Nilipotoa makala yangu iliyokuwa inasema ‘Tujifunze kupendana na siyo kuumizana’, katika gazeti la JAMHURI linalotolewa nchini, Tanzania na kuchapishwa na Jamhuri Media, Toleo No. 249, ISSN Na 1821-8156, Julai 5-11, 2016, mwanandoa mmoja ambaye kwa sababu maalumu sitaweza kulitaja jina lake, alinitumia ujumbe mfupi kwa njia ya simu ya kiganjani. 

Ujumbe huo ulikuwa unasomeka hivi, “Nimeumizwa!, Nimeumizwa!, Na tena nimeumizwa! William siwezi kusamehe! Labda nitasamehe nikiwa kaburini” mwisho wa kunukuu. 

Makala ya leo nitazungumzia msamaha. Abraham Lincoln, Rais wa 16 wa Marekani, anatupa uwezekano wa kuishi msamaha na upatanisho. Wakati akifanya kampeni, alitokea mpinzani aliyefanya kila aina ya mbinu ili kuharibu jina na sifa yake. Huyu aliitwa Edwin McMasters Stanton.

Alikuwa tayari kufanya lolote ili Lincoln asipate nafasi ya kushinda uchaguzi wa urais. Hata hivyo, Lincoln alishinda na alipokuwa anaandaa baraza la mawaziri, jina la Stanton likawapo. Wasaidizi wa rais walifanya juhudi kubwa ila bila mafanikio kumweleza rais chuki aliyokuwa nayo Stanton dhidi yake. 

Hata hivyo, rais alionekana kuzijua wazi mbinu mbaya za Stanton dhidi yake wakati wa kampeni. Rais akasema huyu ananichukia mimi ila siyo Marekani. Huyu ana sifa za kuiongoza Marekani na watu wake. Akamfanya waziri wa ulinzi. Stanton aliposikia uteuzi wake alishangaa mshangao mkubwa. 

Akakubali ule wadhifa na akaifanya hiyo kazi kwa weledi mkubwa. Lincoln aliuawa. Wakati wa maziko yake, Stanton alisema, ‘Hakika huyu asingeondoa chuki yake dhidi yangu, leo hii angezikwa huku akiacha adui duniani, lakini kwa vile roho yake ilikuwa tofauti na yangu ameacha rafiki duniani.’

Tujiulize; kuna faida yoyote anayopata mtu baada ya kukataa kusamehe? Kuna faida yoyote anayopata mtu baada ya kukataa kupokea msamaha? Msamaha ungekuwa unauzwa tungeweza kuununua. Lakini kwa bahati nzuri hauuzwi. Haupatikani mahali popote isipokuwa ndani moyo wako. Jaribu tu kujiuliza, kwa nini nashindwa kusamehe? Msamaha ni zawadi, hebu jaribu kumpa mwenzako zawadi hii. 

Sharti la kusamehewa ni kusamehe. Kila mwanadamu anahitaji kuwa na furaha na amani katika maisha yake. Hakuna mwanadamu anayetamani kuwa na huzuni muda wote. Hakuna mwanadamu anayependa kuwa na msongo wa mawazo muda wote. Lakini unaweza kujiuliza maswali kadhaa, kwa nini tunakutana na watu ambao maisha yao ni kujilaumu na kuwalaumu wengine? Kwa nini tunakutana na wanadamu ambao wamejikatia tamaa ya kuishi hapa duniani?

Sikiliza Oscar Wilde anavyosema; ‘Hakuna mwanadamu aliyeshindwa kusamehe halafu akawa na maisha mazuri.’ Oscar anajaribu kuonesha umhimu wa msamaha. Mwandishi mmoja aliwahi kuandika hivi, ‘tunakuwa kama wanyama tunapoua, tunakuwa kama binadamu tunapohukumu, tunakuwa kama Mungu tunaposamehe’. 

Katika Biblia Takatifu imeandikwa; “Utusamehe makosa yetu, kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea” (Mt. 6:12). Katika andiko hilo ukweli unabaki kuwa ili tusamehewe ni lazima na sisi tuwasamehe waliotukosea. Msamehe mume wako, msamehe mke wako, wasamehe watoto wako, msamehe jirani yako, msamehe mwajiri wako, msamehe mfanyakazi wako na jisamehe wewe mwenyewe.

