KalugendoWakati mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, akiongoza kwa kura nyingi za urais dhidi ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, vigogo maarufu wenye majina makubwa, wamebwagwa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge.

Dk. Magufuli, ameongoza kwa idadi kubwa ya kura katika mikoa karibu yote ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kati. Lowassa amepata kura nyingi mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.

Miongoni mwa vigogo waliobwagwa ni mawaziri, waliowahi kuwa mawaziri na watu wenye “majina makubwa”.

Miongoni mwa “mibuyu” iliyoangushwa ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, aliyeangushwa na mwanasiasa machachari, Esther Bulaya, wa Chadema katika Jimbo la Bunda mkoani Mara.

Hili ni pigo la pili kwa Wasira baada ya kuukosa urais kupitia CCM ambako alikuwa miongoni mwa wanachama 38 waliorejesha fomu.

Bulaya alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kabla ya kujiunga Chadema miezi kadhaa iliyopita. Kuhama kwake CCM kunaelezwa kwamba kulitokana na hesabu zake za ubunge, akiamini kuwa asingeweza kupenya kuwania nafasi hiyo endapo angeomba kupitia CCM.

Mwingine aliyeanguka ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika; aliyeshindwa katika Jimbo la Tandahimba mkoani Mtwara na mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) aliyekuwa akiungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Ahmed Katani.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama (CCM), aambaye alikuwa akikiwakilisha chama hicho katika Jimbo la Songea Mjini ameangushwa na Joseph Fuime wa Chadema.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Aggrey Mwanri (CCM), amebwagwa na mgombea wa Chadema, Rostagodwin Mollel. Mwanri kapata kura 18,584; wakati Mollel kapata kura 22,746.

Milionea Davis Mosha (CCM) aliyekuwa akigombea Jimbo la Moshi Mjini, ameangushwa na Japhary Michael wa Chadema. Kwa miaka 20 sasa Jimbo la Moshi Mjini limekuwa ngome imara ya Chadema. Kabla yake, lilikuwa likiongozwa na Philemon Ndesamburo (Ndesa Pesa) aliyeamua kung’atuka kwa ridhaa yake mwenyewe.

Anthony Komu ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha Chadema, amemwangusha Waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami (CCM) katika Jimbo la Moshi Vijijini.

Waziri wa zamani wa Uchukuzi, Omar Nundu ameangushwa katika Jimbo la Tanga Mjini. Aliyeshinda jimbo hilo ni mgombea wa CUF.

Kimbunga cha kuwaaangusha vigogo kimemkumba pia aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki. Mshindi katika Jimbo hilo la Bukoba mjini ni Mkurugenzi wa Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare. Lwakatare alishawahi kuwa Mbunge wa Jimbo hilo kupitia CUF kabla ya kujiunga Chadema.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour (TLP), Dk. Augustine Mrema, hatima yake kisiasa inaelekea ukingoni baada ya kushindwa vibaya na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, katika Uchaguzi wa ubunge Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro.

Mbunge mahiri wa CCM, Christopher ole Sendeka naye amebwagwa na katika Jimbo la Simanjiro. Aliyemshinda ni James ole Millya wa Chadema, ambaye kabla ya kujiunga katika chama hicho, alikuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha.

Mwanasiasa chipukizi, Vincent Nyerere (Chadema) ambaye ameongoza Jimbo la Musoma Mjini kwa miaka mitano, ameangushwa na Vedastus Mathayo wa CCM. Nyerere ndiye aliyemwangusha Mathayo kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Ushindi mwingine uliotikisa ni wa Saed Kubenea (Chadema), aliyemwangusha aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi katika Jimbo la Ubungo. Dk. Masaburi ambaye anatajwa kuwa mwanasiasa “asiyeshindwa”, ameangushwa kwenye kinyang’anyiro hicho na kuwafanya wanachama wengi wa CCM kutoamini kilichotokea.

Jimbo la Kibamba mkoani Dar es Salaam, John Mnyika (Chadema), amemwangusha Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.

Kipi Warioba ambaye safari hii alipitishwa na CCM kupambana Halima Mdee (Chadema) katika Jimbo la Kawe, ameangukia pua.

Mtwara Vijijini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia (CCM), ameangushwa na mgombea wa CUF

Mtwara Mjini, Husein Murji (CCM) ameangushwa na mgombea wa CUF.

