Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limetangaza rasmi kutoshiriki sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti, mwaka huu.

Baraza limesema litabadili msimako wake endapo ombi la Waislamu la kuingizwa kwa kipengele cha dini kwenye dodoso la sensa, litakubaliwa.

 

 

 

 

Msimamo wa Bakwata umetolewa na Amir Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Mussa Kundecha. Sina hakika kama Waislamu wote waliulizwa na kubariki msimamo huu!

Amesema katika mkutano wa viongozi wa dini na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) uliofanyika Dodoma Juni 11, waliwasilisha ombi lao la kipengele cha dini kuingizwa kwenye dodoso ili kujua dini gani ina waumini wangapi.

Kwake yeye, dodoso hilo litasaidia kuondoa utata wa sasa wa kila taasisi na dini kutoa takwimu zinazotofautiana.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira, akifunga mkutano huo, alisema kamwe Serikali haiwezi kukiingiza kipengele hicho kwa kuwa kinavunja umoja, amani na utulivu wa Taifa.

Ustaadh Sadiki Gogo, naye amesema mfano uliotumiwa na Serikali kukataa ombi la kuingizwa kwa kipengele cha dini kwenye dodoso la sensa hauna nguvu, kwa kuwa umeegemea upande mmoja na kusahau nchi kama Uganda , Uingereza , Australia na Canada , ambazo katika sensa zao wanatumia kipengele cha dini.

Hao wakitoa tamko hilo , Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania , Sheikh Ponda Issa Ponda, amesshasema atahakikisha Waislamu hawashiriki sensa hiyo iwapo Serikali haitarudisha kipengele cha dini.

Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa, amelikataa ombi la Waislamu hao la kujumuisha kipengele cha dini katika dodoso. Amewaambia kwamba suala la udini na kabila ya mtu, si mambo ya kuulizwa kwa sababu maendeleo ya nchi hayapangwi kwa kuzingatia vipengele hivyo. Jibu zuri kabisa!

Hili la kuingiza dodoso la dini likiendelea, pia kuna madai mengine ya Waislamu ya kutaka Ofisi ya Sensa iwe na watumishi nusu kwa nusu, yaani asilimia 50 wawe Waislamu na asilimia kama hiyo wawe Wakristo. Hawajawakumbuka Wahindu, Mabudha na wengine wasioamini kama huyo Bwana Mkubwa wa minguni yupo kweli!

Nimerejea maelezo haya yaliyotoka kwenye vyombo vya habari ili ndugu zangu Watanzania tuone kama kweli madai haya yana msingi wowote au ni

chokochoko za kutaka kuleta mijadala isiyokuwa na maana na tija kwa maendeleo ya nchi yetu.

Wakati Wazungu wakichimba madini na kufaidi utajiri wetu, sisi hayo tumeyaweka kando! Tumeng’ang’ana kujua nani wapo wangapi. Siamini kama kweli mawazo ya hawa watu ni mawazo ya Waislamu wote wa Tanzania .

Nimeufahamu uislamu katika matukio makuu mawili. Kwanza, ni pale nilipopata bahati ya kufanya mahojiano maaalumu na aliyekuwa Sheikh Mkuu wa Tanzania , Mufti (wa ukweli) Hemed Jumaa bin Hemed. Mwaka 1995 nilimhoji Mufti Hemed. Mahojiano hayo yalichapishwa katika toleo la pili la gazeti la MTANZANIA.

Mufti Hemed alikuwa mweledi wa hali ya juu. Alikuwa na ujuzi mkubwa mno katika elimu ya Usilamu. Aliniwezesha kutambua kuwa uislamu ni upendo, uislamu ni udugu, uislamu ni amani, uislamu ni mshikamano; na kwa jumla uislamu ni kuvumiliana.

Kwa hakika, tangu wakati huo, nikawa na mtazamo chanya kwa ndugu zangu Waislamu. Ni kwa msimamo huo, miaka kadhaa baadaye, nikawa mwanafamilia wa kwanza kumuunga mkono mdogo wangu aliyeamua kuwa Muislamu pekee katika familia yetu ya Wakristo. Baba na mama wamemuunga mkono. Mdogo wangu hadi leo anaendelea na imani yake, tena katika kuikoleza, kaamua kuwa na mke zaidi ya mmoja. Hakuna unyanyapaa wowote. Yeye leo ndiye muadhini mkuu wa msikiti kijijini kwetu. Tumemuunga mkono kwa hoja kwamba si yeye, wala sisi tulio na hakika ya dini gani ni sahihi, na ipi si sahihi. Lakini kama dini zote za mapokeo na zisizo za mapokeo zinaamini kwamba kuna huyo asiyeonekana-mwenye nguvu za ajabu, ni kwanini tujione wa dini fulani ni bora kuliko wa dini nyingine?

Pili, niliutambua vizuri uislamu nilipozuru nchi za Kiarabu, hasa Misri mwaka 2003. Nilijifunza mengi mno. Ndipo nilipotambua kwamba kuna tofauti kubwa kati ya Uislamu na Uarabu. Tunaposikia mapigano na mauaji, hilo linaweza kuwa ni tatizo la Uarabu, na si la Uislamu. Waislamu, kupitia kwa mafunzo ya Mtume S.A.W wametakiwa wawapende na washirikiane na hata wasio wa imani yao .

