Suala la usalama ndani na nje ya viwanja vya soka limebaki kuwa tishio kwa wachezaji na watazamaji wa mchezo huo, hali inayoendelea kupunguza idadi ya watu wanaokwenda kutazama mechi, barani Afrika.

Mara nyingi ajali katika viwanja zimekuwa zikisababishwa na uzembe wa baadhi ya watendaji waliokabidhiwa majukumu ya kusimamia mchezo, hali inayowaweka wachezaji na watazamaji katika hatari.

Katika mwendelezo wa ajali ndani na nje ya viwanja, inakadiriwa watu wapatao 17 wamekufa nchini Angola wiki iliyopita wakati wa mchezo kati ya Santa Rita de Casia dhidi ya Reactrativo de Libolo.

Taarifa iliyotolewa na vyombo vya usalama nchini humo, imesema watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni akina mama na watoto, wengine 56 wakibaki majeruhi wanaoendelea kutibiwa.

Tukio la Angola linakuja ikiwa imepita miaka 16 tangu mashabiki wapatao 127  wa soka nchini Ghana walipopoteza maisha mwaka 2001 katika uwanja wa Accra Sport.

Maafa hayo yalitokea wakati wa pambano kati ya mahasimu wawili wa soka nchini humo – Hearts of Oak dhidi ya Asante Kotoko. Katika mchezo huo, takribani mashabiki 127 walipoteza maisha.

Miaka 9 baada ya tukio la Ghana, tukio jingine lilitokea nchini Ivory Coast katika mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia uliopigwa Stade Felix Houfuete Boigne kati ya wenyeji Ivory Coast dhidi ya Malawi. Katika tukio hilo mashabiki 19 walifariki dunia.

Miaka 16 iliyopita nchini Afrika Kusini kwenye Soweto Derby kati ya Kaizer Chiefs na Orlando Pirates, mashabiki 43 walifariki dunia kutokana na uwanja kujaza mashabiki 30,000 tofauti na idadi inayotakiwa ya watu 20,000.

Ajali nyingi katika soka hapa Afrika mara nyingi hutokana na   uzembe wa mashabiki wenyewe, vyombo vya usalama au vyama vya soka kushindwa kuweka mikakati ya kuzuia ajali.

Kwa hapa Tanzania, kumekuwa na ajali zinazotokea ndani au nje ya viwanja na kusababisha wachezaji kupoteza maisha. Kwa mfano, tukio la kufariki uwanjani kwa mshambuliaji wa timu ya vijana ya Mbao FC, Ismail Khalfan, Desemba 4, 2016  bado limeendelea kuacha maswali mengi juu ya usalama katika viwanja vya soka.

Ripoti iliyotolewa na Hospitali ya Mkoa wa Kagera kuhusiana na kifo cha mchezaji huyo, ilionesha kuwa alifariki kutokana na kusimama ghafla kwa moyo (sudden cardiac arrest).

Baada ya uchunguzi, ilibainika kuwa mchezaji huyo hakuwa na jeraha lolote ila kifo chake kilitokana na kusimama ghafla kwa moyo kutokana na kukosekana kwa huduma ya kwanza uwanjani.

Mchezaji huyo alitakiwa kupatiwa huduma ya kwanza ya electrical shock, kitendo ambacho kilitakiwa kufanyika ndani ya sekunde chache, kwa lengo la kuushitua moyo kurudi katika hali yake.

Kitaalamu kawaida moyo una mfumo wa umeme (heart electrical system), ambao unadhibiti mapigo ya moyo, mfumo huu ukisimama basi moyo unashindwa kusukuma damu sehemu muhimu kama vile kwenye ubongo na ogani kuu.

Ukosefu wa vifaa tiba katika viwanja vyetu kama huduma ya kwanza, gari la wagonjwa, umekuwa kama wimbo wa Taifa kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kushindwa kuwa na vifaa hivyo, na pale mchezaji anapopata tatizo anashindwa kupata huduma.

Tumeshuhudia pia mchezaji wa Stand United, Chidiebele, akiumia uwanjani na kuvunjika taya lakini hakukuwa na huduma ya uhakika, achilia mbali wachezaji wengi wanaopata madhara bila ya uhakika wa huduma katika viwanja vingi mikoani.

1062 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!