Pamoja na Nyerere, aliyekuwa Musoma Mjini, Upinzani umepata pigo kubwa kwa kupoteza majimbo mkoani Mwanza. Ezekiah Wenje (Chadema) ameangushwa katika Jimbo la Nyamagana; wakati Highness Kiwia aliyekuwa Ilemela naye ameangushwa na mgombea wa CCM, Angelina Mabula.

David Kafulila wa Kigoma Kusini na Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) wa Jimbo la Muhambwe; na Moses Machali wa ACT – Wazalendo (Kasulu Mjini), nao wameangushwa.

Wabunge wapya ni pamoja na Joseph Haule ‘Profesa Jay’ aliyelitwaa Jimbo la Mikumi, na Anthony Komu (wote kupitia Chadema).

Miongoni mwa wabunge wapya wa majimbo walioandika historia ni Esther Matiko (Chadema) ambaye ameshinda katika Jimbo la Tarime mkoani Mara. Hii ni historia kwa kuwa kwa mila za Wakurya si rahisi kumchagua mwanamke kwenye nafasi kubwa kama ya ubunge.

Baadhi ya wabunge wa upinzani wa zamani waliotetea nafasi zao ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyetetea kiti chake katika Jimbo la Vunjo, na Joseph Mbilinyi (Chadema).

Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, ameshinda kiti cha ubunge kwenye jimbo hilo ambalo kwa mara ya kwanza amekuwa mbunge wake kwa miaka miwili na nusu. Wakati huo alishinda kwenye uchaguzi mdogo.

Balozi wa Tanzania nchini Uturuki ambaye amewahi kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Deodarous Kamala, ameshinda (Chadema) ameshinda Jimbo la Nkenge. Dk. Kamala alikuwa Mbunge wa Jimbo hilo kabla ya kuangushwa kwenye kura za maoni na Mbunge aliyemaliza muda wake, Asumpta Mshama.

Hadi tunakwenda mitamboni, kulikuwa na mvutano mkali katika majimbo ya Kinondoni, Dar es Salaam ambako mtetezi wa kiti cha ubunge Idi Azan (CCM) alikuwa akichuana vikali na mgombea wa Chadema.

Pia hali bado ilikuwa tete katika Jimbo la Kyela mkoani Mbeya, ambako mgombea wa kiti cha ubunge kupitia CCM ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, alikuwa akipambana na mgombea wa Chadema.

 

Matokeo mengine ya Majimbo ni kama ifuatavyo:

 

TUNDUMA

Frank Mwakanjoka wa Chadema alipata kura 32,442 dhidi ya Frank sichalwe wa CCM alivuna kura 17,200, hivyo mgombea wa Chadema kutangazwa kuwa mshindi. Kura 77,100 zilipigwa.

 

MBINGA MJINI

Katibu wa UVCCM, Sixtus Mapunda ameshinda jimbo hilo kwa kuvuna kura 28,364 kwa kumshinda Mario Millinga wa NCCR-Mageuzi aliyepata kura 102.

 

MBINGA VIJIJINI

Martin Msuha wa CCM amemshinda Benjamin Akitanda wa Chadema katika Jimbo wa Mbinga Vijijini. Hata hivyo, Akitanda amepanga kupinga matokeo hayo mahakamani kwa madai kwamba mmoja wa mawakala wake aliumwa na akanyimwa haki ya kumteua mwingine sambamba na ushahidi wa madai ya mpinzani wake kutumia rushwa.

 

MBEYA MJINI

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mbeya Mjini, Dk. Samwel Lazaro ametangaza kwamba Chadema kimevuna kata 26 dhidi ya nane za CCM wakati kata moja uchaguzi wake umeahirishwa.

“Matokeo ya uchaguzi wa ubunge bado, lakini Chadema wanaongoza,” alisema Dk. Lazaro kwani katika kituo cha Mwasyoge kura za urais Dk. Magufuli (85), Lowassa (128).

Kwa upande wa ubunge Joseph Mbilinyi wa Chadema (147) na Shambwee Shitambala wa CCM (63) wakati katika kituo cha Kajigili, kura za urais Dk. Magufuli (105) na Lowassa (96).

Kwa upande wa ubunge Joseph Mbilinyi (105), na Shambwee Shitambala (95) huku kituo cha Mifugo B, Lowassa (104) Magufuli (139), na Mghwira (7).

 

GEITA

Chama cha Mapinduzi kimefanya vema kwa kuzoa kata zote katika majimbi ya Geita Mjini, Geita Vijijini, Bukombe, Mbongwe, Nyang’wale, Chato na Busanda.

