Nakubaliana na kauli ya viongozi, ikiwa ni pamoja na ya Rais John Magufuli, kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya si jambo dogo.

Alitamka: “Hii ni vita kubwa na siyo suala la mzaha. Ni lazima tuisimamie kwa nguvu zote.”

Ni kauli ambayo haipingani sana na kauli za viongozi mbalimbali duniani ambao wanakabiliwa na tatizo la biashara ya dawa ya kulevya ndani ya nchi zao, kutokana na madhara makubwa kwa jamii yanayosababishwa na biashara hiyo.

Nchini Marekani imekadiriwa kuwa athari za biashara hiyo kwa uchumi wa Marekani mwaka 2002 zilisababisha hasara ya dola bilioni 180.9 za Marekani. Pato la taifa la Tanzania mwaka 2013 ilikuwa dola bilioni 32.23 za Marekani tu.

Athari kubwa zaidi kwa nchi ni afya ya watu wanaotumia dawa za kulevya. Na kwa bahati mbaya ni vijana zaidi wanaotumbukia katika vishawishi vya kuanza kutumia dawa hizi, na matokeo wanakuwa waathirika wakuu. Isitoshe, anayetumia dawa mara kwa mara hushindwa kuacha kuzitumia kwa urahisi. Na kwa wale wanaotumia dawa hizo kwa kujidunga sindano, basi ipo hatari kuwa sindano hizo, kwa kutumika kwa kuazimana, huwa chanzo cha maambukizi ya Ukimwi.

Aidha, utegemezi wa mwili wa kutumia dawa za kulevya unamfanya mzazi anayetumia dawa hizo kutanguliza ulevi wake kabla ya kufikiria mahitaji ya watoto wake. Kwa sababu hiyo, watoto wenye wazazi walioathirika wanakumbana na tatizo la kutotimizwa kikamilifu kwa mahitaji yao ya msingi.

Lipo tatizo pia la mwajiriwa anayetumia dawa za kulevya na jinsi matumizi hayo yanavyoweza kuathiri ufanisi wa kazi yake. Tunasikia mara kwa mara ajali za gari zinazosababishwa na madereva wanaoendesha wakiwa wamelewa pombe au dawa za kulevya.

Ukitafakari kwa undani kazi nyeti zilizopo kwenye jamii, kama vile rubani au daktari bingwa anayefanya upasuaji, basi utaona ni jinsi gani kushinda vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya ni muhimu kwa jamii zote.

Siyo watumiaji wote wa dawa ya kulevya wenye uwezo wa fedha wa kununua dawa hizo. Kwa sababu hiyo, wengi wao hujihusisha na uhalifu ili kuweza kupata fedha za kununua dawa. Kwa sababu hiyo jamii inayokabiliwa na biashara hii, inakabiliwa pia na ongezeko la uhalifu wa kundi la waathirika ambao wanafanya uhalifu kwa sababu tu ya kupata fedha za kununua dawa ya kulevya.

Hapo hatujazumgumzia wanaokutwa hatiani kutokana na makosa yanayoainishwa ndani ya sheria mbalimbali, kama vile utengenezaji, usafirishaji, uuzaji, na matumizi. Ukizingatia tena kuwa wanaokutwa hatiani wanaweza kuwa ni wazazi wenye wategemezi, basi tunakuta tena biashara hii inaathiri kundi kubwa la watu wasiojihusisha nayo kabisa.

Kwa hiyo ukiorodhesha gharama za tiba kwa taifa kwa ajili ya waathirika, ukijumlisha idadi ya watu wanaokutwa na hatia mbalimbali kuhusiana na biashara hii haramu na gharama kwa mlipa kodi ya kuwaweka gerezani, ukijumlisha ajali na gharama za ajali zinazosababishwa na waathirika, tija ndogo ya waathirika walioajiriwa na hasara yake kwa uzalishaji, na gharama nyingine nyingi ambazo zinasababishwa na biashara hii, siyo rahisi kupingana na serikali juu ya azma yake ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya.

Lakini hayapo makubaliano kwa kila jambo, ikiwa ni pamoja na njia sahihi za kuchukua kupambana na biashara hii. Zipo njia tatu kuu zinazotumiwa na nchi tofauti: kuchukulia tatizo zima kuwa ni la jinai pekee; kuchukulia kuwa tatizo ni la jinai, lakini kuruhusu matumizi madogo bila kumtia mtu hatiani kwa anayekutwa na dawa hizi; na kuruhusu, kama ilivyo nchini Uholanzi, matumizi ya aina fulani ya dawa za kulevya.

Zile nchi ambazo zinaelekea kuweka mkazo kwenye kuharamisha biashara hii, kama Mexico na Marekani, zimefanikiwa zaidi kuongeza wafungwa kwenye magereza ya nchi hizo. Lakini sehemu kubwa ya hao wanaonaswa ni watumiaji wa viwango vidogo.

Zile nchi ambazo zinaelekea kuweka mkazo kwenye kupunguza msisitizo wa uharamishaji wa biashara hii, hasa kwa watumiaji, kwa mfano Ureno na Uholanzi, zimepunguza wafungwa kwenye magereza na hata kupunguza viwango vya matumizi ya dawa za kulevya ya aina fulani. Ufanisi umetokana na kusisitiza kuwa tatizo la dawa za kulevya ni tatizo la kiafya pia, siyo jinai pekee.

Nchini Mexico vita kubwa dhidi ya dawa za kulevya iliyoibuliwa mwaka 2006 na Rais wake Felipe Calderón ilisababisha kujaza magereza nchini humo. Lakini, kwa mujibu wa takwimu na kama nilivyosema hapo awali, asilimia 41 ya wale waliyo jela ni watu waliokutwa na viwango vidogo mno vya dawa za kulevya.

Hoja ni kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya hufanikiwa zaidi kukamata dagaa, na kuacha nyangumi. Vita hii ingeelekezwa zaidi kupambana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

Changamoto ya kuandama wafanyabiashara ni kubwa kwa sababu ya uwezo wao mkubwa wa fedha. Hata wanapotuhumiwa, wanakuwa na uwezo mkubwa wa kutumia huduma za kisheria za mawakili waliobobea katika utetezi wa watuhumiwa wa uhalifu.

Aidha, uwezo huu wa fedha unafanikisha wakati mwingine kugeuza vidhibiti vya unga unaoaminiwa kuwa dawa za kulevya kuwa unga wa ngano.

Kwa hali hii, papa na nyangumi ambao wananaswa na nyavu ya kisheria kwa muda, huponyoka na kuacha dagaa wakitumikia vifungo gerezani.

Hizi ndiyo changamoto kuu za vita dhidi ya dawa za kulevya. Hazipaswi kufanyiwa mzaha wala dhihaka. Lakini ni changamoto ambazo hazina suluhisho rahisi.

899 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!