Wafanyabiashara na TRA

493. MATATIZO YA UTARATIBU HUU NA MIANYA YA RUSHWA

(i) Idara ya Upelelezi, Uzuiaji na Mashtaka Makao Makuu na Kitengo cha Ofisi za kanda kinawasaka wakwepa kodi, wafanyabiashara ya magendo na wanaolipa kodi ndogo, ikiwezekana kukamata mali zao na kuwafungulia mashtaka. Kwa wale wanaokamatwa mara nyingi wamekuwa wanakubali kufikia usuluhishi nje ya mahakama ambapo mtuhumiwa na Afisa Forodha wanafikia maelewano kuhusu kodi ya kulipa. Utaratibu huu unatoa mwanya kwa Afisa Forodha kupokea rushwa kutoka kwa mteja ili apunguze kiasi cha kodi hiyo.

(ii)Baadhi ya wafanyabiashara wana tabia ya kuchukua hatua za mkato ili kupambana na urasimu ambapo wanalazimika kutoa rushwa kwa watumishi wa Idara ili waweze kufanikisha shughuli zao. Utaratibu wa kujaza fomu nyingi ambazo zinapitia sehemu nyingi kabla ya malipo ni matatizo vile vile.

 (i) Eneo la Long room ni kama bwalo lililopangwa meza nyingi na linawezesha wateja kukutana ana kwa ana na watumishi wa Forodha. Aidha, linamwezesha mteja kuona kila hatua iliyofikiwa wakati wa kushughulikia kadhia yake. Pale mteja anapoona kwamba kadhia yake inaelekea kukwama humwita  mtumishi wa sehemu hiyo na kumpa rushwa ili aweze kupitisha kadhia yake.

 Tume imeelezwa kwamba siku hizi waagizaji wanapowasilisha kadhia zao Idara ya Forodha huweka kiasi fulani cha fedha ambazo maafisa wanaoshughulikia kadhia zao wanagawana ili kadhia hizo zisikwame sehemu yoyote ile. Mamlaka ya Mapato inatarajia kufanya ukarabati wa Long Room ili kuzuia mwanya wa wateja kuonana ana kwa ana na watumishi wa Mamlaka. Utaratibu huu utapunguza kwa kiasi kikubwa mianya ya rushwa katika idara hii.

 (ii) Kila bidhaa inayoagizwa nchini ina namba yake ya tariff ambayo inamwezesha Afisa Forodha kuweka kiwango cha kodi.  Mteja anaweza kutoa rushwa kwa Afisa Forodha ambaye anaweka Tarriff No. yenye kiwango cha chini cha kodi. Kwa kuwa mtumishi wa Long room haoni mizigo, mteja ambaye ameagiza lori jipya anatoa rushwa kwa Afisa Forodha ambaye anatoa namba ya tarriff ya magari yaliyotumika ili alipe kiwango kidogo cha kodi.

 (iii) Sehemu  ya Ukadiriaji (Valuation Section) inatakiwa kuwa na Benki ya Takwimu yenye kuonyesha bei muhimu za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje. Hapo zamani Idara ilikuwa inawapeleka maafisa wake katika nchi ambazo Tanzania inafanya  nazo biashara kwa wingi ili kukusanya bei za bidhaa mbalimbali. Kutokana na matatizo ya fedha shughuli  hii haifanyiki.

 Matokeo yake ni kwamba maafisa katika sehemu hii wanaweza kukataa kupitisha kadhia kwa kisingizio kwamba bei zilizoko katika kadhia ni ndogo bila ya kuwa na bei za malinganisho. Wakati mwingine waagizaji wawili wanaweza kuagiza idadi sawa ya bidhaa moja, lakini sehemu hii inakadiria kodi tofauti. Ili kadhia zao zisikwame wagizaji wamekuwa wanatoa rushwa kwa maafisa hawa na mara nyingine hata kabla mizigo haijawasili nchini.

 (iv) Utaratibu unaowataka Maafisa Forodha kukagua bidhaa zote ili kubaini usahihi wa idadi iliyojazwa kwenye kadhia hautekelezwi kikamilifu. Kwa kutumia kisingizio cha muda wamekuwa wanaruhusu mizigo hiyo bila kuikagua baada ya kupokea rushwa.