 

TARIME MJINI

Msimamizi wa uchaguzi wa Juma Mwanjo, amemtangaza Esther Matiku kuwa mshindi katika Jimbo la Tarime Mjini baada ya kuvuna kura 20,017 dhidi ya mgombea wa CCM Michael aliyepata kura 14,502.

“Ni historia kwa Jimbo la Tarime Mjini kumchague mwanamke,” anasema Mtangazaji wa ITV, George Marato ambaye mbali ya kuwa ni mwanahabari ni mkazi wa eneo hilo ambaye anajua mila na desturi.

Taarifa zinasema kwamba wapigakura waliojiandikisha kwenye jimbo hilo jipya walikuwa 48,515 na waliopiga kura ni 35,172.

 

MOSHI MJINI

Japhary Michael wa Chadema alikuwa anaongoza katika jimbo la Moshi mjini akiingia madarakani na madiwani 14 kati ya 21 wa kata za jimbo hilo ambalo limekuwa upande wa upinzani tangu mwaka 2000.

Matokeo hayo yalipangwa kutangazwa chini ya ulinzi mkali baada ya kutokea vuta, nikuvute kutokana na mashabiki wa vyama hivyo kuamini kwamba kila upande umeshinda.

Michael alimbana Davis Mosha kwani katika kituo cha Shule ya Msingi Mawenzi- 1 Michael, Chadema (150), Davis Mosha, CCM (83) na Marchel Kitali, (UDP (1) na upande wa urais Anna Mngwira (1), Dk. Magufuli (89), Lowassa (131) na Lyimo (1).

Katika kituo cha Shule ya Msingi Mawenzi-2, Lowassa (143), Dk. Magufuli (94) na Rungwe (1) na katika ubunge katika kituo hicho, Buni Ramolewa ACT Wazalendo (1), Mosha, CCM (78), Michael, Chadema (139).

Katika urais, Lowassa wa Chadema amemwacha mbali Dk. Magufuli ni Moshi Mjini kwani mgombea huyo wa CCM hakuambulia hata nusu ya kura zilizopigwa.

 

JIMBO LA CHALINZE

Ridhiwani Kikwete wa CCM ameshinda pamoja na madiwani wake 15 wa kata za Bwilingu, Vigwaza, Kibindu, Kimange, Kiwangwa, Lugoba, Mandera, Mbwewe, Miono, Mkange, Msata, Msoga, Pera, Talawanda na Ubenazomozi.

Tangu juzi, waandishi wa JAMHURI walipita katika vituo mbalimbali na kuona namna ushindani huo ulivyo mkali na hata baada ya kupita katika baadhi ya  vituo jioni baada ya  kura kumalizika kupigwa na hata  baada ya kuwasiliana na vyanzo vya uhakika.

 

IFAKARA

Kwa tarafa ya Ifakara iliyopo Wilaya ya Kilombero-Morogoro maeneo mengi  ambayo Ukawa wanajidhihirishia ushindi kwa urais na ubunge ambako Kata nzima ya Mbasa ambayo imejumuisha vituo vya Mbassa Mlimani (1), Mbasa Mlimani (2), ACT Maendeleo na maeneo mengine huku nafasi ya udiwani kwenye Kata ya Mbassa CCM ilitwaa ushindi .

Mengine ambayo Ukawa inaongoza kwenye urais na udiwani ni Kituo cha Kilimahewa kilichopo Kata ya Tandika, Temeke jijini Dar es Salaam.

 

JIMBO LA TEMEKE

 Katika kituo cha Shule ya Msingi Majimatitu Kata ya Mtoni Kijichi Dk. Magufuli anaongoza kwa kupata kura nyingi dhidi ya Lowassa pamoja na kuwapo kwa dosari kadhaa.

Mmoja wa makarani wa Kituo cha Mbagala Majimatitu Kata ya Kijichi amesema hadi jana asubuhi walikuwa hawahakabidhi masanduku ya kura kwa viongozi.

“Hali ni mbaya ndugu mwandishi tangu juzi (Jumamosi) hatujarudi nyumbani- tunalala sehemu finyu na hadi leo hii ninavyoongea na wewe hatujakabidhi masanduku ya kura kwa viongozi…hawapo,” amesema Karani huyo.

Ameongeza kuwa pamoja na adha hiyo, lakini adha kubwa waliyokumbata nayo ni kutolipwa posho iliyotokana na kazi yao ya kusimamia uchaguzi.

