NA MICHAEL SARUNGI

Wiki chache zilizopita, Rais mstaafu wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, alitunukiwa tuzo ya Mo Ibrahim ya  mafanikio katika uongozi wake katika kipindi cha mwaka uliopita, na kujizolea kiasi cha dola za Marekani milioni tano.

Mwanamama huyo shupavu, ameiongoza Liberia kwa vipindi viwili kuanzia 2006 hadi 2017 huku akisifiwa kwa namna alivyoitoa nchi hiyo katika kipindi cha mpito kutoka vita ya wenyewe kwa wenyewe hadi kufikia hatua ya kubadilishana madaraka kwa amani.

Wakati wa uongozi wake, Sirleaf alipongezwa kutokana na juhudi zake za ziada kuiongoza na kulirejesha taifa la Liberia katika hali ya utulivu, baada ya miaka kadhaa ya vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyosababisha wananchi wengi kupoteza maisha.

Tuzo ya Ibrahim inalenga kutofautisha viongozi ambao wakati wa utawala wao waliweza kuziendeleza nchi zao, kuimarisha demokrasia na kuheshimu haki za binadamu kwa manufaa ya pamoja ya watu kuwa na maendeleo endelevu.

Akitangaza uamuzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Dk.  Salim Ahmed Salim, alisema, “Ellen Johnson Sirleaf alichukua uongozi wa Liberia wakati nchi hiyo ikiwa imeharibiwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe na kuanzisha mchakato wa maridhiano yaliyozingatia ujenzi wa taifa na taasisi zake za kidemokrasia.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha mihula miwili ya uongozi wake, mwanamama huyo alifanya kazi bila kuchoka kwa niaba ya watu wa Liberia na mwisho wa siku Liberia ya leo imekuwa nchi ya mfano wa kuigwa.

Amesema safari hiyo haiwezi kuwa bila vikwazo, na leo Liberia inaendelea kukabili changamoto nyingi. Hata hivyo, miaka kumi na miwili akiwa ofisini, Sirleaf aliweka misingi ambayo Liberia inaweza sasa kujenga juu yake,” amesema Salim.

Ushindi wa mwanamama huyo unapaswa kuwa mfano kwa viongozi wengi wa Afrika ambao bado wapo madarakani huku nchi zao zikilaumiwa kwa uwepo wa chembe chembe za ukiukwaji wa haki za binadamu.

Haya yote yamekuwa yakichangiwa na uchu wa mali na madaraka miongoni mwa wanasiasa wengi wa Kiafrika na wapambe wao, kuwa chanzo kikubwa cha vurugu na maafa makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia.

Kuna haja ya Umoja wa Afrika kuongeza juhudi katika kutatua migogoro ya kivita na kinzani za kisiasa ili amani, utulivu na ustawi viweze kurejea barani Afrika kwa manufaa ya Waafrika wa sasa na kizazi kijacho.

Hali ya kisiasa katika nchi za Burundi, DRC, Rwanda na Uganda zimeendelea kuwa katika hali ya sintofahamu baada ya kubadili katiba ili kutoa nafasi kwa marais wa nchi hizo kutawala hata kama ni kwa kuvunja katiba.

Sirleaf alichaguliwa kuwa Rais wa Liberia Januari 16, 2006 baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa kitaifa mwaka 2005. Aliongoza kipindi cha kwanza mwaka 2006-2011 na kushinda tena muhula wa pili 2012-2017.

Ellen Johnson Sirleaf atapata dola za Kimarekani milioni tano zitakazogawanywa kwa miaka kumi, na dola laki mbili kwa maisha yake yote.

Ellen Johnson Sirleaf anaingia katika orodha ya viongozi wengine waliowahi kutwaa tuzo hiyo wakiwamo Hifikepunye Pohamba wa Namibia (2014), Pedro Pires wa Cape Verde (2011), Festus Mogae wa Botswana (2008) na Joaquim Chissano wa Msumbiji (2007).

Mshindi wa kwanza kuzindua tuzo hiyo akipewa kwa heshima alikuwa Nelson Mandela mwaka 2007.

920 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!