 (v) Chini ya utaratibu wa sasa Afisa Forodha sehemu ya Ukaguzi anaruhusiwa kuongeza kiasi cha kodi pale ambapo anagundua kwamba kodi iliyolipwa mwanzoni ni kidogo kuliko idadi ya mizigo iliyoonyeshwa kwenye kadhia. Utaratibu huu unategemea sana uzalendo, uaminifu na usimamizi wa Afisa Forodha anayekagua mizigo hiyo. Ukweli kwa hali ya sasa ni vigumu kumpata mtumishi wa aina hii na kama anaongeza kodi ni kutokana na maelewano kati yake na mteja.

 (vi) Katika vituo vya mipakani utaratibu wa kuingiza mizigo una matatizo zaidi kwa sababu ya uhaba wa watumishi. Mtumishi mmoja wa Idara anaweza kujaza kadhia za mizigo, kufanya tathmini ya kodi inayotakiwa kulipwa na mwisho kufanya ukaguzi wa mizigo hiyo hiyo. Shughuli zote hizi zikifanywa na mtu mmoja zinaacha mwanya mkubwa wa mteja kutoa rushwa kwa mtumishi huyo ili alipe kodi ndogo. Kwa kuwa hakuna ‘checks and balances’ katika utaratibu huu mtumishi hupokea rushwa bila ya wasiwasi wowote.

(vii) Chini ya utaratibu wa sasa wa kuondoa mizigo bandarini au kituo cha mpakani mteja anawajibika kujaza fomu za ushuru wa forodha, kodi ya mauzo na Excise na Declaration of Disposal Order (D&DO) kwa upande wa bandari. Ijapokuwa hatua hii imechukuliwa kwa makusudi kudhibiti mapato ya serikali, wateja wamekuwa wanalalamika kwamba fomu hizi ni nyingi. Tume inaelewa kwamba Mamlaka ya Mapato ina mpango wa kuandaa fomu moja tu ya kadhia ya kushughulikia mizigo na inaunga mkono hatua hizo.

(viii) Tatizo la risiti bandia limeathiri kwa kiasi mapato ya serikali. Kwa mfano katika zoezi la kulipa ‘surtax’ ya magari lililofanyika mwaka 1994, imebainika kwamba baadhi ya wenye magari walipewa risiti bandia katika vituo vya Idara ya Mapato. Aidha, katika msako wa polisi uliofanywa katika Jiji la Dar es salaam mihuri bandia kadhaa ilikamatwa.

Tatizo hili limeenea hadi Idara ya Forodha ambapo baadhi ya watu kwa kushirikiana na watumishi wa Idara ya Forodha hasa Watunza Fedha wanatumia risiti bandia kuonyesha kwamba wamelipia mizigo hiyo na kuiondoa bandarini. Ijapokuwa idara imekuwa inachukua hatua za mara kwa mara za kukabiliana na tatizo hili bado mafanikio yake sio ya kuridhisha. Tazama Kiambatisho B.

 (ix) Baadhi ya waagizaji bidhaa wamekuwa wanafanya mipango na watengenezaji huko nje na kupewa Ankara (invoice) zinazoonyesha bei ndogo (under invoicing) ya bidhaa hizo. Hii hurahisishwa na mwagizaji kuwa na ndugu au ubia na mtengenezaji au mtengenezaji anakuwa ndiye muuzaji hapa nchini au wakala wake kutoka nje. Matokeo yake ni wafanyabiashara kukadiriwa kodi ndogo na hivyo kukwepa kulipa kodi halali. Pale wanapogundulika na kutakiwa kuongezewa kodi, hutoa rushwa ili waweze kukubaliwa kuondoa mizigo yao bandarini.

 (x) Katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam bidhaa zilizotoka nje zinatakiwa kuondolewa na wenyewe au Wakala wao  kuanzia saa 3.00 asubuhi hadi saa 9.30 alasiri isipokuwa bidhaa zenye kuharibika haraka (perfishables). Ili kuweza kuondoa mizigo hiyo baada ya saa 9.30 mteja anatakiwa kujaza Fomu C21. Wafanyabiashara wakishirikiana na watumishi wa Idara ya Polisi wamekuwa wanatumia fomu hii vibaya kuondoa mizigo Uwanja wa Ndege bila ya kulipiwa kodi kwa kisingizio kwamba ni mizigo ya Chama Tawala, Ikulu au Wizara fulani.

 Kwa mfano wananchi wa Zanzibar walieleza Tume kwamba kuna magari 25 yaliyoagizwa na mfanyabiashara maarufu wa Zanzibar kupitia Mombasa na kueleza kwamba yalikuwa ya Wizara ya Fedha Tanzania. Tume ilipofuatilia suala hili na Ofisi Ndogo ya Ubalozi wetu huko Mombasa ilielezwa kwamba kuna magari 25 yaliyotoka Dubai kwa meli ya Mv Agustino Neto kuja Mombasa tarehe 26/9/1995.