Katika Kituo cha kupigia kura cha Ofisi ya Mtendaji Kata Mtoni Kijichi pamoja na upigaji kura kuanza katika muda uliopangwa (saa 1 asubuhi), dosari kadhaa zilijitokeza ikiwamo ya wasimamizi wa kura kushindwa kuweka nembo za kutambulisha masanduku ya kura za urais, ubunge na udiwani.

Hatua hiyo ilisababisha wapigakura wengi ambao walikwishapiga kura kuchanganya karatasi kwenye maboksi tofauti na baada ya wasimamizi wa kura kugundua hilo waliamua kulirekebisha hilo.

Kasoro nyingine katika Kituo cha Kijichi- CCM ni kuwa mihuri iliyotumika ilikuwa ya mwaka 2010 na michache ya mwaka 2015 ambayo nayo haikuwa na ubora.

“Vuta nikuvute” hiyo imeendelea kuwapambanisha wagombea urais wawili kati ya wanane.

Wagombea wanaovutana ni Dk. Magufuli wa CCM na Lowassa wa (Chadema) anayeungwa mkono na Ukawa.

Hata hivyo, taarifa za awali zinasema kwamba Dk. Magufuli alikuwa akiongoza kwa kura nyingi akifuatiwa na Lowassa.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damin Lubuva alitangaza matokeo ya majimbo matatu na kuonyesha Dk. Magufuli alikuwa akiongoza. Majimbo hayo ni Paje, Makunduchi (Zanzibar) na Lulindi mkoani Mtwara.

Jaji Lubuva aliyekuwa akitangaza matokeo hayo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam alisema, Dk. Magufuli aliongoza kwa kura 8,406 katika Jimbo la Makunduchi.

Katika Jimbo la Paje, Dk. Magufuli alivuna kura 6,035 wakati Lowassa alivuna kura 1,899. Jimbo la Lulindi, Dk. Magufuli alishinda kwa kura 31,603 wakati Lowassa alipata kura 11,543.

Kutoka Musoma Mjini, matokeo ya urais kituo cha CGS Shule ya Msingi Musoma B, Dk. Magufuli (kura 169), Lowassa (124), Anna Mgwira, ACT-Wazalendo (1); Chief Yemba, ADC (1), Janken Kasambala, NRA (0), Fahmi Dovutwa, UPDP (0); Macmillan Lyimo, TLP (0); na Hashim Rungwe, Chaumma (0).

Kwa upande wa kura za ubunge katika kituo hicho Mathayo wa CCM (173); Nyerere, Chadema (119); Eliud Esseko, ACT Wazalendo (1); Gabriel Ocharo, CUF (1); Chrisant Nyakitita- DP (0); Maimuna Matola-ADC (0), Ibrahimu Selemani, Tadea (0), Rutaga Sospeter, AFP (0) na Makongoro Jumanne, UMD (0).

Katika kituo cha Kitaji, Ofisi ya Kata Jimbo la Musoma Mjini matokeo ya ubunge Mathayo –CCM- (167); Nyerere, Chadema (102), Eliud Esseko, ACT Wazalendo (1), Gabriel Ocharo, CUF (0), Chrisant Nyakitita, DP (0), Maimuna Matola, ADC (0), Ibrahimu Selemani, Tadea (0), Rutaga Sospeter, AFP (1) na Makongoro Jumanne, UMD (0).

Vilevile, kwa upande wa matokeo ya urais, katika kituo cha Kitaji ofisi ya Kata, Dk. Magufuli (167), Lowassa (104), Mgwira (1), ADC, NRA, UPDP, TLP na Chaumma hazijapata kura.

Katika kituo cha John Bosco, Dk. Magufuli (143); Lowassa (82), Mgwira (3), Yemba (1) na Rungwe (1). Kwa upande wa ubunge, Mathayo (145), Nyerere (79), Eliud Esseko (2), na Gabriel Ocharo (1).

Katika Jimbo la Monduli matokeo ya ubunge katika kituo cha NMC B, Namelok Sokoine wa CCM (58), Julius Kalanga wa Chadema (137), Navaya Ndaskoi, ACT-Wazalendo (1).

Katika kituo hicho matokeo ya urais Mghwira wa ACT-Wazalendo (2), Lowassa (Chadema) 150, Dk. Magufuli (CCM) 39, Rungwe (Chaumma) 01. Kituo cha NMC A matokeo ya ubunge ni Namelok Sokoine (CCM) 38, Julius Kalanga (Chadema) 169, Navaya Ndaskoi (ACT-Wazalendo) 01.