Jambo la tatu ambalo limenifanya niufahamu vizuri Uislamu, ni urafiki wangu na Waislamu. Sijafanya sensa, lakini nikiri kwamba idadi ya marafiki zangu Waislamu ni kubwa pengine kuliko ya wasio Waislamu. Marafiki zangu Waislamu wamenisaidia sana . Ada ya masomo yangu ya kwanza katika chuo cha uandishi wa habari nililipiwa na rafiki yangu Muislamu baada ya mwajiri wangu Mkristo kuninyima ada. Nina marafiki zangu Waislamu katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani. Wamenisaidia wakati wa raha na wakati wa shida. Wamenisaidia hata pale nilipokwama mbao au mabati ya kuezekea nyumba. Mara zote nikizungumza nao sioni wala sisikii vimelea vya ubaguzi dhidi yangu.

Ndiyo maana najiuliza, hawa kina Kundecha, Ponda na wengine, Uislamu wao ni wa aina gani? Kwanini wakomalie mambo ambayo hayana tija? Watu wazima badala ya kuhimiza ujenzi wa shule ili watoto wengi zaidi wa Kiislamu wasome, wameng’ang’ania kutaka kujua wapo wangapi. Hiyo wangapi ya udini inajenga shule? Inajenga hospitali?

Kujua idadi ya Waislamu au Wakristo katika Tanzania kunamsaidia nini mtoto wa Tanzania anayehitaji elimu na maisha bora? Kutambua kuwa Tanzania ina Wakristo kiasi gani, kutawasaidia nini kubadili hali yao ya maisha? Au kujua idadi kutasaidia vipi kuwadhibiti wezi wa mali za umma ili Watanzania wote-Waislamu, Wakristo na wapagani-wapate maisha bora?

Kudai uwiano sawa wa Waislamu na Wakristo katika ofisi ya sensa kunasaidia nini, na kutokuwapo uwiano huo kunaathiri vipi kuwahesabu Watanzania? Je, maji ya nchi hii yanasambazwa kwa kujua idadi ya imani ya watu? Elimu inatolewa kwa kujua huyu ni wa madhehebu gani? Je, ni kweli kwamba miaka michache tu baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere, misingi ya taifa hili inabomolewa kwa kasi namna hii?

Kama tumeanza kudai uwiano sawa katika sensa, tutashindwa vipi kudai uwiano sawa katika majeshi, udaktari, wauguzi, walimu na kadhalika? Lakini ni lini daktari Mkristo amekosa ajira ndani ya wizara na Serikali inayoongozwa na Muislamu? Sumu hii ikiingia katika vyombo nyeti kama majeshi, hali itakuwaje? Je , Tanzania itasalia kuwa Tanzania moja?

Wapo wanaosema kwamba Tanzania ina marais watano Waislamu, wakimaanisha kwamba kuna Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu Rais, Rais wa Zanzibar na makamu wake wawili-ambao wote ni Waislamu. Je, kuwapo kwao hao viongozi kumewakosesha nini Wakristo? Je, kuna wakristo waliokosa shule, maji, huduma za afya au kwenda kusoma ng’ambo kwa sababu marais wote watano wa Tanzania ni Waislamu?

Ninachokiona hapa ni kwamba taratibu tutafika mahali tutaanza kukubaliwa kulala katika nyumba za wageni kwa kutambuana dini zetu.

Tutaanza kudai tuwe na mochwari ya Waislamu na wengine Wakristo wawe na mochwari yao . Tutaanza kuhoji kwanini dini fulani wawe na magari mengi barabarani kuliko wa dini nyingine. Hii ni hatari kubwa sana . Tuikatae.

Ndugu zangu, bado naamini kuwa Tanzania ina Waislamu makini na wenye weledi wa hali ya juu. Hawa kina Kundecha na Ponda ni wa kupuuzwa kama walivyo Wakristo wengine wanaohubiri utengano. Hawa hawalitakii mema taifa letu.

Kama kuna Waislamu wanataka kujua wapo wangapi, waendeshe sensa kwenye misikiti yao iliyoenea nchi nzima. Kama Wakristo wanataka kujua idadi yao , wapite katika makanisa, vigango na jumuiya zao.

Nisisitize tena kuwa kina Ponda na Kundecha ni wa kupuuzwa. Waislamu makini wana kila sababu ya kuwapuuza kwa sababu si lazima kila linalofanywa Uingereza , Australia au Canada , lifanywe hapa Tanzania . Mataifa hayo kama yana kipengele cha dini kwenye dodoso la sensa zao, basi hiyo iwe kwao. Mataifa hayo yamekomaa. Hayakabiliwi na hatari ya vita ya kidini kama tulivyo sisi katika mataifa haya ambayo bado tuna kizazi kinachoabudu dini za mapokeo.

Walioanzisha Uislamu na Ukristo wanatucheka pale tunapojitahidi, ama kwa kujipendekeza, au kwa ulimbukeni wetu, kujifanya tunazijua sana dini hizo kuliko wao wenye nazo.

Hatari ya udini katika taifa letu sasa inaonekana waziwazi. Kuchomwa kwa makanisa Zanzibar ni kielelezo cha hatari hiyo. Misimamo ya kipuuzi ya kina Kundecha na Ponda ni ya kupuuzwa na Waislamu wote wa kweli.

Vyombo vya habari navyo vikiwapuuza watu wa aina hii vitakuwa vimefanya jambo la maana. Si kila yanayotapikwa na Waislamu au Wakristo wakorofi lazima yaandikwe au kutangazwa. Mengine ni ya kupuuza na kuyatupa.

Chokochoko za kuibua vita zinazofanywa na baadhi ya watu wanaojiita Waislamu na wengine Wakristo zinanifanya nitilie shaka uraia wa baadhi yao . Inawezekana wana nchi zao za asili ambazo wameshajiandalia makazi pindi moto wa vurugu utakapokuwa umeshawaka hapa Tanzania . Kwa umoja wetu, bila kujali dini zetu, tuwapuuze.

 

1060 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!