 Baadaye magari hayo yalitengenezewa ‘shipping order’ nyingine na kupelekwa Zanzibar kwa meli iitwayo Mv. Knud Jespersen tarehe 30/9/1995. Safari hii ‘Documents zote za magari hayo zilionyesha kwamba magari hayo yalikuwa ya Wizara ya Fedha Zanzibar. Magari haya yalikuwa yametumika (second hand) na inaaminika kwamba yalikuwa ya mfanyabiashara mmoja aliyetumia jina la Wizara ya Fedha Zanzibar kama mgongo wa kukwepa kulipa kodi.

 (xi) Maafisa Forodha Uwanja wa Ndege wamekuwa wanafanya mabadiliko ya udanganyifu katika nakala za mizigo (Airway bill) na hivyo kupokea rushwa kutoka kwa wateja. Mbinu zinazotumika hapa ni pamoja na Airway Bill hiyo kutolewa nakala kabla kukadiria kodi zinazotakiwa kulipwa kwa kuzingatia thamani ya bidhaa hizo (Taxable Value) ambayo inakuwa imekwisha jazwa na msafirishaji.

 Katika nakala ambayo inatumika kulipia kodi Afisa Forodha anajaza thamani ndogo ya bidhaa iliyoagizwa (Low Taxable Value) na hivyo kulipa kodi ndogo. Baadaye Afisa Forodha hugawana na mhusika kiasi cha ile tofauti ya kodi ambayo ingestahili kulipa na mizigo kuondolewa uwanjani.

 (xii) Eneo lingine ambalo lina mianya ya rushwa ni lile la abiria katika viwanja va ndege. Baadhi ya abiria wanatoa chochote kwa watumishi wa Idara ili warudipo nchini wasipekuliwe. Aidha, viongozi wenye stahili ya kutumia VIP lounge wamekuwa wanatumia fadhila hiyo vibaya kwa kuwapitisha watu wasiostahili na mizigo yao bila ya kupekuliwa na Maafisa Forodha ili waweze kulipia kodi mizigo hiyo.

 Hapana budi ikumbukwe kwamba mifuko ya mikononi (Brief cases) inaweza kubeba mali za thamani kubwa ikiwa ni pamoja na madawa ya kulevya. Kwa mfano abiria anayebeba mkoba uliojaa saa za bei ghali kama aina ya RADO 100 akipita bila ya kulipa ushuru anakuwa amepitisha mali ya karibu Shs 10,000,000/- kiasi ambacho kodi yake inazidi kodi itozwayo bidhaa za kontena moja.

 

MAPENDEKEZO:

494.  Mamlaka  ya Mapato Tanzania iandae mfumo ambao utafupisha utaratibu wa kuondoa mizigo bandarini utakaozingatia mambo yafuatayo:

 (i) Ukarabati wa Long room utakaoondoa mtindo wa watumishi wa Idara kuonana na wateja. Mteja akishawasilisha kadhia yake sehemu ya mapokezi ya Long room asiwe na nafasi ya kuiona tena, bali akaisubiri sehemu ya malipo ya ushuru na kodi ya mauzo.

 (ii) Utaratibu wa ‘Movement Sheets’ utakaoonyesha sehemu nyaraka imekwama ili ofisa anayehusika afahamike mara moja na kuchukuliwa hatua.

 (iii) Urudishaji (Rejections) wa nyaraka ambazo sio kamilifu ufanyike  baada ya kupitia sehemu zote badala ya ile ya sasa ya kufanyika sehemu moja baada ya nyingine. Utaratibu huu utapunguza ule usumbufu wa nenda rudi kwa waagizaji.

 (iv) Mpango wa kuweka na kutumia kompyuta sehemu ya Long room uharakishwe.

 495.  Idara ya Forodha itengewe fedha za kutosha ili iweze kujenga Benki ya Takwimu muhimu za bei za bidhaa zinazoagizwa nje ambao itasaidia katika ukadiriaji wa viwango sahihi vya ushuru.

496. Pale ambapo ukaguzi wa mizigo unafanyika na ikagundulika kwamba mizigo iliyoko hailingani na ile iliyoonyeshwa kwenye Bill of Lading. Afisa Forodha asiruhusiwe kuongeza kodi, bali atoe taarifa kwa Kamishna wa Forodha au Ofisa aliyekasimiwa madaraka hayo ambaye atamtaka mteja kulipa tofauti ya kodi mara moja na kufunguliwa mashtaka ya udanganyifu na ukwepaji wa kodi.

