifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Saudi Arabia; wanachama waandamizi wa OPEC+, katika mkutano wao wa Dubai wiki iliyopita, wamesema hawatajihusisha na ‘siasa’ zinazoendelea duniani, pamoja na shinikizo wanalopata wakitakiwa kuitenga Urusi ambayo pia ni mwanachama mwenzao.

Alipoulizwa iwapo wanadhani kuwa wanawajibika kimaadili kuiondoa Urusi kwenye OPEC+, Waziri wa Mafuta wa Saudi, Abdulaziz bin Salman, amesema: “Tukiingia kwenye vikao vyetu kila mmoja anayaacha mlangoni masuala ya kisiasa.

“Kama tusingekuwa tunafanya hivyo isingewezekana kufanya biashara na nchi nyingi namna hii duniani katika vipindi tofauti. La sivyo kuna wakati tungelazimika kuwaondoa Iraq, na wakati mwingine tungewaondoa Iran.”

OPEC+ imekuwa katika shinikizo kubwa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24, mwaka huu; wakitakiwa kuongeza uzalishaji.

Mwanamfalme Abdulaziz na waziri mwenzake wa UAE, Suhail al-Mazrouei, wamesema wanacholenga ni kuweka ulinganifu katika soko la mafuta ghafi na kuwaridhisha wateja.

“Lengo letu ni moja tu; kurekebisha hali ya soko la mafuta. Kwa hiyo hatutaki kuingizwa kwenye siasa… tunataka soko liwe shwari,” amesema Mazrouei na kuongeza:

“Kama tutamwondoa mmoja wetu, maana yake tunaongeza bei, kitu ambacho wateja hawatakipenda.”

Mataifa ya Ghuba, marafiki wa Marekani, ni wanachama wa OPEC+, umoja unaojumuisha pia wanachama wa OPEC na wazalishaji wakubwa wa mafuta kama Urusi na Mexico. Abdulaziz amesema Urusi inazalisha asilimia 10 ya mafuta yayotumika duniani.

By Jamhuri