Wananchi katika Kijiji cha Nyasirori, Butiama mkoani Mara, wanalalamika kuondolewa katika ardhi yao kupisha kampuni ya uchimbaji dhahabu bila kulipwa fidia.

Wameuomba uongozi wa juu wa Serikali kufika Nyasirori kuona namna walivyoonewa na kampuni hiyo ya ZEM Co. Ltd ambayo awali iliitwa Henan-Afro Asia.

Oktoba 29, mwaka jana saa 11 alfajiri raia wa China ambao ni wafanyakazi katika kampuni ya ZEM Co. Ltd, walikamatwa wakiwa na kilo 700 za ‘makinikia’ wakisafirisha kwenda Dar es Salaam. Walitumia magari yenye namba T 641 DKJ na T636 DKJ. Suala hilo ‘limemalizwa’ na sasa watuhumiwa wote wanaendelea na kazi kama kawaida.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa wananchi wananchi watano, Simon Koru, Musa Juma, Pili Makoba, Omar Makoba na Moshi Gavana, walifungua kesi katika Baraza la Ardhi na Nyumba Musoma mwaka jana na kuushinda uongozi wa Kijiji cha Nyasirori na ZEM.

“Shaka tunayoipata ni kuona kuwa kampuni hii haitutendei haki, lakini ina uhusiano wa karibu sana na uongozi wa wilaya na hata mkoa,” amesema mwananchi akiomba jina lake lisiandikwe gazetini.

Kampuni ya Henan-Afro Asia (ambayo sasa inaitwa ZEM) iliingia Nyasirori ikidai kwamba ilikuwa ikifanya utafiti wa dhahabu katika kijiji hicho na maeneo jirani.

Juni, 2016 ilibadilisha jina na kuitwa ZEM Co. Ltd ikiwa na Sanduku la Barua 2321 Mwanza. Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwapo uhusiano wa karibu wa ZEM Co. Ltd na ofisi nyingine yenye jina la Tianyu Geological Test Center (T) Ltd zilizoko Mtaa wa Nyamongolo, Igoma jijini Mwanza.

“Walianza kuzunguka wakisema wanafanya utafiti, lakini eneo husika ni la wananchi ambao wamekuwa wakiishi, wakilima na kufuga kwa miaka mingi sana.

“Agosti 18, 2016 tangazo likatolewa kuwa wananchi wasiendelee na shughuli za kilimo na ufugaji na kuambiwa kuwa Agosti 22 mwaka huo huo wangefanyiwa tathimini waondolewe.

“Wakapima ardhi ya kila mwanchi, lakini hawakupiga picha wenye maeneo hayo kama sheria inavyotaka. Hakuna rekodi zilizoonyesha ukubwa wa ardhi inayotwaliwa, miti au mazao yaliyomo. Wao kikubwa waliandika majina tu,” kimesema chanzo chetu na kuongeza:

“Hatukupewa haki ya kujua tunalipwa nini badala yake tukalazimishwa kufungua akaunti benki, baadhi ya wananchi walipigwa makofi na maofisa wa ardhi Butiama baada ya kuhoji malipo. Tukasainishwa kwa nguvu na kupewa bahasha. Wananchi 108 walitakiwa kulipwa, lakini 10 walikataa. Wakatishiwa kwa madai wanawasumbua wawekezaji.

“Wananchi sita wakafungua kesi mahakamani. DC na viongozi wengine wa wilaya wakafika Nyasirori wakaamuru wananchi waliokuwa ndani ya uzio wa ZEM waondolewe kwa usimamizi wa polisi wa Butiama. Wananchi waliondolewa kwa nguvu, nyumba zikabomolewa, mazao yakaharibiwa. Kuna mwananchi alizuiwa kabisa kuingia ndani kung’oa mihogo yake.”

Licha ya kuwapo hukumu ya kuwataka wananchi wasiondolewe, Machi 29, mwaka jana, Ofisa Mtendaji Kijiji cha Nyasirori, aliwaandikia barua wananchi wawili – Mwita Simeu na Kwami Masibuka – akiwataka waondoe mifugo katika eneo alilosema ni la ZEM Co. Ltd.

“Kwa barua hii mnaamriwa na ofisi hii kuondoa mifugo yenu yote kutoka katika hifadhi hiyo mara moja.

“Hii inatokana na agizo la Mkuu wa Wilaya alilolitoa wakati akiwa hapa kijijini kwa ziara yake ya kikazi. Mifugo yenu kuendelea kuwa katika hifadhi hiyo ni kutaka kuleta fujo kati yenu na kampuni ya ZEM Co. Ltd bila sababu yoyote.

“Hivyo basi, kama mtapuuza agizo hili kumbukeni hatua stahiki dhidi yenu wote zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa nguvu na kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria,” alisema Mwenyekiti huyo Kabeba.

Mapema mwaka jana, aliyekuwa Kamishna wa Madini, Benjamin Mchwampaka, alimwandikia barua mmoja wa wananchi wanaolalamika, Kitamara Simeu, akisema suala la utwaaji ardhi na ulipwaji fidia ili kupisha uchimbaji madini linafanywa kisheria.

Akamweleza mwananchi huyo kuwa alishawasiliana na Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Victoria Mashariki Musoma ili kuyashughulikia malalamiko yake.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyasirori, Zablon Mkongwe, ameliambia JAMHURI kuwa suala hilo linafuatiliwa; na kwamba yeye kama kiongozi wa kijiji bado hajapata taarifa za maandishi kuhusu hatima ya mgodi huo na wananchi.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wafanyakazi katika mgodi wa ZEM wamelalamika kuwa hawalipwi mishahara na stahiki nyingine kisheria.

“Tuna miezi mingi hatulipwi mishahara, hawa wanasema wanafanya utafiti lakini mbona madini yanasafirishwa kila wakati?” Amehoji mwajiriwa mmoja.

Mwaka jana, uongozi wa ZEM ulizuia Kamati ya Kuratibu Mapato Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kuzuru mgodi huo kujionea shughuli zinazofanywa.

Katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Oktoba 31, mwaka jana, Diwani wa Masaba, Cosmas Matoka aliwalalamikia ZEM Co. Ltd kwa kukataa kusaidia maendeleo katika eneo hilo.

Mmoja wa madiwani aliyezungumza na JAMHURI amesema: “Mwaka juzi mwanzoni tulijulishwa katika vikao kuwa ZEM walikuwa katika utafiti, sasa wameanza uzalishaji, lakini wanatuzuia madiwani kujua kinachoendelea humo ndani na hakuna ushuru wala kodi wanazolipa kwa halmashauri.

“Ombi kwa Serikali – waangalie Watanzania wanaofanyakazi ZEM wapate mikataba. Pia Watanzania wapate nafasi kwani Wachina ni wengi katika mgodi huu.”

Uongozi wa kampuni hiyo haukuweza kupatikana kujibu tuhuma zinazowakabili.

Uchunguzi huu umefanywa kwa uwezeshaji wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF

By Jamhuri