Na Bashir Yakub

Tangu Aprili mwaka huu 2018, utaratibu wa
kusajili kampuni umebadilika. Ni tofauti
kabisa na ambavyo tulizoea. Hata hivyo,
yapo mambo ambayo yamebaki vilevile
kama awali, kadhalika yapo mengi pia
yaliyobadilika. Tutapitia utaratibu wa awali
kidogo na huu mpya.

Utaratibu wa awali

a) Ulikuwa unatakiwa kuandika barua
kuuliza jina unalotaka kutumia kama jina la
kampuni iwapo lipo au hapana. Kama lipo
ungetakiwa kuleta jingine, na kama halipo
ulikuwa unapewa ruhusa ya kulitumia katika
usajili.
b) Ulikuwa unatakiwa kuandaa waraka na
katiba ya kampuni (article and

memorandum of association). Zilikuwa
zinatakiwa kwa uchache angalau nakala
nne.
c) Ulikuwa unatakiwa kupakua fomu namba
14(a) na 14(b) kutoka kwenye mtandao wa
BRELA, au kuzifuata fomu hizo hapohapo
BRELA ambapo ungetakiwa kuzijaza kisha
kuzisaini.
d) Kisha ulikuwa unatakiwa kubeba hizo
nakala za waraka na katiba ya kampuni,
pamoja na hizo fomu zilizojazwa na
kuzipeleka BRELA Mnazi Mmoja, jengo la
Ushirika kwa ajili ya usajili.
e) Huko BRELA, baada ya kuzipitia na
kuona hazihitaji masahihisho, sasa
ungepewa ruhusa ya kulipia ambapo malipo
yalikuwa yakifanyika kupitia Benki ya
CRDB.
f) Baada ya hapo ungetakiwa kusubiri
kipindi cha wiki moja au wiki na siku
kadhaa, au wiki mbili ili uweze kupatiwa
cheti rasmi cha usajili wa kampuni
(certificate of incorporation).

Utaratibu mpya

a) Hitaji la kwanza kabisa katika utaratibu
mpya ni lazima uwe na kitambulisho cha
taifa. Si kile cha mpiga kura, bali kile cha
NIDA. Hiki ni lazima. Na si lazima tu kwa
yule anayetaka kufungua kampuni, bali
lazima kwa yeyote ambaye atakuwa
mwanahisa katika kampuni (shareholder),
au ataandikwa (subscribe) kama
mkurugenzi katika kampuni.
Kwa ufupi, yeyote anayeingia kwenye
nyaraka za kampuni ambazo zinatakiwa
kuwasilishwa BRELA kwa ajili ya usajili wa
kampuni ni lazima awe na kitambulisho hiki.
Lakini pia tangu mabadiliko haya yafanyike,
muamala wowote unaotakiwa kuufanya
kuhusiana na kampuni, mathalani kubadili
jina (name change), kubadili aina ya
kampuni, kubadili wakurugenzi, kuongeza
au kupunguza wanahisa au hisa, mrejesho
wa mwaka (annual return), kuuliza hadhi ya
kampuni (official search) nk, lazima uwe na
kitambulisho hiki.
b) Lazima ufungue akaunti au mtu
mwingine mwenye akaunti akusaidie
kukusajilia. Usajili wa sasa unafanyika
kwenye mtandao kupitia akaunti
iliyofunguliwa na mhusika anayehitaji
kufungua kampuni. Kufungua akaunti

unaingia kwenye WEBSITE ya BRELA
humo utaona maelekezo ya kufungua
akaunti ambayo kimsingi si yenye utata
(complicated). Kufungua akaunti ni rahisi
sana, sharti kubwa ni uwe tu na
kitambulisho nilichoeleza hapo juu kwenye
‘a’.
c) Ukishakuwa na akaunti, uta-scan waraka
na katiba ya kampuni (memorandum &
article of association), kadhalika uta-scan
fomu zote zilizojazwa taarifa husika, utajaza
taarifa za ziada kwenye mtandao kwenye
akaunti yako kisha utatuma BRELA.
d) Ada za usajili sasa unalipia kwa njia ya
mtandao wa simu – Tigo Pesa, M – Pesa
Airtel Money nk, au benki ukitaka iwe hivyo.
e) Muda wa kusubiri usajili nao umepungua,
ambapo kama kila kitu kimefanyika vizuri
unaweza kusubiri chini ya wiki moja ili upate
cheti cha usajili wa kampuni (certificate of
Incorporation).
f) Cheti cha usajili nacho kikiwa tayari
kinatumwa moja kwa moja kwenye akaunti
yako, na wewe hukohuko uliko utakichapa
(print) na kuanza kukitumia bila kuhitaji
kwenda BRELA kukifuata kama ilivyokuwa
awali.
Ada, masuala ya uandaaji wa nyaraka na

kuzijaza taarifa, kuzisaini ikiwa ni pamoja na
kuzigonga mihuri ya wakili yamebaki
vilevile. Kubwa lililobadilika ni hitaji jipya la
kitambulisho cha taifa, na usajili kupitia
mtandao kutoka mfumo wa usajili wa ana
kwa ana (physical/manual).

Mwisho

By Jamhuri