Msamaha ni kiungo wa amani katika jamii msamaha ni mlango wa amani katika familia. Msamaha ni mlango wa amani katika urafiki. Samehe, usamehewe. Usipende kusamehewa kama wewe mwenye hupendi kusamehe. Msamaha unatibu majeraha ya chuki. Unatibu majeraha ya ugomvi. Unatibu majeraha ya nafsi. 

Martin Luther J. King Jr, anatoa ushauri unaosema binadamu sharti avumbue njia ya kutatua migogoro ya kibinadamu ambayo inakataa kulipiza kisasi, matumizi ya mabavu na falsafa ya jino kwa jino. Msingi wa njia hiyo ni upendo.

Kama tunahitaji amani ya kweli na ya kudumu ndani ya mioyo yetu na kwa jamii inayotuzunguka, ni lazima tuwe tayari kutoa msamaha na kuupokea. Tuwe waenezaji wa sera ya msamaha. Papa Yohana wa XXIII anatuhimiza kwa nasaha hii, “Wanangu daima tafuteni yale yanayowaunganisha na siyo yale yanayowatenganisha.”  

Msamaha unaunganisha. Ukitaka kuwa na furaha maisha yako yote msamehe kila anayekukwaza. Utaishi kwa amani. Indira Gandhi anasema, “Msamaha ni fadhila ya wenye ujasiri.”

Papa Yohana Paulo II alizaliwa tarehe 18 Mei 1920 na aliaga dunia tarehe 2 April, 2005. Papa Yohana Paulo II alimsamehe Mehmet Ali Agca ambaye alijaribu kumuua tarehe 31 Mei, 1981. Papa Yohana Paulo II baada ya kupata unafuu wa jeraha alienda kukutana na Ali Agca gerezani. Baada ya kukutana na Ali Agca gerezani alisema, “Tuliyozungumza yatabaki siri yangu na yeye. Nilizungumza na Ali Agca kama rafiki yangu ambaye nimemsamehe na ambaye nina imani kamili kwake.” Huu ni mfano bora ambao mimi na wewe tunaweza kujifunza.

Baba wa Taifa la Afrika kusini, Nelson Mandela, alitumikia kifungo cha gereza kwa muda usiopungua miaka 27. Alifungwa, si kwa sababu alikuwa mhalifu, hapana. Alifungwa kwa sababu alikuwa anapigania haki za watu weusi wa taifa lake, alifungwa kwa sababu alikuwa anapigania uhuru wa taifa lake. Alipotoka gerezani alitoa nasaha isiyoweza kusahaulika katika kumbukumbu za kihistoria alisema, “Hakuna aliyezaliwa awe na chuki.”  Akaongeza pia kwa kusema, “Watu wenye ujasiri hawaogopi kusamehe kwa ajili ya amani.”

Kwa msingi huo, anatukumbusha kwamba chanzo cha amani katika jamii ni msamaha. Kumbuka, jirani yako ni yule unayesita kumtakia mema, jirani yako ni yule ambaye hampikiki chungu kimoja, jirani yako ni yule mgonjwa anayehitaji neno lako la kumfariji, jirani yako ni huyo aliyehukumiwa kwa miaka kadhaa baada ya kuwa umemshinda kesi mahakamani, jirani yako ni huyo ambaye unasita kumpa mkono wa amani.

Kardinali, Walter Kasper anasema, Kama hatuna uwezo wa kutangaza kwa njia mpya ujumbe wa huruma ya Mungu kwa watu wanaoteseka aidha kimwili au kiroho, bora tubaki kimya tusiongee kuhusu Mungu. Kila siku Mwenyezi Mungu anatutafuta, anatutafuta tujenge mahusiano mazuri na jirani zetu. 

Hakuna binadamu aliye chini ya jua ambaye ni mkamilifu. Sisi sote tulio chini ya jua si wakamilifu. Tunahitaji neema ya kusamehewa pale tunapokoseana, tusameheane. Msamaha unatufundisha unyenyekevu. Mtu mnyenyekevu anafanikiwa kwa kila jambo analoliwazia.

