Leo najua Taifa linakabiliwa na matatizo mengi. Kuna wenzetu waliopotea kwa kusema ukweli. Sina uhakika kama kwa mwenendo huu nchi yetu itabaki salama. Wanaopotelewa na ndugu zao wakiungana, tutakuwa na jeshi kubwa la kupinga upoteaji. Sina uhakika pia kama kwa kuandika makala hii nami sitapotea siku moja.
Sitanii, kwa muda nimekuwa nikisikia habari za watu kupotea katika nchi jirani za Rwanda, Kenya, Uganda, Burundi na DRC. Niliamini tumeishavuka mipaka ya kupotezana. Niliamini tuna hofu ya Mungu. Ipo siku, kama wapo wanaoshiriki kupoteza wengine, nao watapotea. Binadamu hatuishi zaidi ya miaka 100. Wanadhani hawafahamiki, wengine wanatolea watu bastola, ila ipo siku!
Ni bora tukasema Mungu yupo, kuliko kusema hayupo tukafika mbinguni na kukuta ndiye anayepokea wageni. Narudia, hata ukitumwa na chama cha upinzani au chama tawala au Serikali kwamba kamteke fulani, jiulize mara mbili. Siku ya mwisho utapeleka hesabu. Kwamba hapa duniani matendo yako yalichangiaje ustawi wa wengine! Na wala si shida sana, unapomteka mtu, ukampoteza, ipo siku utakufa tu kwa mapenzi ya Mungu.
Saa chache kabla ya kwenda mitamboni, nimesikia Roma Mkatoliki amepatikana. Inabidi ahojiwe vilivyo. Aeleze alikuwa wapi. Ikithibitika kuwa alijiteka, kama baadhi ya watu wanavyodai kuwa kuna wanaojificha kuitia Serikali joto, basi aadhibiwe vilivyo. Ikithibitika alikuwa ametekwa, basi aliyemteka achukuliwe hatua kali za kisheria.
Nchi hii tukiacha mambo haya yanayoonekana kuwa ni madogo yakaendelea, mwisho wa siku tutashuhudia makubwa. Narudia, sisi sote ni wadau wa amani. Tunalo jukumu na tunapaswa kuilinda amani ya nchi yetu, kudumisha upendo na mshikamano. Ukimwona mwenzako anatenda ndivyo sivyo, toa taarifa kwenye mamlaka. Tuchunge usalama wetu. Tulindane na huo ndiyo ustaarabu. Tusikubali mwenzetu hata mmoja apotee.
Leo, kichwa cha makala hii kinasema ‘Wabunge wetu, kodi za nyumba’. Tupo hapa Kilimanjaro, Moshi tunafanya mkutano wa wahariri wa mwaka. Wapo wawasilishaji kadhaa walionigusa katika mada zao. TASAF walitupeleka vijijini. Tumeshuhudia umaskini wa kutisha. Mtu anaishi kwenye nyumba ya tembe, bila kujali baridi ya Moshi. Ni hatari.
NMB Bank wamewasilisha mada yao, ikaonekana wameanza kutafuta hadi wakulima, hapana shaka ni kutokana na ugumu wa maisha. Ni jambo jema kurudi kwa wananchi, ila kuna kila dalili kuwa sasa maisha si kama zamani. Ni magumu.
Sitanii, tumepita Tanga Cement, wanaozalisha saruji ya Simba. Nao wanalia. Makaa ya mawe wanayopewa hayatoshi. Wanahitaji tani 12,000 kwa mwezi, lakini kiwango hiki hakijawahi kufikiwa hata mara moja, wanapata chini ya tani 7,000 hivi. Hili ni tatizo kubwa. Wanalia na kuruhusu viwanda vipya vya saruji. Hii ni hatari. Tukilia sote nani atamfuta machozi mwenzake?
Mwaka 2005 Tanzania ilifuta kodi ya kichwa. Kodi hii ilikuwa inalipishwa kwa mwanaume mwenye umri wa kuanzia miaka 18. Kwa bahati mbaya, Sheria ya Fedha ya Mwaka 2016 imerejesha kodi ya kichwa kupitia mlango wa nyuma. Sheria hii inataka sasa kila Mtanzania kulipa kodi ya nyumba anayoishi.
Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni watekelezaji, ila wanaitetea kodi hii usipime. Kodi hii haitendi haki. Sote tunahamasishana tulipe kodi, ila si kwa utaratibu huu. Binafsi, sina tatizo na kodi ya nyumba kwa nyumba za biashara. Kinachonipa shida ni kutoza kodi nyumba anayoishi mtu.
Hii mana yake ni nini? Kwa mtu anayefanya kazi au biashara, ina maana fedha alizotumia kujenga nyumba (kama zilitokana na mapato halali) kwa maana ya mshahara au biashara) alikwishazilipia kodi kwa utaratibu wa lipa kadri unavyopata (PAYE).Ikiwa nyumba anayoishi haimwingizii pato lolote, mtu huyu kwa nini alipe kodi, na anazolipa fedha anazipata wapi?
Kumtoza kodi wakati hakuna pato analoingiza kutokana na nyumba hii kwa njia rahisi ni kumhamasisha auze mali alizonazo alipe kodi. Inawezekana wabunge hawakuliona hili wakati wanapitisha bajeti. Nasema, wabunge wetu watusaidie. Watu watalazimika kuuza mali zao kulipa kodi.
