Mamlaka husika zimetakiwa kuwa makini katika kuhakikisha zinatengeneza mazingira rafiki kwa wasanii wa nyimbo za asili, ambao wapo wachache kutokana na ukosefu wa soko katika burudani hiyo.

Imebainika kuwa baadhi ya wasanii wanaofanya sanaa za utamaduni ikiwamo ngoma, nyimbo za asili na mashairi, wapo katika mazingira magumu ya kiuchumi kwa kuwa kipato chao kinategemea kazi kutoka taasisi mbambali pale wanapokuwa na tukio fulani.

Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi Mtendaji wa Kikundi cha Jivunie Tanzania Sanaa Group, Mariamu Mponda ‘Mama Mipango’, amesema licha ya kupata kazi kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), lakini bado hamasa inahitajika ili kuendeleza utamaduni wetu.

Mtunzi huyo wa mashairi na tenzi, amesema ameanzisha kikundi cha burudani za nyimbo za asili ili kuendeleza sanaa za utamaduni hapa nchini, pamoja na kutoa ajira kwa vijana wenye mwamko na utamaduni.

Amesema licha ya kufanya kazi kwa muda wa zaidi ya miaka 25 ndani ya tasnia sanaa, lakini mafaniko ni kidogo ikilinganishwa na muda aliofanya kazi hizo.

“Hali hii ya uchumi inatokana na nyimbo za asili kukosa hamasa kwa Watanzania, hivyo tunapaswa tuwe na utamaduni wa kupenda vitu vya kwetu ili kuutangaza utamaduni wetu kwa wageni,” amesema Mama Mipango.

Amesema amekuwa akiimba mashairi kwa muda mrefu, huku akibainisha kuwa uimbaji wa mashairi unahitajika umakini pamoja na mpangilio wenye vina pamoja na maudhui, ili kuleta mvuto kwa wasikilizaji.

 JAMHURI: Upo kwenye sanaa zaidi ya miaka 25, una kipi cha kujivunia.

Mama Mipango: Kile ambacho nimekipata ndani ya sanaa ni kufahamiana na watu, ukweli nimefurahi sana kwani inanisaidia kupata fedha kwa ajili ya kuendesha maisha yangu.

JAMHURI: Nini siri ya mafaniko yako?

Mama Mipango: Nina kipaji cha kuimba kwani kipindi cha nyuma nilikuwa nasikiliza radio na kujifunza mwenyewe, pia baadhi ya watu walikuwa wananifundisha ili kuboresha kipaji changu.

 JAMHURI: Jambo gani ambalo huwezi kulisahau katika safari yako ya sanaa?

Mama Mipango: Wakati najifunza kuandika mashairi nilikuwa nahangaika kumtafuta mwalimu wa kunifundisha, kwani watu waliokuwa wanajua kuandika mashairi walikuwa ni wachache tofauti na kipindi hiki.

 JAMHURI: Sasa utamaduni umeonekana upo nyuma tofauti na zamani, tatizo ni nini?

Mama Mipango: Ni kweli kipindi cha nyuma kulikuwa na mwamko mkubwa, kwani Radio Tanzania Dar es Salaam sasa TBC Taifa, ilikuwa na meza ya uchambuzi wa mashairi ambapo nilikuwa napata fursa ya kwenda kuchambua mashairi.

 JAMHURI: Mbali na sanaa, unafanya shughuli gani za kukuingizia kipato?

Mama Mipango: Kazi zetu ni za msimu hasa kipindi cha kampeni za uchaguzi ndiyo tunakuwa tunapata kazi nyingi, hivyo kabla ya msimu wa uchaguzi, ninafanya biashara ndogo ndogo.

Naye Katibu wa Jivunie Tanzania Sanaa Group, Ismail Kambangwa, amesema endapo Serikali haitakuwa makini katika kuendeleza sanaa za utamaduni hapa nchini, kuna uwezakano wa kuipoteza sanaa hiyo ambayo ni muhimu kwa Taifa.

“Tunaweza kukaa mwaka mmoja bila kupata kazi na kusababisha kuwa na mazingira magumu ya kiuchumi kwa vile tunategemea matukio ya taasisi fulani watualike ili tupate posho ya kuendesha maisha yetu,” amesema Kambangwa.

Amesema nguvu ya ziada inahitajika ili kuhakikisha burudani ya asili haipotei kwa sababu tayari kuna viashiria vya kupotea kutokana na idadi ndogo ya wasanii.

Mkurugenzi wa kikundi hicho, Mariamu Mponda ‘Mama Mipango’, ni mkazi wa Mbagala Charambe nje kidogo ya jijini Dar es Salaam. Amezaliwa mwaka 1954 mkoani Lindi na alianza elimu yake ya msingi mwaka 1966 na kumaliza mwaka 1972 katika shule ya Kililima iliyopo wilayani Kilwa.

Mwaka 1984 alijiunga na kazi ya sanaa ya utunzi wa mashairi na tenzi ambayo imemwezesha kumiliki kikundi cha sanaa ya utamaduni ambapo mwaka 2009 kilitambuliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Mama Mipango amefanikiwa kutunga mashairi kadhaa ikiwamo ‘Sanaa ya Kazi’, ‘Kiswahili ndiyo dira’ pamoja na ‘Tunatakiwa kutubu’.

By Jamhuri