 497. Vituo vya Forodha vya mipakani vipatiwe watumishi wa kutosha ili kuimarisha udhibiti wa watumishi na mapato ya serikali.

 498. Utaratibu wa kuondoa mizigo katika viwanja vya ndege ufuatwe kikamilifu na pale ambapo mizigo inatakiwa kuondolewa baada ya saa za kazi Mkuu wa Sehemu ajulishwe na aidhinishe kimaandishi.

499. Afisa Mkadiriaji akishafanya makadirio kwa misingi iliyowekwa kisheria, wakuu wake wa kazi wasimwingilie na kupunguza kiasi cha kodi ambacho mteja anatakiwa kulipa.

500. (i) Idara ya Forodha itekeleze sheria inayoruhusu Idara kununua mizigo itakayoonekana imewekwa bei ndogo (under valued).

 (ii)Serikali itenge fungu la fedha la kutosha kwa Idara ya Forodha ili iweze kununua bidhaa zozote zitakazoonekana kama ‘under valued.’

 

MIZIGO INAYOKWENDA NCHI JIRANI (TRANSIT GOODS)

 501. Utaratibu

 Baada ya kutolewa bandarini, mizigo hii hupelekwa nchi jirani kwa kutumia fomu maalum inayoitwa ‘Road Customs Transit Documents (RCTD)’ mwenye kusafirisha mizigo hiyo hutakiwa kuweka dhamana ambayo ni sawa na kiasi cha kodi inayotakiwa kulipwa kama bidhaa hiyo ingetumika hapa nchini. Dhamana huchukuliwa na serikali ikiwa mizigo hiyo haitafika inakotakiwa.

Makasha yenye mizigo na magari ya kubeba mafuta hufungwa kwa lakiri za forodha (seals) zenye namba ili msafirishaji asije akauza mizigo hiyo hapa nchini bila ya kulipa kodi. Magari haya hutakiwa kupita katika barabara maalum ili yaweze kukaguliwa katika vituo vya Forodha vilivyoko katika barabara hizo. Gari hili linapofika kituo cha mpakani Afisa Forodha anakagua makasha ya mizigo hiyo ili kuona kama lakiri zilizowekwa hazijavunjwa. Baadaye anaweka kumbukumbu za gari hilo na kupiga mihuri katika karatasi zinazosafirisha mzigo huo na kuruhusu gari kuvuka mpaka.

Kwa upande wa kituo cha Forodha cha nchi jirani, gari hilo hukaguliwa tena na kuandikishwa kwenye vitabu vya kituo kuonyesha kwamba mizigo imeingia nchini mwao. Mzigo huo ukishamfikia mwenyewe unatakiwa kusaini ‘Lading Certificate’ ambayo inarejeshwa Idara ya Forodha katika kipindi cha miezi miwili.

502. Utaratibu wa kusafirisha mizigo kwenda nchi jirani (Transit Goods) umekuwa unatoa mianya ya rushwa pamoja na kuinyima serikali mapato kama ifuatavyo:

(i) Wasafirishai wa mizigo hususan petroli, dizeli, mitumba na bidhaa mchanganyiko (General merchandise) wamejenga tabia ya kuuza bidhaa hizo ndani ya nchi bila ya kuzilipia kodi na hivyo kupata faida kubwa. Wanachofanya watu hawa ni kwamba baada ya kuuza mizigo hiyo wanapeleka fomu ya Road Customs Transit Documents vituo vya mipakani na kwa kutoa rushwa, fomu hizo zinapigwa mihuri kuonyesha kwamba mizigo hiyo imevuka mpaka.

Mtindo huu sio hauwadidimizi wafanyabiashara wale wanaoagiza bidhaa za aina hii kihalali tu, bali  unainyima serikali mapato yatokanayo na kodi. Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli kuhusu mafuta yanayotakiwa kupelekwa nchi jirani, lakini yanauzwa humu humu nchini katika kipindi cha Juni 1994 hadi Julai 1995 umebaini kwamba kiasi cha lita 118.5 milioni ya bidhaa za petroli ziliuzwa nchini na hivyo kusababisha serikali kupoteza kiasi cha shilingi bilioni 8.1 kutokana na kutolipiwa kodi kama inavyoonyeshwa katika Kiambatisho C.

Kutokana na hali hiyo,vituo vya kuuza petroli na bidhaa za petroli katika njia kuu vimekuwa vinaibuka kama uyoga. Kwa mfano kati ya Dar es Salaam na Chalinze kuna vituo 19 vinavyouza petroli na bidhaa zake na vingine bado vinaendelea kujengwa.