Sitanii, wapo watu wanasema kiasi kilichokadiriwa kwenye kodi za nyumba kwa mtu ambaye hajafikisha miaka 60 ni kidogo. Wanaona Sh 3,000 au 10,000 ni pesa kidogo. Kabla ya kufikisha hitimisho hili wangewasiliana na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Ukishuhudia watu wanapokea Sh 20,000 kwa matumizi ya miezi miwili, ndipo utakapofahamu kuwa umaskini upo.
Inapotokea mzazi mwenye umri wa miaka 60 na zaidi akafariki, kinachotokea watoto wanaorithi hiyo nyumba inabidi waanze kulipa hiyo kodi ya majengo mara moja. Sheria hii nadhani ilitungwa haraka haraka. Hivi, kama huyo mwenye nyumba ameacha watoto wenye umri wa miaka 3, 4, 5 au miezi kadhaa, na mama yao aliishafariki pia, hawa watalipa kutoka wapi?
Sitanii, kodi ya kichwa iliyofutwa mwaka 2005 ilikuwa ni Sh 3,000. Wakati Waziri wa Fedha wa wakati huo, Basil Mramba, anaifuta, alisema kodi hiyo ina madhara zaidi huko mbele. Mramba aliangalia uchaguzi, lakini uhalisia madhara ya kodi kwa mtu asiye na kipato ni makubwa kuliko tunavyodhani.
Enzi hizo labda kwa watu ambao hawakuwapo, wanaume walikuwa wanalala maporini. Watu wengi walikimbia makazi yao na kulala misituni kwa sababu ya kodi ya kichwa. Kodi hii ilianzishwa na mkoloni mwishoni mwa miaka ya 1800 kama rungu la kulazimisha watu kwenda kwenye mashamba ya mkonge na kwingineko.
Siyo siri kwamba wakati huo kazi zilikuwa zinatafuta wa kuzifanya. Hali ni tofauti kwa sasa. Watu wanatafuta kazi hadi nyayo zinauma. Wengine wanaachishwa kazi baada ya kampuni kushindwa kujiendesha kwa ufanisi. Mtu wa aina hii kulazimisha kuwa apate hiyo hela aliyokadiriwa kwa nyumba aliyojenga kwa kutumia fedha za mshahara zilizolipa kodi wakati wa kupatikana, ukiacha kuwa ni kutoza kodi mara mbili, pia ni kumlazimisha mtu auze mali zake kulipa kodi kama nilivyosema hapo juu.
Kodi hii ilipoanzishwa nchini Uingereza, walitokea watu jasiri wakaenda mahakamani wakaipinga na ikafutwa. Sisi hapa kwetu sina uhakika iwapo tunafahamu madhara ya kodi hii mbele ya safari. Ikisimamiwa vilivyo, wapo watu wengi watakaoishia magerezani kwa kushindwa kulipa kodi hii.
Sitanii, nasisitiza kuwa kupanua wigo wa kodi si kurudisha kodi ya kichwa. Aliko Dangote amefungua kiwanda tayari amelipa kodi zipatazo Sh bilioni 45. Huko ndiko tunakopaswa kujikita. Ghana wamefanya uamuzi wa kisera, kwa kusema kiwanda kimoja kwa kila wilaya moja. Hii maana yake ni nini? Tanzania inazo wilaya 170 hivi kwa wastani.
Kama kila wilaya ingekuwa na kiwanda kinachozalisha na kulipa wastani wa Sh bilioni 30 tu kwa mwaka, tungepata zaidi ya Sh trilioni 5 kutokana na chanzo hiki kipya cha mapato. Wala tusingefikiria kuanzisha kodi ya kichwa tena. Viwanda vipo vingi vya kuanzishwa na tukauza nje ya nchi.
Vitu kama viatu, vijiko, nguo, sabuni, mafuta, saruji, vigae, nondo, mabati, vikombe, njiti za meno na vingine vingi vinatumika hapa nchini, lakini hakuna sera ya makusudi kuwezesha viwanda vya aina hiyo kujengwa hapa nchini.
Watanzania hawajaelimishwa wanawezaje na ni hatua zipi wanapaswa kuzipitia kupata mtaji wa kujenga kiwanda. Wengi wanafikiri ni lazima utafute fedha kwa nguvu zako zote, na uwezo wako wote ndipo upate mtaji wa kama Sh bilioni 400 kujenga kiwanda. Kwa utaratibu huu utatafuta hadi ufe kabla hujazipata.
Watanzania wanahitaji elimu ya mikopo na utaratibu wa kupatikana kwa mikopo yenyewe. Si rahisi nchi ikapiga hatua na kupata mapato makubwa tusipoweka sera rafiki za kuwezesha watu kupata mikopo, wananchi wakawa na hela, mzunguko wa fedha ukawa mkubwa, na katika kulipwa au kulipa kwao Serikali ikakusanya kodi ya maana.
Sitanii, naunga mkono ulipaji kodi, ila si kwa utaratibu huu. Waheshimiwa wabunge liangalieni hili. Najua mnazo siasa zenu kama tulizozishuhudia wakati wa mnyukano wa kupata wabunge wa Afrika Mashariki, lakini inapofika suala la kitaifa kama hili la kodi, hebu unganeni kusaidia kuionesha Serikali wapi pa kupata kodi hizo na njia za kuanzisha vyanzo vipya ya haki, ila si kwa njia hii ya kurejesha kodi ya kichwa kiujanjaujanja.
Leo mjiangalie kuwa mnao uwezo wa kulipa hiyo kodi, fikiria ipo siku hata ninyi mtakuwa hamna kipato. Hali hii tusisubiri itukumbe. Mungu ibariki Tanzania.

1366 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!