Urais kituo cha NMC A, Mghwira (ACT-Wazalendo) 0, Lowassa 178, Dk. Magufuli (30), Lyimo (0).

Taarifa kutoka Dodoma zinasema, matokeo ya urais kituo cha Mwangaza-1, Mghwira (2), Dk. Magufuli (156) na Lowassa (131) wakati ubunge katika kituo hicho, Christina Alex wa ACT Wazalendo (5), Antony Mavunde wa CCM (144) na Kigaila Singo, Chadema (135).

 

SHINYANGA

Matokeo ya awali ya urais katika kituo cha Uwanja wa Soko Mageuzi: Dk. Magufuli (134), Lowassa (104), Mghwira (1) na wagombea wengine hawakupata kura; wakati kwa upande wa ubunge katika kituo hicho, Steven Masele wa CCM (112), Patrobas Katambi, Chadema (127), Nyangaki Shilungushela wa ACT Wazalendo (1).

 

MWANZA

Katika jimbo la Nyamagana, kituo cha Calfonia Majengo Mapya B, Chacha Okong’ wa ACT Wazalendo (1), Mabula Stanslaus wa CCM (152), Wenje EzekiaH, Chadema (99), Faida Hassan, CUF (1); Mohamed Juma, Jahazi Asilia (0); Ahmed Mohamed, NRA (2) na Ramadha Uhadi wa UDP hakupata kitu.

Kwa upande wa urais Mgwira (0), Dk. Magufuli (170), Lowassa (85) na waliosalia wamepata 0.

Hali imeanza kuwa tete Zanzibar ambako maduka kadhaa yamefungwa.

Mbali ya Unguja, pia Pemba taarifa zinasema katika Kituo cha Skuli ya Bwagamoyo, Jimbo la Mtambwe wilayani Wete, Pemba katika Kituo Namba 1, Maalim Seif Sharrif Hamad amepata kura 317 na Dk. Mohamed Shein 5, wakati kituo Namba 2- Maalim Seif (220), Dk. Shein (2).

Katika kituo cha Gombani Station (1),(2) na (3) jimbo la Wawi, Mkoa wa Kusini Pemba, Dk. Shein (18), Maalim Seif (258), Hamad Rashid (4).

Katika kituo cha Station 2, Dk. Shein (21), Maalim Seif (246), TLP (1), ADC (1), ACT (1), Tadea (1) na SAU(1). Matokeo hayo yalitolewa na msimamizi mkuu wa kituo cha Gombani Stadium, Abubakar Shaame Faki.

Matokeo ya awali katika Kituo cha Skuli ya Bwagamoyo Wilaya ya Wete, Pemba, Kituo namba moja, Jimbo la Mtambwe, Maalim Seif amepata kura 317 na Dk. Mohamed Shein (5). Kituo Namba 2, Maalim Seif (220) na Dk. Shein (2).

Taarifa nyingine zinasema kwamba Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Steven Kebwe naye ameangushwa na mgombea wa Chadema katika Jimbo la Serengeti mkoani Mara.

Mkoa wa Kusini Pemba, Jimbo la Mkoani, Dk. Magufuli amepata kura 3,341 wakati Lowassa 7,368; Jimbo la Mtambile Dk. Magufuli amepata kura 902 wakati Lowassa alipata kura 5,875.

Jimbo la Chambani, Dk, Magufuli alivuna kura 818 na Lowassa 5,319; Mkoa wa Pemba katika Jimbo la Kiwani Dk. Magufuli alipata kura 1,661 wakati Lowassa alivuna kura 4,229.

Mkoa wa Katavi katika Jimbo la Nsimbo Dk. Magufuli wa CCM amepata kura 31,413 wakati Lowassa amepata 6,042; mkoani Mtwara katika Jimbo la Ndanda Dk. Magufuli amevuna kura 33,699 na Lowassa alipata kura 19,077.

Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar Jimbo la Donge, Dk. Magufuli amepata kura 5,592 wakati Lowassa amepata kura 1,019 wakati katika Mkoa Kaskazini Unguja, Jimbo la Kiwengwe Dk. Magufuli (3,317) na Lowassa (1,104).

Huko mkoani Tanga, Jimbo la Bumbuli Dk. Magufuli amepata kura 35,310 wakati Lowassa amevuna kura 7,928 huku Mkoa wa Pwani-Jimbo la Kibaha Mjini Dk. Magufuli alipata 34,604 na Lowassa kura 25,448.

By Jamhuri