(ii) Idara ya Forodha imekwa inachukua hatua za mara kwa mara za kudhibiti tatizo hili ikiwa ni pamoja na kuwafutia wateja wakorofi leseni za uwakala, lakini kwa sababu kuna ushirikiano mkubwa kati yao na watumishi wa idara wa vituo vya mipakani, inakuwa vigumu kulipatia ufumbuzi wa kudumu. Tazama Kiambatisho D.

(iii) Baadhi ya wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo kwenda nchi jirani wakifika huko mikoani huandika barua kwa Maafisa Forodha wa Kanda kuomba bidhaa hizo zilipiwe kodi ili zitumike hapa nchini kutokana na visingizio mbalimbali. Mfanyabiashara anaweza kuomba vibali mara kadhaa kwa kisingizio hicho hicho na nyakati  zote anakubaliwa.

 Mfanyabiashara huyo akishapata kibali cha kuuza mizigo hiyo hapa nchini anaonyesha mali kidogo kwa ajili ya kulipia kodi. Kwa mfano kama ana Conntainers tano analipia ushuru na kodi ya mauzo kwa container moja au mbili. Container 3 hazilipiwi kodi. Hii ni kwa sababu Maafisa Forodha wa Kanda wanapewa rushwa ili kuruhusu mizigo hiyo.

 (iv) Tume imepata mfano wa kuonyesha namna wafanyabiashara wanavyotumia mwanya wa uagizaji mizigo inayokwenda nchi jirani (transit goods) kukwepa kulipa kodi. Tume ilipokea taarifa kwamba katika Bonded Warehouse Na. 84 mali ya Mohamed Enterprises Ltd., kulikuwa na bidhaa zilizotakiwa kwenda Uganda, lakini zilikuwa zinafanyiwa mbinu ili ziweze kuuzwa hapa nchini bila ya kulipiwa kodi.

Bidhaa hizo zilikuwa mali ya Tanzania Commodities Company Ltd. Tume ilipowaita wakuu wa kampuni hiyo walidai mizigo hiyo iliingizwa nchini kupitia kwao kama wataarifiwa “notify party” kwenda Uganda na kwamba ilipofika bandarini walimkabidhi Mohamed Enterprises (T) Ltd. Walidai pia kwamba baada ya kumkabidhi Mohamed Enterprises hawajui hatima ya mizigo hiyo.

Wanasema wao hawakuagiza hiyo mizigo ila ililetwa tu na mtumaji (Shipper R. Piyarelall International PVT Ltd ya Calcutta India). “Bills of Landing” zinaonyesha mtumiwaji ni Habib Bank Ag. Zurich ya London Uingereza.

Walidai pia baada ya mizigo kupakiwa kwenye meli mwagizaji aliagiza “manifesto” irekebishwe kusomeka kuwa mwagizaji sasa ni Uganda Commodities Trading Co. Ltd ya Kampala, Uganda. Bidhaa zote zinazohusika ziliingia nchini Aprili na mwanzoni mwa Mei 1996 na zote zilijaziwa “Road Customs Transit Declaration” kuonyesha zilikuwa zisafirishwe kwa barabara kupitia Mutukula kwenda Uganda.

Tume pia imepata ushahidi kuonyesha kwamba ECCO Traders Limited wa 92 Moorgate London, EC2 P2EX walituma kwa Uganda Commodities Trading Company Ltd, bidhaa ya mchele kutoka India na sukari kutoka Thailand kama ifuatavyo:

 

1.     Mchele

(a)  Bill of Landing No. 2 (Inv. No. ETL/120019/95 Metric Tons 1,500

(b) Bill of Landing No. 4 (Inv. No. ETL/1200E/95 Metric Tons 1,000

(c)  Bill of Landing No. 5 (Inv. No. ETL/1200C/95 Metric Tons 1,000

Ingawaje mizigo hii ilikuja kwenye meli moja ilikuwa na “bills of landing” tofauti. Zote ziliondolewa bandarini tarehe 23 Aprili, 1996 na kuhifadhiwa kwenye Bonded Warehouse No. 84 mali ya Mohamed Enterprises (T) Ltd., pamoja na kujaziwa Road Customs Transit Declaration iliyoonyesha mizigo ilikuwa ikisafirishwa kwa barabara kupitia Mutukula.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 anazungumziaje eneo la sukari na wafanyabiashara katika kulipa ushuru na utaratibu unaotumika? Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonyesha upungufu ule ule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.

1648 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons