Rais mpya wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume ametaja mambo matano ambayo atayafanyia kasi baada ya kuchaguliwa kuongoza chama hicho, Jumamosi mjini Arusha.

Fatma Karume ambaye ni binti wa Rais Mstaafu wa Zanzibar amesema kuwa, ataendeleza yale yaliyofanywa na mtangulizi wake, Tundu Lissu, ikiwamo kusimamia demokrasia, haki, utawala bora, haki za wanasheria pamoja na kufanya uchunguzi ili kubaini sababu zinazopelekea watu kutokutaka kuifanya kazi hiyo.

Katika uchaguzi huo, Fatma alipata kura 820 akimzidi Godwin Gwilimi aliyepata kura 363, Godwin Mwalongo (12) na Godfrey Wasonga (6).

Aliongeza kuwa TLS itahoji mamlaka ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na Upelelezi (DPP), kuhakikisha wanasheria wanashirikishwa katika utungaji wa sheria na ada za uanachama wa TLS.

Baada ya kuingia katika uongozi, Fatma alisema kuwa jambo la kwanza atakalolifanya ni kubadili hali ya wanasheria nchini.

“Nataka kujua kwa nini hawataki kufanya kazi za uwakili. Kuna tatizo hapa la kwa nini wanasomea kazi hii lakini hawataki kuifanya. Nataka nitafute sababu,” alisema.

Alisema wanachama wa TLS waliofanya kzi za uwakili kwa mwaka 2016 walikuwa 2,931 lakini kwa mwaka 2018 wamepungua na kufikia 2,270.fatma ameseama kuwa TLS imepoteza wanachama 661 waliokuwa wanafanya kazi za uanasheria.

“Tukumbuke mwaka huu na mwaka jana kumetokea nini? Ofisi za (kampuni ya uwakili ya) Immma zilishambuliwa kwa bomu, ofisi za wanansheria wengine zimeshambuliwa na wengine wamewekwa selo bila makosa, lakini pia (aliyekuwa ) Rais wa TLS alipigwa risasi,” alisema.

Fatma, ambaye pia ni mwanasheria wa kampuni ya Immma, alisema hata kama serikali itasomesha vijana wengi kuwa wanasheria, kama mazingira ya kazi yatabaki kuwa ya vitisho na mashambulizi, wengi wataachia taaluma hiyo.

“Kwa maana hiyo wananchi ndio wataathirika. hii ni changamoto kubwa sana,” alisema.

Jambo la pili ambali alisema atalifanyia kazi akiwa TLS ni kuhoji namna DPP anavyotumia madaraka yake.

Alisema DPP amekuwa akiwakamata watu na baadaye kuwanyima dhamana au kuendelea kuwashikilia akidai kuwa upelelezi haujakamilika.

“Inakuwaje anawakamata watu wakati upelelezi haujakamilika? Watu wakiomba kudhaminiwa anasema wasidhaminiwe. Anaiambia mahakama hakuna kutoa dhamana, hii ina maana anatumia madaraka vibaya,” alisema.

“Mpaka sasa unajua ni wanasheria wangapi wako ndani na kesi zao hazijasikilizwa na hawajapewa dhamana?

“TLS isimamie suala hili kwa nguvu sana, kuhusu namna anavyotumia madaraka yake vibaya.”

Alisema zamani TLS ilipuuza suala hilo, lakini kwa sasa limekuwa kubwa na wameona walifanyie kazi kwa kina.

Kadhalika, Fatma amesema suala la tatu ni kuhakikisha wanasheria wanashirikishwa katika shughuli za kutunga sheria.

“Lazima tushirikishwe kwa sababu sisi ni wadau na tuna wajibu wa kutazama sheria, kuangalia hii inafaa na hii haifai, hii itamuumiza huyu,” alisema.

Kuhusu suala la ada za uanachama wa, Fatma alisema hakuna haja ya kuzishusha kwa sababu hilo si ytatizo linalosababisha wanachama kuacha kufanya kazi za uanasheria.

“Hatutapunguza ada, baraza kuu limeamua kuwa ni bora ada kubaki vilevile. Mungu akijalia tutamaliza mwaka ssalama na ninataka kuhakikisha kwamba tunawavutia watu kuingia katika taaluma hii kwa sababu (kwa sasa) imeharibiwa,” alisema.

Kuhusu kufuata nyayo za Lissu, mwanasheria huyo alisema Mbunge huyo wa Singida Mashariki (CHADEMA) ni kiongozi aliyesimamia utawala bora, haki za wanasheria hivyo na yeye anakwenda kusimamia hayo.

Kuhusu kanuni za uchaguzi za TLS, Fatma alisema juzi baraza Kuu la Chama hicho lilikubaliana kwamba alichokifanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ni uvunjaji wa sheria.

Machi 10, 2018, TLS ilidai kuwa ofisi ya AG imeongeza masharti katika mabadiliko ya kanuni za uchunguzi wa chama hicho, yanayowanyima futsa watumishi wa umma na wanasiasa kuwania uongozi owote wa chama hicho.

Fatma alisema wanachama zaidi ya 1,500 wa baraza kuu la chama hicho walikubaliana kuwa AG alivunja sheria. Hata hivyo hawakutaka kusema hatua ambazo TLS inachukua.

920 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!