Unyenyekevu ni jina jingine la msamaha. Kanuni ya kwanza ya kufanikiwa ni unyenyekevu. Ya pili ni unyenyekevu. Ya tatu ni unyenyekevu. Tufanye nini ili tuishi maisha yanayoongozwa na unyenyekevu? Msikilize mwanateolojia wa Kanisa Katoliki, Augustino, wa Hippo anavyosema, “Mungu ni mwenye uwezo wa juu kabisa, jinyenyekeze atakushukia, lakini ukijitukuza atakukimbia.” 

Yule mwovu shetani daima anatamani sana kuharibu picha ya Mungu ndani ya nafsi ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Na picha ya sura hiyo anajaribu kuiharibu kwa njia ya kuwafanya watu kuwa wagumu wa kutoa msamaha pale wanapokesewa kidogo au sana. Kuna wakati inatakiwa utafakari. Unapata faida gani pale unaposhindwa kutoa msamaha kwa aliyekukosea?

Kusamehe waliokukosea kiubinadamu ni jambo gumu sana, lakini ndilo jambo ambalo na sisi linatupatia matumaini ya kusamehewa na Mwenyezi Mungu aliyetuumba kwa sura na mfano wake. Tuepuke dhana ya kuwa na kitabu cha kumbukumbu cha kuandika makosa ya wengine. Kama baadhi ya watu wasingekuwa tayari kuwasamehe wale wanaowakosea, dunia ingegeuka kuwa jehanamu. Ndani ya jamii yoyote hawatakosekana watu ambao wanahasimiana kwa sababu nyingi na tofauti. Lakini tunapokuwa tayari kutoa msamaha kwa wale waliotukosea tunajiponya wenyewe na kuwaponya wale wanaohitaji msamaha wetu. 

Hatuwezi kuishi pasipo kutoa msamaha au kuupokea msamaha. Hatuwezi kabisa. Kumbuka,  msamaha unajenga mahusiano yaliyovunjika. Una kila sababu ya kutoa msamaha, una kila sababu ya kuwa na amani, una kila sababu ya kuwa na uhusiano mzuri na familia yako, una kila sababu ya kuwa mshauri mzuri, hivyo basi kuwa mwepesi wa kutoa msamaha kwa wanaokukosea. 

Anza leo kuomba msamaha kwa Mungu, anza leo kuomba msamaha kwa uliowakosea, anza leo kuwasamehe waliokukosea.  Leo hii utakuwa mwana wa Mungu na mbinguni ndiko kutakakokuwa nyumbani kwako milele yote. Nakusihi wewe ambaye umeumizwa na mzazi wako, msamehe; uliyeumizwa na mtoto wako wa kumzaa,  msamehe; uliyeumizwa na mume wako msamehe, umeumizwa na mke wako, msamehe; umeumizwa na kaka yako au dada yako msamehe, umeumizwa na jirani yako, msamehe.

Kusamehe ni bure. Yawezekana kwa wakati huu mambo yako hayaendi kwa kiwango kinachotakiwa, una mawazo, hupati usingizi, unawaza lakini hupati majibu ya mawazo yako, unahisi umetengwa, unahisi umekataliwa na familia au jamii. Unakuwa mtu wa kunung’unika kwa kila jambo. 

Nakusihi; usitunze chuki moyoni kwa muda mrefu. Ajabu ni kwamba ukiwa na uvundo mwingi wa chuki moyoni mwako unaweza ukaanza kuwaza mawazo ya kujinyonga, kulipiza kisasi, kunywa pombe kupita kiasi ama kunywa sumu. 

Unapokuwa umeshindwa kusamehe usitegemee kupata amani ndani ya roho yako. Chanzo cha kukosa furaha katika maisha ni kutokutoa msamaha kwa waliokukosea.  Familia yako ni familia yako hata kama wamekutenga kwa makusudi. Ukweli unabaki kwamba bado ni familia yako. Usiangalie nyuma, usiangalie ukatili wa nyuma. Angalia mbele. 

Ukiwasamehe wanandugu utamsamehe kila mmoja. Maisha ya kutokusamehe hayana faida. Yana hasara, maumivu, majonzi, huzuni. Kumbuka kwamba, hupati faida yoyote ile unaposhindwa kusamehe waliokukosea, unaposamehe unapata faida. Moyo wako unakuwa na amani, unakuwa mtu wa furaha na upendo, unajikubali ulivyo, unapata utulivu wa ndani, unaondokana na mishituko ya mara kwa mara. 

 

0789 090828 au 0719 700446

By Jamhuri