Watuhumiwa Abdullah Hauga (kushoto) na Issa Haji wakiwa mahakamani kusikiliza kesi inayowakabili.

Watu wawili akiwemo Mkurugenzi wa Meli ya Lucky Shipping, Issa Haji (39) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi wa kupeperusha Bendera ya Tanzania bila kibali.

Mbali ya Haji, mshitakiwa mwingine ni mfanyabiashara Abdullah Hauga (73) ambaye ni Mkazi wa Mbezi Beach. Kwa pamoja walisomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.

Wakili Wankyo alidai washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 2 ya mwaka 2018 ambapo wametenda makosa mawili. Alidai kuwa kosa la kwanza ni kujihusisha na mtandao wa kiuhalifu ambapo walilitenda kati ya July 19,2017 na January 1,2018 maeneo ya Dar es Salaam.

Baada ya kueleza hayo, Wankyo alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, pia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) amewasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa.

Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Dismas Raphael aliiomba mahakama iwapatie dhamana wateja wake. Pia ameomba kuwasilisha pingamizi kuhusu hati ya kuzuia dhamana iliyotolewa na DPP.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi January 22, 2018 kwa ajili ya kusikiliza pingamizi hilo pamoja na kutoa uamuzi.

By Jamhuri